Dotto C. Rangimoto
JF-Expert Member
- Nov 22, 2012
- 1,985
- 1,286
Uchaguzi wa ngazi ya taifa ndani ya CHADEMA umeshabisha hodi. Hodi hiyo watoa paruwanja vijana 10,000 wa CHADEMA hadi sasa wameshasaini waraka wa kumtaka Mbowe agombee uenyekiti wa CHADEMA. Aidha vijana hao wanataka kuchanga fedha kwa ajili ya kumchukulia fomu bwana Mbowe.
Hili si jambo zuri kwa sababu zifuatazo.
Mosi.
CHADEMA ni chama kinachojipambanua kama mabadala mzuri wa CCM. Kwa kujipambanua huku kinatakiwa kuwa mfano na kigezo chema kwa vyama vingine.
CHADEMA iko katika vita ya kuihami demokrasia inayokanyagwa na uongozi wa Magufuli. Kitendo cha Mbowe kuendelea kuwa mwenyekiti wa CHADEMA kwa vipindi vingi si kitendo cha kidemokrasia. Sasa chama ambacho ndani kwake hakuna demokrasia kinawezaje kuongoza vita ya kuitetea demokrasia?
Pili.
Hivi sasa kuna kundi ndani ya CCM lina mkakati wa kumfanya Magufuli kuendelea kuwa Rais hata baada ya kumaliza vipindi vyake viwili. Kundi hili linapendezwa na mambo mengi anayoyafanya Magufuli na wanataka aendelee zaidi kuwa madarakani ili azidi kufanya hayo mazuri.
Hili kundi la CCM lazima tupambane nalo na tunataraji CHADEMA kuongoza mapambano hayo. Hata hivyo CHADEMA itakuwa na uhalali gani wa kuongoza mapambano hayo ikiwa ndani mwao kuna kundi la watu linalompenda Mbowe kiasi cha kumtaka awe mwenyekiti wa milele? Hivi hatuoni kitendo cha Mbowe kukubali matakwa ya kundi hili ndio kulipa uhalali kundi la CCM kufanya hivyohivyo kwa Magufuli? Mbowe kemea hawa BAVICHA wasiojitambua.
Tatu
Mwanzoni katiba ya CHADEMA ilikuwa na kipengele cha ukomo wa uongozi lakini kikaja kutolewa kwa marekebisho ya katiba yaliyofanyika mwaka 2006.
Mwaonaje tujikumbushe sababu zilizopelekea kufanyika marekebisho hayo mwaka 2006? Kipindi hicho hasa mikoani wanachama walikuwa hawajitokezi kugombea na wale viongozi waliokuwepo kushindwa kuendelea kugombea baada vipindi vyao viwili vya kuongoza kuisha kutokana na kikwazo cha kikatiba.
Ndipo hapo CHADEMA ikaondoa ukomo wa UONGOZI kwenye katiba yake ili kuruhusu viongozi walioko madarakani kuendelea kugombea hata zaidi ya vipindi viwili. Madhumuni hasa ni kuondoa hatari ya nafasi za uongozi huko mikoani kuwa wazi na kukosa wa kuzishika kikatiba.
Sasa tujiulize CHADEMA bado chama kichanga? CHADEMA bado haina watu kugombea kiasi iendelee kuacha watu kushika nyadhifa moja za chama kwa vipindi zaidi ya viwili? Namaanisha zile sababu zilizopelekea CHADEMA kufuta UKOMO WA UONGOZI katika KATIBA yake zingali zipo? Ni dhahiri hazipo, na mbaya zaidi wabakaji wanatumia huo mwanya kuibaka demokrasia. Hili si sawa, Mbowe kemea hao.
Nne.
Nini tafasiri ya Mbowe kuendelea kuwa mwenyekiti wa CHADEMA? Tafasiri yake kubwa ni moja tu. Ndio ni moja na si nyingine ila kufeli kwa Mbowe kujenga mfumo madhubuti wa kuzalisha viongozi ndani ya chama.
Hii ina maana kwa muda wa miaka kumi na tano ya uongozi wake, Mbowe ameshindwa kujenga chama chenye wanachama wenye uwezo wa kushika wadhifa wa uenyekiti wa chama taifa. Kama ameshindwa kuzalisha wanachama wa namna hiyo ni dhahiri hafai kuendelea kuwa mwenyekiti.
Kama tafasiri hiyo ina kigegezi huenda hii ikawa mujarabu. Pengine Mbowe hakushindwa kujenga mfumo huo, sema tu ana atabia kujiona kuwa yeye ndiye peke mwenye uwezo mkubwa wa kukiongoza na kukivusha chama katika nakama mbalimbali.
Tabia hii ni ya kidikteta, kama ni vibaya kuwa nayo Rais wetu pia si vizuri kuwa nayo kiongozi yeyote ndani ya vyama vyetu. Maana Rais wetu hatoki popote ila ndani ya vyama vyetu. Nani wa kumkemea Mbowe huko CHADEMA?
Tano.
Kuna hoja ya kitoto ya wanaotetea Mbowe kuendelea kuwa mwenyekiti. Ati wanasema CCM wanataka kuwawekea mamluki kwenye chama chao.
Hawa watu lazima kwanza wajue. Ndio wajue si kwamba ndani ya chama chao hakuna wasiotaka Mbowe kuendelea kuwa mwenyekiti. Wapo. Tena wengi tu; sema sauti zao zinamezwa na hanikizo la sauti za sarafu zinazoangushwa na Mbowe kwa makusudi kwenye makorido na kumbi za CHADEMA. Maana uchao huko kwasikika, njenjele njenjele; sasa hizo njenjele katu haziwezi kuruhusu sauti zilobeba neno "HAPANA" kusikika, labda na kusikilizwa, pengine na kuheshimiwa.
Zaidi hawa wasiotaka Mbowe kuendelea kuwa mwenyekiti sababu yao si kwamba Mbowe kuna mahala kaharibu, hapana, sababu yao hasa ni Mbowe kukalia wadhifa huo kwa muda mrefu. Na kwanini hasa iwe hivyo kama chama kampuni yake?
Aidha lazima hawa wenye hoja hii ya kitoto wajiulize. Hivi Mnyika, Lissu, Prof Safari, Salimu Mwalimu, Heche, Mdee, Msigwa, na hata Wenje hawa ni mamluki wa CCM? Kama sio hawafai kupokea kijiti cha Mbowe na kuendeleza pale alipoishia? Kutumikia kwao kote hakujawafanya waaminike? Kama hawa hawaaminiki nani huko CHADEMA mwenye kuaminika? Nani hasa hupewa jukumu la kuwaamini wanachama? Mbowe? Mtei? Au vikao vya chama?
Mathalani nani asiyeijua BAVICHA ya Heche? Ilikuwa madhubuti kwelikweli. Kwanini nyie BAVICHA musimchukulie fomu huyu Heche na kumshawishi agombee? Huenda watu niliowataja hapo wana kwingi kusita katika kumkabili Mbowe, lakini likitokea kundi la kuwashika mikono huenda watathubutu kuchukua fomu na kugombea.
Au ndio mnamuacha Mbowe aweke makanyaboya wa kushindana naye ili kutuhadaa watu wazima na ndevu zetu?
Sita.
Uzuri wa kuongoza ni kutoka uongozini ilihali watu wanakupenda. Mbowe anapendwa na wanachama. Huu ndio wakati kung'atuka akiwa bado yuko nyoyoni mwa wanachama. Wanachama wamng'ang'anize kama hivi na kisha naye aseme, "yatosha aje mwengine kukalia kiti."
23/11/2019
Dotto Rangimoto
NjanoTano
0762845394
Morogoro