SHIRIKISHO la Soka Tanzania, TFF,
limesema klabu ya Simba inaweza
kufanya lolote kwa Mbwana Samatta
kwa kuwa ni mchezaji halali wa klabu hiyo.
Kauli ya TFF imekuja baada ya African
Lyon kutaka simba iwape fedha zote
za usajili wa mchezaji huyo aliyeko
katika majaribio nchini DR Congo.
Simba ilimchukua mchezaji huyo kutoka African Lyon.
Lyon waliibuka baada ya klabu ya TP
Mazembe ya DR Congo kumnunua
mchezaji huyo kwa dola 100,000
(sh150mil) ambazo Simba
imekubaliana na Mazembe huku African Lyon wakidai kuwa fedha hizo
hazikustaili kwenda Simba kwa kuwa
mchezaji huyo alienda Simba kwa
mkopo.
Mwenyekiti wa kamati ya Mashindano
ya TFF, Saad Kawemba alisema kuwa kwa upande wao hawana mkataba
wa African Lyon na Samatta bali wana
nakala ya mkataba wa Simba
unaoeleza kuwa Samatta ni mchezaji
wao halali.
Alisema kama mchezaji huyo angekuwa sio halali kamati hiyo
ingeinyang'anya Simba pointi zote
ambazo walipata katika michezo yote
ambayo Mbwana alicheza kwa mujibu
wa kanuni zinavyoeleza.
Alisema na kama mchezaji huyo asingekuwa halali na kama usajili
wake ungekuwa na mashaka basi
Simba isingeruhusiwa kumtumia
mpaka pale watakapomalizana na
klabu husika ambayo mchezaji huyo
katoka. Wakati hayo yakiendelea kushika
kasi, Vicky Kimaro anaripoti kuwa
uongozi wa Afrika Lyon unapanga
kulifikisha suala lao Shirikisho la Soka
bAfrika (CAF) na lile la kimataifa, FIFA
kutokana na kutumia ubabe kumuuza mchezaji wao.
Akizungumza na Mwananchi kiongozi
wa juu wa klabu hiyo alisema mbali na
Simba pia wataishtaki TFF kwa kitendo
chao cha kupuuza barua zao za
malalamiko walizowaandikia TFF mwaka jana.
"Hakuna mkataba wowote kati ya
Afrika Lyon na Simba ambao
ulikubaliana Samata na Rashid Gumbo
kuichezea Simba, hakuna hata mali
kauli si uongozi wetu wala ule uliopita, na hili suala tuliwaandikia TFF barua
kama nane hizi hapa,(alionyesha)
wakati Kayuni anakaimu nafasi ya
katibu mkuu lakini hakuna hata moja
aliyoifanyia kazi,"alisema kiongozi
huyo "Tangu tumeichukua Afrika Lyon
tumekuwa tukiwandikia TFF barua
mara kwa mara kuwakumbusha
kuhusu wachezaji wetu, chochote
kitakachotokea tusibebeshwe lawama
na kesho (leo) tutaweka wazi mikataba ya wakina Samata na barua
zote ambazo tuliwaanindikia TFF na
hawakuchukua hatua yoyote,"
alisema.
Hata hivyo, habari zilizopatikana
baadaye jana jioni zilisema kuwa Katibu Mkuu wa Lyon, Brain Ernest
alisema kuwa wanachodai Simba ni
fedha za usajili ambazo klabu hiyo
haikumalizia katika usajili wake.
Katika hatua nyingine viongozi wa
Simba wameanza kufanya mazungumzo na mshambuliaji wa
Yanga, Samte Ally ili aweze kuichezea
Simba msimu ujao wa ligi kuu
Tanzania bara.
Habari ambazo zilipatikana jana
kutoka kwa moja wa viongozi wa Simba zilieleza kuwa Kamati hiyo ya
usajili imeanza mazungumzo na
mchezaji huyo tangu wiki iliyopita
lakini kumekuwa na kutokubaliana
kwa baadhi ya wajumbe wa kamati
hiyo wakidai kuwa mchezaji huyo amekuwa na utovu wa nidhamu kwa
muda mrefu.
Mpaka sasa Simba imekwishanasa
saini za Obadia Mungusa, Mwinyi
Kazimoto,salum Machaku na Patrick
Mafisango, Godfrey Katerega (Atraco) na Ulimboka Mwakingwe.