Mauno ya Kangi hayajamsaidia

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
2,055
3,239
BARAZANI

‘Mauno’ ya Kangi hayajamsaidia

Na Ahmed Rajab

KUPOROMOKA kwa Alphaxard Kangi Ndege Lugola ni funzo kubwa kwa viongozi wote wenye kiburi waliolewa madaraka na wa ngazi zote za utawala. Kangi Lugola alikuwa akiwashangaza watu tangu ateuliwe na Rais John Magufuli Julai Mosi, 2018 awe waziri wake wa mambo ya ndani.

Hata kuanguka kwake Lugola pia kuliwashangaza wengi kwa namna alivyopopolewa hadharani na mkuu wa nchi.

Aliwashangaza kwanza kwa mavazi yake yaliyokuwa kama na viraka vya bendera ya Tanzania. Labda akitaka kuonesha kwamba amewapiku Watanzania wote kwa uzalendo.

Halafu akawashangaza kwa ujeuri wake. Kila alipokuwa akizidi kulewa madaraka kiburi kikimzidi. Na kila kiburi kilipokuwa kikimzidi ndipo alipozidi kuwaona wananchi wenzake kuwa kama sisimizi. Maneno yake yalikuwa makali na ya kutisha.

Wizara ya mambo ya ndani ni kama kaa la moto. Wenye kulishika huwa hawadumu sana, mara hilo kaa huwaunguza wakaanguka.

Wizara aliyokuwa amekabidhiwa ni moja kati ya wizara nyeti na nzito katika serikali. Ina dhamana kubwa kwa vile huhusika na usalama wa raia na kwa kiwango fulani hata na usalama wa taifa. Chini ya wizara hiyo kuna jeshi la polisi, idara za magereza, uhamiaji, kikosi cha zima moto na uokozi, idara ya wakimbizi, ya huduma ya jamii pamoja na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Mbawa za wizara hiyo zinaruka hadi Zanzibar kwani ni moja ya wizara za serikali ya Muungano wa Tanzania zenye mamlaka Zanzibar.

Kabla ya Muungano wizara hiyo ilikuwa mikononi mwa vigogo wa siasa za Tanganyika, George Kahama (1961-1962) na Oscar Kambona (1962-1963). Siku hizo Kambona akionekana kuwa kiongozi mwenye ushawishi mkubwa kwa wananchi na uzito wa kisiasa uliopikuliwa na ule wa Mwalimu Julius Nyerere.

Baada ya hapo kati ya mawaziri 24 walioishika wizara hiyo ni tisa tu waliokuwa Wazanzibari, wengi wao wakiwa wateule wa Nyerere. Hali hiyo ni ya kusikitisha tukizingatia umuhimu wa wizara hiyo na haja ya kuwa na usawa baina ya nchi mbili zinazounda Muungano.

Miongoni mwa Wazanzibari waliowahi kuishika wizara hiyo ni Ali Hassan Mwinyi, Hassan Nassor Moyo, Salmin Amour na Abdalla Said Natepe. Hawa wote waliteuliwa na Nyerere.

Wengine ni Ali Ameir Mohamed, Mohamed Seif Khatib na Ramadhani Omar Mapuri. Hawa waliteuliwa na Rais Benjamin Mkapa.

Mzanzibari pekee aliyeteuliwa na Rais Jakaya Kikwete awe waziri wa mambo ya ndani alikuwa Shamsi Nahodha.

Mwinyi alipokuwa rais hakumteua hata Mzanzibari mmoja katika wizara hiyo. Na hadi sasa Magufuli naye hakuona haja ya kumteua Mzanzibari. Mwinyi alifanya historia alipokuwa waziri wa mambo ya ndani kwa hatua aliyoichukua 1976 ya kujiuzulu wadhifa wake wa uwaziri baada ya kubainika kwamba raia wasio na hatia waliuliwa na askari mkoani Shinyanga.

Baadaye, Mwinyi alisema kwamba ingawa si yeye aliyewaamrisha au kuwaambia hao polisi wende Shinyanga kuua watu na ingawa hawakumshauri kuhusu suala hilo, hata hivyo alijiuzulu kwa sababu ilikuwa lazima awajibike kwa mauaji hayo. Kilikuwa kitendo kisicho cha halali.

Lau Lugola angelizifuata nyayo za Mwinyi za uwajibikaji basi angelijiuzulu mapema sana kutokana na visa chungu nzima vya kupotea watu, mauaji yasiyofahamika pamoja na vitendo vya polisi vya kuwatisha wakosoaji wa serikali.

Kwa kujiuzulu kwenye uwaziri Mwinyi alikuwa ameanzisha utamaduni mzuri wa kuwajibika katika siasa, dhana iliyo muhimu katika ustawi wa utawala bora. Baada ya kuondoka kwenye wizara ya mambo ya ndani, Mwinyi aliteuliwa balozi nchini Misri, halafu akawa Rais wa Zanzibar na hatimaye alimaliza kuitumikia Tanzania akiwa Rais kuanzia 1985 hadi alipostaafu 1995.

Alipokuwa Mwinyi Rais wa Tanzania kuna visa viwili vitatu vilivyotokea vilivyowahusu mawaziri wake wa mambo ya ndani na ufisadi. Cha kwanza ni cha ndugu wawili wafanyabiashara V.G. Chavda na P.G. Chavda na waziri wa mambo ya ndani wa siku hizo, Augustine Mrema.

Ndugu hao walituhumiwa kwamba mnamo 1993 waliutumia vibaya mkopo maalum wa dola za Marekani milioni tatu na nusu. Waliahidi kuzitumia fedha hizo kuyafanyia ukarabati mashamba ya mikonge iliyo Tanga.

Miongoni mwa mipango yao ilikuwa kuzitengeneza nyumba waishio wafanyakazi kwenye mashamba hayo, kuzitengeneza mashine kongwe na kupanda miche mipya ya mikonge. Walidai kwamba miradi yao itapelekea papatikane ajira 1,400 na kwamba itaipatia nchi fedha za sarafu za kigeni zenye thamani ya dola za Marekani milioni 42.

Ukweli wa mambo ni kwamba walizihaulisha fedha hizo nchi nje wakijidai kununua mashine bandia na spea. Baadaye ilibainika kwamba ndugu hao walikuwa wakikingwa na wanasiasa wazito, akiwemo Mrema. Kwa hivyo, walinusurika wasishtakiwe.

Mwanzoni mwa 1995, kampuni maarufu ya Mohamed Enterprises ilituhumiwa kwamba ikiuza vyakula visivyofaa kuliwa na wanadamu. Mrema aliahidi kwamba ataitia adabu kampuni hiyo lakini kabla hajachukua hatua aliondoshwa kwenye wizara hiyo na akashushwa cheo kwa kuteuliwa waziri wa vijana na utamaduni, wizara nyepesi kushinda aliyokuwa nayo.

Mrema akaanza kuishambulia serikali ya Mwinyi kwamba ikivumilia ufisadi na kwa kutowachukulia hatua wenye kuhusika na vitendo vya ufisadi. Halafu akafukuzwa kwenye uwaziri na akajiunga na chama cha upinzani chs NCCR-Mageuzi.

Siku moja mwezi Machi 1995, Mwinyi aliwaita mawaziri wake kwa mkutano. Mawaziri hao walifika Ikulu, Dar es Salaam, wakitaraji kwamba watakuwa na mkutano wa muda usiopungua saa tatu. Kwa sababu hiyo baadhi ya hao mawaziri waliwaambia madereva wao waondoke na warudi baadaye.

Kinyume na mawaziri walivyotarajia mkutano wao ulianza na kumalizika baada ya dakika zisizozidi tatu. Mwinyi aliwaambia kwa ufasaha mkubwa kwamba aliwataka mawaziri wote 26 na manaibu wao 14 wajiuzulu papo hapo.

Waliokuwa wameingia kwenye chumba cha mkutano wakitabasamu tabasamu zao zilikauka ghafla moja. Waliokuwa wamewaambia madereva wao waondoke na warudi baadaye wakianza kutafakari namna ya kuutwanga mguu kwenda makwao.

Mwinyi hakumfukuza mtu mmoja. Aliwafuta kazi jumla ya watu 40 waliokuwa wazito na wasiokuwa wazito. Wote, wakiwa pamoja na waziri mkuu Joseph Warioba, aliwafukuza kwa sitara si kwa izara.

Ulimwengu haukujua yaliyojiri mpaka kadhia hiyo ya kufutwa kazi mawaziri kwa mkururo ilipotangazwa saa saba mchana kwenye taarifa ya habari ya Radio Tanzania, Dar es Salaam.

Mwinyi alieleza baadaye kwamba alilazimika kuwafukuza mawaziri wake wote kwa sababu akitaka kuupiga vita ufisadi uliokuwa umezagaa katika wizara zote na kwa kutokuwako uwajibikaji. Mwinyi alisema kwamba hali ilikuwa mbaya sana hata wauza njugu walibidi walishie ili waweze kuendesha biashara zao!

Waziri mmoja (jina linalihifadhi) alikurukupa na kusema kwamba alikuwa na miadi Ulaya iliyopangwa kwa muda mrefu. Aliambiwa aivunje miadi hiyo.

Wizara ya mambo ya ndani ilioza kwa rushwa. Ilikuwa kwenye safu ya mbele ya wizara zilizokuwa zikivuma kwa ufisadi.

Inavyosemekana ni kwamba mwanzoni mwa Februari Halmashauri ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (NEC-CCM) ilikutana na kukabidhiwa ripoti ya “Kamati ya Uchunguzi Kuhusu Ufisadi”. Kamati huyo ilikuwa imeundwa miaka miwili kabla na ripoti yake haikusaza kitu. Iliweka kila kitu bayana.

Ripoti hiyo ilizitaka taasisi 12 kuwa zilinuka kwa ufisadi. Miongoni mwazo zikiwa Wizara za Mambo ya Ndani, Afya, Sheria na Ardhi. Inasemekana kwamba Mwalimu Nyerere, alishikilia msimamo kwamba mawaziri wote wa wizara zinazohusika wafikishwe mbele ya kamati kuu ya CCM.

Inasemekana pia kwamba Waziri wa Sheria, akiamini kwama hakuwa mkosa, aliandika barua ya kujiuzulu asije akaadhiriwa kwa kufukuzwa. Waziri mkuu naye, vivyo hivyo, alijiuzulu.

Lakini waziri wa mambo ya ndani alikuwa na msimamo mwingine. Alikuwa tayari kuikabili kamati kuu ya CCM. Na alidokeza kwamba atayoyasema yatawafedhehesha wengi. Ndipo Mwinyi alipoamua kwamba kheri nusu ya shari kushinda shari kamili. Nusu ya shari ilikuwa kuwaambia mawaziri wote na manaibu wao wajiuzulu badala ya kumuachia Waziri wa Mambo ya Ndani aende mbele ya kamati kuu ya CCM na kuwafedhehesha wengi.

Kangi Lugola alikuwa mmoja wa waliochangia kuifanya serikali ya awamu ya tano ionekane kutawala kwa vitisho. Alikaa kimya na kufurahia askari wake wa polisi walipokiuka katiba kwa kujionesha wazi kwamba wanakipendelea chama kinachotawala au pale walipokuwa wakiwakandamiza kwa kusudi wapinzani na wakosoaji wa serikali wanaoendesha shughuli zao kwa mujibu wa katiba.

Badala ya kuonesha uongozi wenye uadilifu kwa kuvikemea vitendo kama hivyo yeye alivivumilia. Pamoja na kutoheshimu miongozo ya utawala bora, Lugola pia hakuupa heshima wadhifa aliokabidhiwa wa kuingoza wizara nzito kama ya mambo ya ndani ya nchi.

Mara kwa mara akionesha utovu wa adabu hadharani kwa kukatika mauno kama yumo kwenye beni ya “mbwa kachoka”. Alijiamini kuvuka mpaka hata akakosa nidhamu na heshima aliyostahiki awe nayo kwa wadhifa aliokuwa nao.

Ama kweli wahenga hawakukosea waliposema kwamba mwisho wa maji ni tope.

Juzi tu Lugola akionekana kama mtu mwenye kutisha; leo amegeuzwa kinyago. Amekuwa mtu anayefanyiwa dhihaka na tashtishi zisizo kifani ndani ya mitandao ya kijamii. Kilichochongea yakamfika yote hayo ni kiburi chake.



Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab




Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom