Watu wengine wanaamini kwamba ukinywa soda nyeusi (cola), kuchemsha majani ya chai mengi kisha uyanywe au energy drink mara baada ya tendo la ndoa, mbegu za kiume hufa tumboni na hivyo mimba inazuilika. Nilishangaa zaidi kuwa kuna mtaalamu wa afya pia aliwahi kueleze kuhusu hii ishu. Sikumuamini na nashindwa kuelewa "how this works"
Lakini pia watu wamekuwa wakidanganyana kuhusu kunywa maji mengi, majivu, maji baridi na hata kuruka sarakasi au kunawa kunaweza kuzuia ujauzito. Je kuna ukweli wowote
Lakini pia watu wamekuwa wakidanganyana kuhusu kunywa maji mengi, majivu, maji baridi na hata kuruka sarakasi au kunawa kunaweza kuzuia ujauzito. Je kuna ukweli wowote
- Tunachokijua
- Utafiti uliochapishwa katika jarida la 'Reproductive Toxicology' ulibaini kuwa matumizi ya kafeini kwa wanawake hayakuwa na athari kwenye kuzuia ujauzito. Hata hivyo inaongeza kuwa matumizi makubwa ya kafeini (≥300mg/kwa siku) kwa wanaume yalihusishwa na kupungua kidogo kwa uwezo wa kusababisha ujauzito. Uhusiano huu ulionekana kuhusiana zaidi na matumizi ya soda zenye kafeini na vinywaji vya kuongeza nguvu (energy drinks)
Inaelezwa kuwa hata kama yai likifanikiwa kurutubishwa na mbegu ya kiume, ujauzito unaweza kutokea bila kujali kama mhusika ametumia soda au la. Ingawa soda haiwezi kuzuia ujauzito moja kwa moja, matumizi ya kupita kiasi yanaweza kuathiri uwezo wa kupata ujauzito kutokana na baadhi ya viambato vyake.
Wolters Kluwer Health katika utafiti wake uliochapishwa katika jarida la 'Epidemiology' ulibaini uhusiano kati ya matumizi ya vinywaji vyenye sukari na kupungua kwa uwezo wa kupata ujauzito kwa wanawake na wanaume, ambapo na kuhusiana zaidi na soda zenye sukari, ambazo ndizo vinywaji vyenye sukari vinavyokunywa zaidi.
Iligundulika kupungua kwa kiasi kikubwa kwa uwezo wa kupata ujauzito kwa wanawake na wanaume waliotumia zaidi ya kinywaji kimoja cha energy drink chenye sukari, kwa siku, ingawa matokeo yake yalitokana na idadi ndogo ya washiriki.
Vinywaji hivyo vyenye sukari vinaweza kuwa na athari mbaya kwenye uzazi kwani vimehusishwa na ubora duni wa mbegu za kiume na matumizi ya soda na wanawake yamehusishwa na kupungua kwa uwezo wa kupata ujauzito ambapo utafiti mmoja uliofanywa Marekani ulibaini kuwa wanawake waliokuwa wakinywa mara kwa mara walikuwa na idadi ndogo ya mayai yaliyotungwa, ikilinganisha na wanawake wasiokunywa kabisa.
Uwezekano wa kupata mtoto ulikuwa pungufu kwa asilimia 12 kwa wanawake waliokunywa kikombe kimoja cha vinywaji hivyo kwa siku, na asilimia 16 kwa wale waliokunywa zaidi ya kikombe kimoja kwa siku.
Kadhalika Tovuti ya Semic health inabainisha madai mengine ikiwemo mchanganyiko wa maji na chumvi, juisi ya limao, chai ya rangi na kadhalika kuwa yanahusisha nahu taratibu ambazo ni hatari kwa afya. Pia inaongeza kuwa hakuna kinywaji chochote kilichotengenezwa au cha nyumbani kilichoidhinishwa au kuthibitishwa kisayansi kuzuia ujauzito.
Je, vipi wanaoamini kujiosha ukeni baada ya tendo la ndoa kunaweza kusaidia kuzuia ujauzito?
Tovuti ya Women health inaeleza kuwa kujiosha kwa maji au dawa maalum (douching) baada kufanyika kwa tendo la ndoa hakuzuii kupata ujauzito. vilevile haishauriwi kabisa kutumika kama njia ya uzazi wa mpango.
Ikiwa umefanya tendo la ndoa bila kutumia njia ya uzazi wa mpango au njia uliyotumia haikufanya kazi ipasavyo, unaweza kutumia uzazi wa mpango wa dharura ili kujikinga usipate mimba.
Wapo baadhi ya watu amabo huamini kuwa Coca-Cola inao uwezo wa kuzuia mimba. Mfano mzuri huko nchini Angola, vijana waliowahi kunywa Coca-Cola wakiwa wamechanganya na aspirin mbili au zaidi baada ya tendo la ndoa wakiongea na UNFPA
“Nilijaribu hii zamani sana, nikiwa kijana mdogo,” mwanamke mmoja mzee alieleza. Mchanganyiko huo ulimletea madhara tumboni. “Nilipata wakati mgumu sana,” alisema.
Kinywaji hiki pia kimewahi kutumika kama dawa ya kuoshea uke huko Amerika Kaskazini, Ulaya Mashariki na Asia ya Kati. Njia hii pia haina ufanisi na inaweza kusababisha kuharibu tishu na kusababisha maambukizi.
Vilevile wapo wanawake wengi ambao hujiosha kwa kutumia sabuni na maji baada ya tendo la ndoa wakiamini kuwa ni njia ya kuzuia ujauzito. Dkt. Su Sandy kutoka Population Services International Myanmar alinukuliwa katika tovuti ya UNFPA (United Nations Population Fund) akisema “Wanadhani wataweza kuondoa mbegu za kiume, lakini mbegu hufika kwenye mfuko wa uzazi kabla hata hawajapata nafasi ya kuosha,” aidha daktari huyo aliongeza kuwa tabia hii inaweza kubadilisha usawa wa asidi ukeni na kusababisha muwasho au maambukizi.
Kwa mujibu wa tovuti ya Women health tunapaswa kufahamu kuwa uke wenye afya huwa na bakteria wazuri na wabaya. Uwiano wa bakteria hao husaidia kudumisha mazingira yenye asidi ambapo husaidia kulinda uke dhidi ya maambukizi au muwasho.
Kujiosha (douching) kunaweza kusababisha kuongezeka kwa bakteria wabaya. Hali hii inaweza kusababisha maambukizi ya fangasi (yeast infection) au bacterial vaginosis. Ikiwa tayari una maambukizi ukeni, kujiosha kunaweza kusukuma bakteria wanaosababisha maambukizi kupanda hadi kwenye mfuko wa uzazi, mirija ya mayai na ovari. Hali hii inaweza kusababisha magonjwa ya uchochezi wa nyonga (pelvic inflammatory disease), ambayo ni tatizo kubwa la kiafya.