Chilojnr
JF-Expert Member
- Jul 5, 2012
- 302
- 1,306
- Thread starter
- #41
Sehemu hii ni ijayo....sehemu iliyotakiwa kupostiwa ni hii hapa chiniSEHEMU YA 07.
Ilikuwa ni lazima Nasria atoke ndani ya chumba hicho na kurudi nyumbani kwake lakini hakujua ni kwa namna gani angeweza kuondoka bila kugundulika. Yule mwanamke jini lilipotea na kutimka zake, lilimwacha ndani ya chumba kile huku akiwa na mwili wa Kamulika tu.
Hakujua afanye nini na kutoka, kumfuata dada wa mapokezi na kumwambia yule mwanaume alikufa chumbani kwake angeaminika kwa kuwa kweli amekufa na mwili wake kuonekana kitandani ila suala la kumwambia ni jini ndilo lililomuua, hakia kingekuwa kichekesho na kila mtu angemuona alikuwa akijitetea.
Kurudi mapokezi na kumwambia mhudumu kwamba kulikuwa na maiti lingekuwa jambo gumu sana na kitu alichokifikiria ni kuondoka chumbani humo. Kitu cha kwanza kabisa alichokifanya ni kufuta alama zote za vidole kwa kutumia kitambaa kilichokuwa na unyevunyevu.
Alifanya hivyo kwa kuwa alipenda sana kusoma simulizi za kipelelezi, pale wauaji walipokuwa wakimmaliza mtu, kitu cha kwanza kilikuwa ni kufuta alama za vidole vyao ili kuwapa kazi polisi kuwatafuta, naye alifanya hivyo.
Alipomaliza, akahakikisha hajasahau kitu, akakishika kitasa na kuufungua mlango, halafu akafuta tena alama za vidole vyake na kuanza kutembea kuelekea mlango wa nyuma. Alitaka kutoroka kupitia huko. Kwenye loji nyingi huwa na mlango wa nyuma ambao huwa mahususi kwa wazinzi wote ambao hawakutaka kuonekana mlango wa mbele, hasa wale waliokuwa wakiingia na wake za watu ama walikuwa wakifahamika sana.
Alikwenda huko, akakutana na geti, huku akionekana kutokujiamini, akalifungua na kuondoka zake, sasa akawa anatembea kwa mwendo wa haraka kutafura bodaboda. Akiwa njiani ndipo akaanza kukumbuka kilichokuwa kimetokea chumbani mule, akaanza kulia, hakika aliumizwa na hakujua lile jini lilifanya nini mpaka kumuingia.
Aliliota usiku huo, likampa mhemko mkubwa wa kufanya mapenzi, akamtafuta Kamulika lakini kilichotokea, likajitoa mwilini mwake na kumuua. Machozi yalikuwa yakilowanisha macho yake, aliumizwa moyoni, hakuamini kama alisababisha kifo cha mwanaume huyo.
Huku akiwa anaendelea kuomboleza, sasa akaanza kuwa na hofu wa watu wengine kufahamu kilichotokea, ilikuwa ni lazima watu wagundue kama yeye ndiye aliyesababisha hilo kama tu Kamulika aliwapigia simu marafiki zake usiku ule na kuwaambia alikuwa akimfuata.
“Ningechukua na simu yake!” alijisemea.
Alifanya kosa kuiacha kwani namba yake ingeonekana humo, uchunguzi wa polisi ungefanyika hata kupitia kwa simu ya Kamulika, na endapo namba yake ingeonekana, tena akiwa amempigia simu basi lingekuwa tatizo.
Alichokijua polisi wangeanza na yule mhudumu, angeelezea kilichotokea na baada ya hapo, wangetaka kumfahamu mwanamke aliyekuwa humo. Ili kumfahamu ilikuwa ni lazima kuchukua simu yake na kuangalia namba iliyoingia muda huo, ilikuwa ni lazima kuiona namba yake, angepigiwa simu na kutakiwa kituo cha polisi, endapo angefika huko na kukutana na yule mhudumu, ilikuwa ni lazima kumkumbuka.
“Nifanye nini?” akajiuliza huku akiwa na hofu.
Kurudi kule loji lilikuwa jambo lisilowezekana hata kidogo, kurudi huko ilimaanisha alikuwa akiyarudia matatizo yake, alihisi inawezekana mhudumu ama watu waliochukua vyumba vya jirani tayari walijua kilichotokea, endapo angejifanya kurudi, angedakwa na kupelekwa polisi.
“Kurudi ni upumbavu!” alijisemea.
Moyo wake ukaingia kwenye mateso makubwa na hofu nzito, hakujua ni kipi hasa alitakiwa kufanya, alijiona kuanza kupitia kwenye matatizo makubwa mno, hakutaka kufungwa jela wala kupata tatizo lolote lile, alikuwa na pesa, biashara zake, alitaka kuona zikiendelea na kuwa tajiri mkubwa.
Mwanamke jini.
Huyo ndiye aliyempa maswali makubwa, hakuwahi kuwa na jini, alisoma madrasa tangu akiwa binti mdogo tu, alishiriki kwenye shughuli zote za Kiislamu zikiwemo Maulidi lakini kote huko hakuwahi kuona ama kuambiwa alikuwa na jini, hilo jini lilitoka wapi na nini kilitokea?
Hakumfikiria mume wake wala kumuwaza kwa lolote baya, alichokijua ni kwamba walimalizana na wakati ndiyo kwanza mwanaume huyo alikuwa ameanza. Alitembea mpaka alipofika katika Barabara ya Shekilango sehemu iitwayo Sinza Makaburuni na kuita bodaboda.
Akataka apelekwe Manzese Tip Top, hilo halikuwa tatizo, akachukuliwa na kupelekwa huko kulipokuwa na klabu ya usiku. Alifanya hivyo makusudi kwa kuwa hakutaka kugundulika kabisa, bodaboda ilichukua dakika kadhaa, ikafika, akamlipa dereva na kuondoka zake.
Akasimama kwa dakika kadhaa, kulikuwa na watu wengi kiasi waliokuwa wakiendelea na mambo yao, hakutaka kujishughulisha nao sana, kwa jinsi alivyokuwa, muonekano wake kila mmoja alihisi alikuwa mmoja wa wanawake waliokuwa wakijiuza.
Akaenda mbele mpaka alipoona bodaboda nyingine na kuichukua ambayo ilimpeleka Tandale. Kila kitu alichokuwa amekifanya kilitokana na simulizi mbalimbali za kipelelezi alizowahi kuzisoma.
Kama mtu amefanya kosa sehemu na aliona baada ya hapo angetafutwa, mara baada ya kuchukua usafiri ilikuwa ni lazima kubadilishabadilisha, hilo lingewafanya hata watu kumpa kuwa vigumu.
Kwa alichokifanya, hata kama asubuhi ingegundulika maiti halafu kuifuatilia, hata kama wangempata dereva ambaye alimpeleka Manzese, angesema yeye alimpeleka huko na kuondoka kumbe mwenzake alichukua bodaboda nyingine na kumpeleka Tandale, tena si bodaboda ya eneo aliloachwa.
Alipofikishwa Tandale, akateremka na kufungua geti na kuingia chumbani kwake, sehemu ya kwanza kwenda ilikuwa ni bafuni, akaoga na kwenda chumbani. Usingizi haukuja, alikuwa na hofu tele na alikuwa akifikiria kile kilichokuwa kimetokea.
Hakika kilimtisha, hakuamini kama kwenye maisha yake siku moja angemuona mtu akifa
Je, nini kitaendelea?
Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
Ukishaisoma hiyo ya chini ndio uje hiyo ya juu. Nimejichanganya kuposti.
Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app