Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 4,783
- 14,975
Akijibu hoja iliyoibuliwa na Mwandishi wa Habari kwenye kikao maalumu baina ya Ofisi ya Msajili wa Hazina na wahariri, kuhusu changamoto ambayo imekuwa ikijitokeza kwa nyakati tofauti kwa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kushindwa kuzingatia muda na ratiba za safari, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu amesema Kulikuwepo na changamoto za kiufundi lakini zinapatiwa ufumbuzi.
Akizungumza Juni 2, 2025 Jijini Dar es Salaam, Mchechu amesema kuna changamoto kidogo zilikuwepo ikiwemo kukosekana kwa baadhi ya ndege ambazo amesema zimerudi pamoja na mabadiliko ya uongozi.
Aidha, katika jitihada za kuongeza ufanisi zaidi Mchechu amesema kwamba wapo katika mchakato wa kuona uwezekano wa kufanya mgawanyo wa kiutendaji kwa kuanzisha mamlaka rasmi zitakazokuwa na jukumu la kushughulika na miundombinu huku nyingine ikishughulika na uendeshaji (Infrastructure Board & Service Board).
Amesema kuwa wanawaza namna ya kufanya hivyo kwenye baadhi ya Taasisi za kiserikali ikiwemo ATCL, TRC ili kuongeza uwajibikaji zaidi.
Ikumbukwe Msajili wa Hazina ana mamlaka ya kusimamia shughuli zote, rasilimali zote za mashirika ya umma, taasisi na wakala wa serikali, kupitia matumizi ya pesa katika mashirika ya umma na yaliyoundwa kisheria kwa lengo la kupendekeza hatua zinazolenga kuunganisha, kuvunja au kuboresha utendaji wake.