BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,789
- 288,015
Mbowe amvaa Kikwete
Ambeza kutangaza kufunga mjadala wa Dowans
Ambeza kutangaza kufunga mjadala wa Dowans
na Edward Kinabo
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amemtaka Rais Jakaya Kikwete, kutofunga mjadala wa suala la mitambo ya kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura, Dowans, bila kuwaeleza wananchi ukweli kuhusu wamiliki wake na mahala walipo.Tanzania Daima~Sauti ya Watu
Mbowe aliyasema hayo jana katika mahojiano maalum na Tanzania Daima, akitoa maoni yake kuhusu baadhi ya masuala aliyoyazungumza Rais Kikwete juzi usiku, wakati akilihutubia taifa kwa njia ya redio na televisheni.
Alisema hatua ya Rais Kikwete kutangaza kufunga mjadala wa Dowans ni ya kuungwa mkono kwa kuwa mjadala huo si jibu la matatizo ya umeme nchini, lakini alimtaka kwanza awaeleze Watanzania ukweli wote kuhusu Kampuni ya Dowans, ndipo aufunge mjadala huo vizuri.
Tunakubaliana na ushauri wake wa kutaka mjadala wa Dowans uishe. Tunakubaliana naye kwa sababu Dowans si jibu la matatizo ya msingi ya sekta ya nishati nchini. Hata hivyo, Kikwete asikimbilie kufunga mjadala bila kuwaeleza wananchi, Dowans ni nani. Watoe tamko, waueleze umma wa Watanzania, wamiliki wa Dowans ni nani, wako wapi, wanafanya nini, wataje watu wote wanaonufaika na Dowans, kisha ndipo atufungie mjadala huo vizuri. Kikwete anataka kuficha ukweli, alisema Mbowe.
Akizungumzia tatizo la uhaba wa umeme nchini, alisema si mara ya kwanza kwa Rais Kikwete kuahidi kumaliza tatizo la umeme, kwani wakati wa sakata la kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond, alishaahidi kuwa tatizo la umeme lingekuwa historia.
Si mara ya kwanza rais kuahidi kwamba nchi haitakuwa gizani. Ameshaahidi hivyo wakati wa vuta nikuvute ya Richmond, ameshasema hivyo karibu mara tatu. Alishasema kwamba matatizo ya umeme yatakuwa historia, lakini hadi leo nchi haina umeme wa uhakika. Rais anaendelea kutoa maneno matamu, hatuwezi kupata umeme kwa maneno yake .
Asitazame tu uchaguzi wa 2010, na kuwapa watu maneno matamu, atazame mbele. Tunahitaji mkakati wa muda mrefu na mfupi. Na si mkakati tu, tunahitaji mpango wa utekelezaji, maana sera ya nishati imeainisha yote hayo, lakini tatizo utekelezaji. Serikali inapaswa kuwa na uhakika wa kulipatia taifa umeme hata kwa miaka zaidi ya 50 ijayo, alisema Mbowe.
Alisema kwa kiasi kikubwa sekta ya umeme nchini inaathiriwa na wafanyabiashara wakubwa ambao ni maswahiba wa Rais Kikwete na Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaoigeuza sekta hiyo kuwa chanzo chao cha mapato, kwa kuanzisha kampuni za kufua umeme wa dharura na kuiuzia TANESCO kwa gharama kubwa.
Alisisitiza kuwa, msingi wa tatizo la nishati ya umeme nchini ni kutokuwapo kwa sera endelevu na mikakati yakinifu na inayotekelezeka, ya muda mrefu na mfupi, ya kuzalisha na kusambaza umeme.
Alisema pamoja na uhaba wa umeme unaozalishwa, bado sehemu kubwa ya umeme huo imekuwa ikiibwa na kusababisha wananchi wengi kukosa haki ya kupata umeme.
Na tatizo hapa si uhaba wa umeme unaozalishwa tu. Bado kuna umeme mwingi sana unaibwa, lakini serikali halizungumzii hili, alisema Mbowe.
Alisema tatizo jingine ni umeme unaozalishwa kuwa wa gharama kubwa kiasi cha wananchi wengi kushindwa kuupata na kuutumia.
Tuna network (mtandao) kubwa sana ya umeme. Maeneo mengi nyaya za umeme zinapita jirani na nyumba za watu, lakini wenye uwezo wa kuunganisha umeme huo kwenye nyumba zao ni wachache sana. Gharama za kufunga umeme majumbani ni kubwa mno kwa Mtanzania maskini kumudu. Gharama za kuutumia, kulipa ankara pia ni kubwa.
Kwa hiyo Rais Kikwete na serikali yake, wasiishie tu kuzungumzia uzalishaji, lakini pia lazima waeleze ni jinsi gani watapunguza gharama za umeme ili Watanzania maskini nao waweze kuutumia, alisema Mbowe.
Akizungumzia tahadhari ya Rais Kikwete, kwamba kwenye baadhi ya mikoa kuna uwezekano wa kutokea tatizo la chakula kwa sababu ya kuchelewa kwa mvua za masika, Mbowe alisema ni aibu na fedheha kubwa kwa nchi yenye maji mengi yanayotiririka kama Tanzania, kutangaza njaa ndani ya msimu mmoja wa matatizo ya mvua.
Sikio la kufa halisikii dawa. Tatizo la chakula ni tatizo la kujitakia. Kukosa mvua msimu mmoja, halafu rais anatangaza njaa, ni jambo la kutia aibu sana. Tuna maji mengi sana yanatiririka, tuna mito na maziwa, ardhi yenye rutuba nzuri sana. Tuna kila kitu, tatizo ni ukosefu wa sera nzuri na uongozi bora, alisema Mbowe.
Alisema Rais Kikwete anapaswa kumfukuza mara moja Waziri wake wa Kilimo na Chakula kwa kushindwa kusimamia programu za kilimo cha uwagiliaji nchini.
Walipoingia madarakani walikutana na tatizo la chakula. Kikwete na Lowassa waligawa chakula na kuahidi kwamba njaa ile isingetokea tena, sasa leo wanatuambia nini? Wamefanya nini? Na hii ndiyo kawaida yake, anaahidi halafu anasahau. Nchi hii ikipata viongozi wazuri serikalini, kilimo cha umwagiliaji kinaweza kabisa kumaliza tatizo la njaa za mara kwa mara, alisema Mbowe.
Alisema serikali inapaswa kuwa na mpango wa makusudi wa muda mrefu wa kuzalisha na kuhifadhi chakula kwa wingi, ili kiwe kinaingia katika mtandao wa matumizi ya wananchi, pindi kunapokuwa na uhaba wa chakula.
Katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi uliopita, Rais Kikwete pamoja na mambo mengine, alitaka mjadala wa kununua au kutonunua mitambo ya Dowans, ufungwe baada ya wahusika (TANESCO), kutangaza kuachana na uamuzi wa kutaka kuinunua.
Alisema anashangazwa na malumbano ya baadhi ya viongozi wa siasa kuhusu jambo hilo.
Mjadala wa Dowans, hivi karibuni uliwaingiza katika malumbano makali, Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, wote wa CCM.