Wanafunzi Suye hatarini
na Grace Masha, Arusha
CHOO katika shule ya Msingi Suye kata ya Kimandolu jijini Arusha kiko hatarini kudidimia baada ya kuchakaa na kuta zake kuweka ufa hali inayohatarisha maisha ya wanafunzi wanaokitumia.
Hali hiyo imesababisha wazazi katika kikao chao cha Machi 30, mwaka huu, kuomba shule hiyo ifungwe mpaka kitakapokamilika choo kingine kilichokuwa kikijengwa na kampuni ya ukandarasi ya Gaimo inayomilikiwa na Meya wa jiji hilo, Gaudense Lyimo, ambacho ujenzi wake umesimama tokea mwezi Desemba mwaka jana.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Geoge Peter akizungumza na gazeti hili alithibitisha kuwepo kwa hali hiyo ambapo alisema kuwa amekuwa akiwasiliana na uongozi wa halmashauri ili kulipatia ufumbuzi hasa baada ya ujenzi huo kusimama.
Alisema kuwa mwezi Agosti mwaka jana alitoa taarifa kwenye ofisi ya mkurugenzi juu ya uchakavu wa choo hicho ambapo mhandisi wa Majengo, J. Nguvumali alifika kukikagua na kuthibitisha kwa maandishi kuwa choo hicho kimeanza kudidimia kutokana na uchakavu hivyo akaamuru wasikitumie.
Peter alisema kuwa baada ya hapo ilipatikana kampuni ya ukandarasi ya Gaimo ambayo ilianza ujenzi wa choo kingine mwishoni mwa mwezi Agosti lakini tangu mwezi Desemba mwaka jana ujenzi umesimama ukiwa umefikia hatua ya kuanza kupauliwa ambapo alipofuatilia aliambiwa anasubiri malipo ili aweze kumalizia ujenzi huo.
Alisema kuwa walikifunga choo hicho mwezi Agosti mwaka jana ambapo walimu na wanafunzi walikuwa wakitumia choo cha kimoja chenye matundu manne lakini hali ilikuwa mbaya wanafunzi walikuwa wakijisaidia kwenye maeneo mbalimbali ya shule jambo alilohofia kuwa linaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa.
Mwalimu mkuu huyo alisema kuwa ilipofika Januari mwaka huu baada ya kuona ujenzi umesimama waliamua kufungua baadhi ya vyoo hivyo ili wanafunzi wavitumie ingawa ni hatari sana lakini wanafunzi 1,042 kutumia matundu manne ni vigumu.
Kwa upande wake mkurugenzi wa jiji la Arusha, Estomih Changa, alikiri kufahamu tatizo hilo ambapo alisema kuwa kwa sasa wako kwenye mchakato wa kulishughulikia huku akikataa kuzungumzia suala hilo kwa undani.
Hata hivyo mhandisi wa majengo, Nguvumali akizungumza na gazeti hili alikiri kufahamu juu ya uchakavu wa choo na kuwa tayari kuna ujenzi wa choo kingine cha matundu 10 kitakachogharimu kiasi cha shilingi milioni 35 hadi kukamilika.
:whoo::whoo::whoo::whoo::angry: