Dk. Slaa: Namtaka JK
Ataka mdahalo wananchi wawapime
na Kulwa Karedia
MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbrod Slaa, amemtaka mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, katika mdahalo wa kitaifa kabla ya Uchaguzi Mkuu ili taifa liwapime.
Akizungumza na Tanzania Daima mjini hapa jana, Dk. Slaa alisema hatua ya kufanya mdahalo ni fursa nzuri ya kuwaeleza Watanzania kile ambacho wamekusudia kukifanya kama watapewa ridhaa ya kuongoza taifa hili.
Niko tayari kufanya mdahalo na Rais Kikwete na wagombea wengine wa urais kwa asilimia 100. Mtakumbuka mwaka 2005 tuliandaa mdahao kama huu lakini katika hatua za mwisho Rais Kikwete alijitoa. Natarajia safari hii hawezi kufanya hivyo, alisema Dk. Slaa.
Alisema kitendo cha Rais Kikwete kukimbia mdahalo katika hatua za mwisho, licha ya mdahalo huo kuandaliwa na taasisi ya Tanzania for Center Democracy (TCD), kulisababisha Watanzania kumchagua bila kumjua vizuri.
Wahisani walijitolea kutoa fedha kupitia TCD, maandalizi yote yakakamilika, ratiba ilipangwa vizuri na mratibu wa mdahalo lakini siku ya mwisho tukaambiwa mgombea wa CCM kajitoa, alisema Dk. Slaa.
Alisema baada ya kitendo hicho, waandaaji wa mdahalo huo waligoma kuendelea bila ya kuwepo mgombea wa CCM.
Alisema moja ya faida za mdahalo huo, ni kutoa nafasi kwa wagombea wote kuwaeleza Watanzania njia ya kuondoa kero zao, na kufikisha ujumbe kwenye makundi ya watu wa ngazi za chini moja kwa moja.
Unajua siku hizi hata kule vijijini wananchi wameendelea sana , wamefunga vingamuzi vya runinga, ambavyo vinawawezesha kupata matangazo ya televisheni kila siku. Sasa kwa njia hii ni rahisi sana kusikiliza mdahalo kama huu, alisema Dk. Slaa.
Alisema mdahalo ni fursa ya kutoa hoja zilizopangilika na huwafikia wananchi wengi, tofauti na mikutano ya wanasiasa ambayo hutumika kuzungumza mambo mbalimbali katika mpangilio usio rasmi kama wa mdahalo.
Alisema hatua hiyo ni kipimo tosha kwa wagombea; hivyo hakuna sababu ya mgombea yeyote kukimbia, kwani siasa si uadui kama baadhi ya watu wanavyofikiria.
Tunakuwa na mdahalo kwa sababu tunataka kujadili mustakabali wa taifa letu. Sasa kwanini watu waingiwe na woga? Nimesikia kupitia vyombo vya habari kwamba wapo wagombea zaidi ya wanne tayari wamejitokeza kuwania urais, alisema Dk. Slaa.
Tayari taasisi ya Vox Media inaandaa mdahalo utakaowakutanisha wagombea urais wote mara kampeni zitakapoanza mwishoni mwa mwezi huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Vox Media, Ansbert Ngurumo, alilithibitishia gazeti hili kuwa maandalizi yanaendelea kuhusu mdahalo huo, ambao utahusisha vyombo vyote vya habari. Alisema taarifa kamili zitatolewa kwa umma katika siku chache zijazo.
Mbali na Dk. Slaa, mgombea mwingine aliyeomba mdahalo na JK ni Profesa Ibrahim Lipumba wa Chama cha Wananchi (CUF).
Dk. Slaa na msafara wake walipowasili mjini hapa wakitoka mkoani Mbeya kwa ajili ya kuomba udhamini wa wananchi, alipokewa na maelfu ya wananchi waliomsindikiza kuanzia Uwanja wa Ndege wa Songea hadi kwenye Uwanja wa Bombambili.
Wananchi walijipanga kando kando ya barabara, huku wengine wakiimba muda wa mageuzi umefika.
Kabla ya kufika katikati ya mji, Dk. Slaa alipokewa na wafuasi wa CCM zaidi ya 20 wakiwa wamevalia sare za chama hicho huku wakipunga mikono na kuonyesha alama ya vidole viwili, ambavyo kwa kawaida hutumiwa na CHADEMA kama salamu ya chama.
Naye mwanachama mpya wa chama hicho na mwanasheria maarufu nchini, Mabere Marando, akiwahutubia wananchi wa mji wa Songea kwenye uwanja wa Bombambili mjini hapa, alimjia juu Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba, akisema ni kiongozi asiyekuwa na ubavu wa kupambana naye kisiasa.
Mimi nawaambia mwaka huu ni mwaka wa mageuzi, licha ya baadhi ya viongozi wa CCM ambao wamekuwa wakibeza, napenda kumwambia Makamba hana ubavu wa kisiasa wa kupambana na mimi, tumejiandaa kuwashughulikia, nina majalada yao jinsi walivyoiba sehemu mbalimbali.
Nawaambia mwaka huu haitakuwa burudani kwao, watatoa machozi kwa vile tunajua wazi nani kafanya nini katika taifa hili. CHADEMA tumejipanga kikalimilifu tofauti na miaka mingine, alisema Marando.
Baada ya mkutano huo, Dk. Slaa alikwenda Mtwara ambako alihutubia mkutano mkubwa kwenye Uwanja wa Umoja, akawataka wananchi wa mkoa huo kubadilika kwa kuchagua viongozi kutoka kambi ya upinzani.
Wana Mtwara tangu mfumo wa vyama vingi umeingia nchini, mkoa huu hamjawahi kuchagua mbunge hata mmoja wa kambi ya upinzani
. Umefika wakati sasa wa kukaa chini na kutafakari kwa kina, chagueni wabunge kutoka upinzani, alisema Dk. Slaa huku akishangiliwa. Leo Dk. Slaa anatarajia kuwasili katika mikoa ya Morogoro na Kilimanjaro kwa ajili ya kuendelea kuomba ridhaa ya wananchi kumdhamini ili kupata sahihi za wananchi zitakazomwesha kugombea urais.