Mbuzi wa Moshi hakaribishi Noeli | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mbuzi wa Moshi hakaribishi Noeli

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Felixonfellix, Apr 30, 2010.

 1. Felixonfellix

  Felixonfellix JF-Expert Member

  #1
  Apr 30, 2010
  Joined: Feb 16, 2010
  Messages: 1,680
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 135
  Rai ya Jenerali


  [​IMG][​IMG]
  Jenerali Ulimwengu​
  Aprili 28, 2010[​IMG]
  NI bayana kwamba mwaka huu wote utakuwa na heka heka za kila aina kutokana na uchaguzi mkuu, na tayari heka heka zimekwisha kuanza. Tutazishuhudia kwa wingi na uzito mkubwa zaidi kadri tunavyokaribia uchaguzi wenyewe mwezi Oktoba.
  Yapo mambo mengi ambayo hatuna budi kuyaangalia kwa makini kwa sababu yanao uwezo wa kuvuruga mchakato mzima wa uchaguzi na kuufanya uchaguzi upoteze maana yake. Kumbuka, nimeeleza mara kadhaa kwamba uchaguzi unatakiwa utambulike kama asasi takatifu, na jambo lo lote linalouchafua linautia najisi.
  Baadhi ya mambo yamejadiliwa kirefu na wakati mwingine yameonekana kidogo kama mzaha. Hapa nafikiria ile sheria ambayo ilipitishwa na Bunge ili kudhibiti matumizi ya fedha katika uchaguzi. Haitoshi kwamba muswada umepelekwa bungeni, ukapitishwa, ukatiwa saini hadharani, kisha ikagundulika kwamba vifungu fulani ndani ya muswada “vilichezewa” kabla Rais wa Jamhuri hajautia saini.
  Sasa, inaelekea muswada huo, ambao umekwisha kuwa sheria umezua malumbano makali na hali ya kutoelewana baina ya wabunge na asasi za serikali, kama vile ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Inavyoelekea, ni kama vile wanasiasa hawajakubali suala la msingi kuhusu udhibiti wa matumizi ya fedha katika kampeni.
  Hili ni jambo la msingi na ambalo kama halikuangaliwa kwa makini litazifanya chaguzi zetu zipoteze maana kwa sababu zitakuwa zimeingia ile najisi niliyoizungumzia mapema, na hiyo ni hatari ambayo wanasiasa wetu wanajifanya hawaioni ingawa i wazi kabisa.
  Hebu tazama: Hata leo tunaendelea kusikia taarifa za wizi unaojulikana kwa kifupi kama EPA. Madai ni kwamba fedha nyingingi zilichotwa kutoka Benki Kuu (BOT) mijali ya kusaidia chama tawala kishinde uchaguzi miaka mitano iliyopita. Wanatajwa watu wakubwa, watu waliokuwa na dhamana kubwa ndani ya serikali kama wahusika wakuu wa wizi huo.
  Hadi leo hakuna hata mmoja wa hao wakubwa aliyekwenda jela, ingawaje kw muda fulani tuliambiwa kwamba wezi hao walikuwa wameanza “kurejesha” fedha walizoiba. Hivi sasa hatusikii tena iwapo “urejeshaji” huo unaendelea au vipi, na wala hatujapewa jedwali la kuonyesha ni kiasi gani kimerejeshwa hadi leo.
  Shughuli imekuwa ni “funika kombe mwanaharamu apite” kwa imani kwamba mwanaharamu akiisha kupita tutafunua kombe letu tuendelee kula kama awali. Kwa bahati mbaya (kwa wanakombe hawa) mwanaharamu huyo ni mwananchi anayeguswa na wizi huu kwa sababu ni wizi unaomnyima haki yake ya kuchagua, mbali na kwamba ni wizi wa kawaida pia. Na huyu mwanaharamu hapiti, kwani hapa ni kwake na hana safari ya kwenda ko kote.
  Kwa hiyo mwanaharamu huyo atauliza maswali kuhusu hicho kinachofichwa ndani ya kombe hilo lililofunikwa. Atataka lifunuliwe ili ajionee mwenyewe. Wanakombe watakataa, watamwekea vizingiti ili asipate kujua undani wa kombe hilo, lakini atang’ang’ania kujua, na hatimaye mwanaharamu huyo atajua ni nini kilichomo ndani ya kombe hilo.
  Michezo tunayocheza ni michezo ya hatari, na tunaendelea nayo kana kwamba nchini hapa sisi ni watalii na baada ya muda kidogo tutaondoka na kurudi makwetu, wapi sijui. Ndiyo maana tunafanya mambo ya hovyo, labda kwa kuamini kwamba bomu likija kulipuka sisi tutakuwa hatupo. Lakini wakati huo huo tunazaa, na wanetu nao wanazaaa, nasi tunasema tunawapenda.
  Hebu tuache maskhara, tuachane na utani huu ulio ghali. Huwezi kuwa unakabiliwa na kelele za ‘mwizi, mwizi !’ zikiwatuhumu wakuu wa asasi za dola, pamoja na mkuu wa nchi mstaafu, halafu ukajifanya husikii, huoni, hunusi wala huhisi. Huwezi kuwa unazungumzia udhibiti wa matumizi ya fedha katika uchaguzi huku unaruhusu sheria ya kuelekeza udhibiti huo inachokonolewa na watu wasiohusika, halafu hakuna anayewajibika, na shughuli ni kama kawaida.
  Huwezi, nasema, huwezi kuleta maana hata machoni mwa watoto wa shule ya msingi iwapo wafanyakazi wako wanaazimia kugoma kwa madai ya nyongeza ya kamshahara kidogo tu, wewe unawaomba wawe wavumilivu na huku unasema utatumia shilingi bilioni 50 kwa ajili ya kampeni za urais, na bilioni nyingine kadhaa kwa kampeni ya ubunge na bilioni nyingine tena kwa ajili ya udiwani, na bilioni nyingine tena…..
  Ni dhahiri katika hali kama hii kwamba kinachogomba hapa si sheria bali ni mantiki. Sheria zinaweza kutungwa na wahuni na wahuni hao hao wakawa ndio wasimamizi wa utekelezaji wake, na wakahakikisha kwamba hata kile kidogo kilichobakizwa ndani ya sheria hizo hakitekelezeki
  Jaji mwandamizi mstaafu amenisaidia majuzi katika kulielewa hili. Anasema kwamba sheria za kudhibiti uhalifu hutungwa kwa uelewa kwamba wahalifu watakuwa ni wachache sana katika jamii au asasi, na kwamba watu walio wengi watakuwa ni watiifu kwa sheria na mamlaka. Anasema ukikuta hali ambamo walio wengi wameegemea katika uhalifu na kutotii sheria na mamlaka, sheria yo yote inayotungwa kudhibiti uhalifu inakuwa haina maana.
  Kama tunavyoshuhudia hivi sasa sheria ya aina hiyo inazaliwa ikiwa imekufa. Binafsi sina shaka kwamba hii sheria ya kudhibiti matumizi ya fedha imekwisha kufa kabla hata haijazaliwa, kwa sababu wanasiasa wahuni hawaitaki, na wao ndio wenye nguvu nchini humu.
  Tutapata wasaa wa kuichnguza kwa karibu zaidi mara itakapochapishwa (kama itasambazwa) na tutajionea wenyewe ni kwa kiasi gani itafanikiwa kufanya hicho inachotarajiwa kufanya. Matumaini yangu si makubwa sana kwa sababu sipati ushahidi wa utashi wa kisiasa.
  Ni utashi huu wa kisiasa ambao tunahitaji kuujenga kwa nguvu zetu zote, si miongoni mwa wanasiasa hawa matapeli (mbuzi wa Uchagani haikaribishi Krismasi) bali miongoni mwa wananchi ambao ndio wahanga wa utapeli huu.
  Naamini kwamba asasi zisizo za serikali zinaweza kufanya kazi hii ya kuhamasisha umma uzinduke na uachane na matapeli hawa ili uweze kuchagua wawakilishi na viongozi wa kweli. Inawezekana.
   
 2. Lekanjobe Kubinika

  Lekanjobe Kubinika JF-Expert Member

  #2
  Apr 30, 2010
  Joined: Dec 6, 2006
  Messages: 3,067
  Likes Received: 18
  Trophy Points: 135
  Nammaindi sana Ulimwengu, kapitia misukosuko mingi kutokana na mkono wake huo wenye kushika kalamu na mdomo ulioficha ulimi wake.
   
Loading...