neema shamuhenya
JF-Expert Member
- May 24, 2018
- 312
- 216
WAKATI uhusiano wa kibiashara baina ya Kenya na Tanzania ukirejea katika hali yake ya kawaida baada ya nchi hizo kutafuta mwarobaini wa mgongano wa kibiashara, mauzo ya bidhaa za Kenya nchini Tanzania, yamepanda kwa kasi kubwa ndani ya miezi mitano.
Julai 5 mwaka huu, Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Tanzania, Profesa Elisante Ole Gabriel na mwenzake wa Kenya, Dk Chris Kiptoo walikutana na kufikia maazimio kadhaa yaliyozika dosari zilizotajwa kudumu kwa muda mrefu.
Walikutana kutekeleza maagizo ya marais, Uhuru Kenyatta wa Kenya na Dk John Magufuli wa Tanzania.
Kutokana na muafaka huo, taarifa inaonesha kuwa Tanzania iliagiza bidhaa zenye thamani ya Sh za Kenya bilioni 10.54 kati ya Januari na Mei mwaka huu, likiwa ni ongezeko la asilimia 28.58 ikilinganishwa na mauzo ya mwaka jana katika kipindi kama hicho.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Taifa la Takwimu Kenya (KNBS) iliyotolewa hivi karibuni.
Wakati Kenya ikinufaika kwa kuingiza Tanzania bidhaa zenye thamani kubwa, Pakistan imeendelea kuwa mnunuzi namba moja wa bidhaa za Kenya hasa chai, kwa kuagiza bidhaa zenye thamani ya Sh za Kenya bilioni 23.7, likiwa ni anguko la asilimia 7.11 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.
Aidha, Uholanzi ambayo kwa kiasi kikubwa huagiza maua imekuwa ya pili, kwani manunuzi yake yameongezeka kwa asilimia 13.45 kwa kununua bidhaa zenye thamani ya Sh bilioni 21.65.
Uganda imeshuka hadi nafasi ya tatu kwa ununuzi wa bidhaa za Kenya, kwani imenunua bidhaa za Sh bilioni 21.31 hivyo kushuka kwa asilimia 2.76.
Waagizaji wengine wa bidhaa Kenya ikiwemo Uingereza, imeipiga Marekani na kushika nafasi ya nne kutokana na kuagiza bidhaa zenye thamani ya Sh bilioni 17.57 sawa na ongezeko la asilimia 12.93. Marekani iliagiza bidhaa za Sh bilioni 17.13.
Rais Kenyatta na Rais Magufuli, Februari mwaka jana waliziagiza mamlaka katika nchi zao kuhakikisha zinaondoa ukiritimba na migogoro ya kibiashara baina ya nchi hizo. “Tunaendelea vyema. Tumeondoa dosari na sasa tumeboresha sana uhusiano kati ya nchi zetu, yaani Kenya na Tanzania.
Pia tuna mawasiliano ya karibu sasa, mambo ni mazuri,” alisema Dk Kiptoo.
Profesa Gabriel hakupatikana kuzungumzia kwa undani suala hilo, ingawa alishawahi kusema kuwa, wanahangaika kutafuta suluhu ya kudumu ya tofauti za kibiashara kati ya nchi hizi mbili jirani na wanachama wa jumuiya inayokua kwa kasi kiuchumi ya Afrika Mashariki (EAC).