VIKAO vya Kamati Kuu (CCM) na Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), vinatarajia kukaa wiki ijayo, huku agizo laKatibu Mkuu wa chama hicho Dk. Bashiru Ally la kumtaka ofisini kwake kada wachama hicho Bernard Membe, likiwa halijatekelezwa.
Ingawa haijaelezwa vikao hivyo vitafanyika Dodoma ama Dar es Salaam, tayari imeshatangazwa kuwa vitafanyika kwa siku mbilimfululizo, Desemba 17 na 18 mwaka huu.
Moja ya ajenda ya vikao hivyo imeshawekwa wazi kuwani uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya chama hicho kwa serikali zote mbili ya Muungano na ile ya Zanzibar.
Ikiwa imesalia miezi 12 kufikia mwaka 2020, imeelezwa kuwa chama hicho kitawasilisha ile ya mwaka 2015 hadi 2020.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanavitazama vikao hivyo kwa sura mbili, moja ikiwa ni kutathmini mwenendo wa mambo ndani na nje ya chama hicho na pili ni kushughulikia makada wao ambao wanaonekana kwenda kinyume na matakwa ya CCM mpya.
Wapo baadhi ya makada wa chama hicho ambao pia ni wabunge wamepata kunyooshewa vidole hadharani na baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho.
Miongoni mwao ni Bernard Membe (Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa), ambaye hivi karibuni jina lake liliingia kwenye mjadala mkali baada ya kutakiwa kufika ofisini kwa Dk. Bashiru ili akajieleze.
Membe ambaye bado hajatekeleza agizo hilo, ametakiwa akajieleze baada ya kuwapo kwa tuhuma za kuendesha mikakati ya kutaka kumkwamisha Rais Dk. John Magufuli.
Ilidadavuliwa kuwa nia ya Membe ni kutaka kuwania urais mwaka 2020 huku akijua wazi kuwa utamaduni wa chama hicho tangu kurejea kwa chaguzi za vyama vingi ni kuachiana kwa vipindi viwili.
Ingawa Membe hajawahi kusema chochote kuhusiana na siasa tangu uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 umalizike na yeye kuishia kwenye hatua ya tano bora, ameingia kwenye tuhuma hizo kutokana na taarifa zilizowahi kuripotiwa na moja ya magazeti ya kila siku nchini.
Hatua ya Katibu Mkuu wa chama kumtaja moja kwa moja Membe hadharani, inatafsiriwa kama hatua ya kumweka katika kona, hatua inayoweza kuibua uamuzi wa kumvua uanachama, kama ilivyopata kufanyika kwa baadhi ya makada akiwamo Sophia Simba, ambaye amesharudishwa kundini.
Wachambuzi wa mambo ya siasa wanaamini kuwa vikao hivyo vya juu vya chama, havitaweza kupita salama bila kuwagusa makada wake wanaoonekana kwenda kinyume na matakwa ya chama, akiwamo Membe.
Membe anaingia kwenye tanuru hili huku kukiwa na kumbukumbu ya kunusurika kuvuliwa uanachama mwaka 2014 baada ya kutuhumiwa kuanza kampeni mapema, yeye na makada wengine watano.
Mwaka 2014 Membe alilazimika kukaa nje ya ulingo wasiasa kwa miezi 12, akiwa pamoja na aliyekuwa hasimu wake ndani ya CCM, Edward Lowassa, Januari Makamba, Frederick Sumaye, William Ngeleja na Stephen Wasira.
Adhabu yao ilikoma mwaka 2015 na kukutwa hawanahatia, hata hivyo kwa mwenendo wa sasa wa CCM mpya, upo uwezekano mkubwa wamwanasiasa huyo ambaye jina lake limerejea kwenye siasa za mitandaoni kwa kasi akakumbana na adhabu kali zaidi itakayomweka nje ya siasa za chama chake.
Hatua ya kuitwa kwake ambayo ilionesha kuwashangaza baadhi ya wakongwe wa chama hicho, inaibua fikra za moja kwa moja kuwa mbunge huyo wa zamani wa Mtama amekalia kuti kavu ndani ya chama chake na haitakuwa rahisi kuachwa bila kupewa adhabu ya namna yoyote ile.
Watu wa karibu na Membe walithibitisha kuwa majibu aliyoyatoa kwa Katibu Mkuu wake kupitia ukurasa wake wa twitter ni yake na ni kweli atatii agizo hilo kwa kutaka aliyetoa tuhuma hizo dhidi yake naye awepo.
MZEE MWINYI AMSIHI BASHIRU
Wakati joto la Membe na Dk. Bashiru likiwa katika hali ya kupoa kidogo huku wafuatiliaji wa mambo ya siasa wakisubiri wawili hao kukutana, mwishoni mwa wiki iliyopita iliripotiwa kuwa Dk. Bashiru alikwenda kumjulia hali Mwenyekiti mstaafu wa pili wa CCM, Ali Hassan Mwinyi.
Safari hiyo iliibua mazungumzo mafupi yaliyogusa maeneo mbalimbali ikiwamo masuala ya chama na Serikali.
Mzee Mwinyi, aliyekuwa Rais wa awamu ya pili, akichukua kijiti cha uongozi wa chama na nchi kutoka kwa hayati Julius Nyerere, alikutana na Dk. Bashiru, nyumbani kwake, jijini Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine mazungumzo ya wawili hao, yanayoelezwa kutawaliwa na hekima na busara zaidi, yalijikita kwenye masuala ya maendeleo hasa ya chama na serikali kwa ujumla, zikiwamo pongezi.
Miongoni mwa mambo yaliyobeba sura ya kusihi pamoja na kuhusia yaliyozungumzwa na Mzee Mwinyi ni kumtaka Dk. Bashiru anahakikisha chama hicho kinaendelea kuisimamia serikali.
Mbali na suala la CCM kuisimamia serikali, lakini pia Rais huyo mstaafu alitaka kuimarishwa kwa nidhamu kwa hoja kuwa elimu isiyo na nidhamu inaweza kusababisha fujo kwa watoto, watuwazima na hata kwa watumishi wa umma.
Katika kudadavua hoja yake hiyo imeelezwa kuwa Dk. Bashiru aliambiwa nidhamu inasaidia kujenga na kuimarisha taifa imara na lenyewatu wenye kuheshimu kanuni, utaratibu na sheria za nchi.
Katika kuonesha kuwa anapaendezwa na mwenendo wa mambo ndani ya serikali ya awamu ya Tano, Mzee Mwinyi alisema kauli mbiu ya Rais ya kuchapa kazi ambayo dhamira yake ni kuwaletea watanzania maendeleo ibebe tija ni lazima sheria na kanuni zifuatwe.
Katika mazungumzo yao imebainishwa kuwa Dk. Bashiru alimshukuru Mzee Mwinyi kwa kuendelea kutoa mchango wake mkubwa katika kuimarisha Muungano na kukuza lugha ya Kiswahili.
Aidha aliweka wazi kuwa Mzee Mwinyi ni kiongozi wanchi aliyekuwa na mchango mkubwa katika serikali zote mbili na ameendelea kuwakumbusha, kuwashauri na kuwaombea Watanzania kila anapopata nafasi.
Tazama yote
Ripoti tatizo.
Source RAI