Mauzo ya bidhaa nje ya nchi yapaa

elivina shambuni

JF-Expert Member
May 31, 2018
461
295
1578389393397.png

BAADA ya Tanzania kusuasua kwa muda mrefu katika mauzo ya bidhaa nje ya nchi, hatimaye sasa mambo yameanza kubadilika, ambapo mauzo hayo yameongezeka kwa kiasi kikubwa, huku dhahabu ikitajwa kuchangia kupanda huko.

KwaB mujibu wa Ripoti iliyotolewa na Benki Kuu Tanzania (BoT) kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Novemba mwaka jana, serikali imeuza dhahabu ya Dola za Marekani milioni 2,139.9 na imechangia asilimia 51.4 ya bidhaa zilizouzwa nje ya nchi.

Hilo ni ongezeko la asilimia 41.9, ikilinganishwa na kipindi kama hicho kwa mwaka juzi, ambapo mapato yalikuwa ni Dola za Marekani milioni 1,507.6. Taarifa hiyo ilibainisha kuwa sababu ya dhahabu kuchangia kiasi hicho cha fedha, ni kutokana na mabadiliko ya sera na sheria za kuiendesha sekta ya madini nchini, ambapo tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk John Magufuli, sekta hiyo imezidi kuimarika.

Rais Magufuli alianzisha mkakati wa kulinufaisha taifa kupitia madini, kwa kuanzisha Tume ya Madini ambayo moja ya majukumu yake makubwa ni kusimamia rasilimali ya madini kikamilifu, ikiwemo kuhakikisha yanauzwa mahala sahihi na kwa bei stahiki.

Katika kuhakikisha inafanikisha hilo, tume hiyo ilianzisha masoko ya madini kila kona ya nchi, ambapo kupitia masoko hayo serikali kwa sasa inajua kiasi halisi kinachopatikana katika madini hayo, ambapo yanauzwa ndani na nje ya nchi na kuliingia fedha taifa. Hadi sasa yapo masoko ya madini 28 nchi nzima.

Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa kuna ongezeko la asilimia 28.4 la bidhaa za viwandani, zilizouzwa nje ya nchi na kuliingizia taifa Dola za Marekani milioni 996. Taarifa hiyo ilitaja asilimia kubwa ya bidhaa hizo ni zenye asili ya chuma na vigae. Kwamba bidhaa za kilimo za tumbaku, katani na mbolea, nazo ziliuzwa kwa wingi nje ya nchi hasa baada ya kuongezewa thamani.

Pia ripoti hiyo ya BoT, ilibainisha kuwa bidhaa za asili ambazo ni za kilimo, zimeendelea kufanya vibaya kwa kushuka kwa asilimia 21.4 na kuingiza Dola za Marekani milioni 740.3 hadi kufikia Novemba mwaka jana. Mazao ya kahawa, pamba na katani, yaliuzwa kwa wingi nje ya nchi na kufanya vizuri kwenye masoko ya nje kutokana na ukuaji mzuri. Lakini, bidhaa nyingine nyingi za asili zilishindwa kufanya vema.

Zao la korosho lilishindwa kufanya vema, kutokana na kuporomoka kwa soko la bidhaa hiyo katika Soko la Dunia, hali ambayo pia ililikumba zao la karafuu. Kwa upande wa bidhaa zilizoingizwa kwa wingi ndani ya nchi ni za ujenzi, ambazo zimeingizwa nchini na kutumiwa kwenye ujenzi wa miradi mikubwa ya kimkakati, inayoendelea kujengwa. Miongoni mwa miradi ya kimkakati ni ujenzi wa Reli ya Kisasa(SGR), Bwawa la Umeme la Mwalimu Julius Nyerere kwenye maporomoko ya Mto Rufiji na Barabara za Juu Ubungo, Dar es Salaam.

Hadi kufikia Novemba mwaka jana, Dola za Marekani milioni 11,004.5 zilitumika kununua bidhaa za ujenzi ikiwa ni ongezeko la asilimia tisa. Mafuta yaliyoingizwa nchini, yamechukua asilimia 23.1 ya bidhaa zote zilizoingizwa nchini na kufikia Dola za Marekani milioni 2,078.6. Huenda kiwango hicho kikaongezeka kutokana na miradi hiyo mikubwa inayozidi kujengwa.
 
Back
Top Bottom