Matarajio ya ajira yanadumaza maendeleo ya wahitimu

Peter Mwaihola

JF-Expert Member
Jun 23, 2022
227
333
Maatarajio ya vijana wengi ni kunufaika na elimu pindi wanapohitimu katika ngazi mbalimbali za elimu
hususani elimu ya vyuo vya kati na juu.

Kumekuwa na mitazamo mbalimbali juu ya sababu zinazopelekea vijana wengi kushindwa kujiajiri pindi wanapohitimu taaluma zao.

Vijana wengi hujikuta katika hali ya kukosa kazi, hivyo kuishi bila matumaini ya kukidhi mahitaji yao ya msingi hasa yale ya kijamii.

Baadhi ya sababu zinazotajwa kusababisha wahitimu wengi kukosa shughuli za kujihusisha nazo ni pamoja na uhaba wa mitaji ili kuweza kuwekeza katika
shughuli mbalimbali.

Pia kasumba ya wahitimu wengi kutaka kujiajiriwa katika nafasi za maofisini ni sababu inayotajwa.

Gabriel Mbuba ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu cha Iringa anaejihusisha na ujasiriamali wa bidhaa za ususi ikiwemo vikapu anasema kuwa wahitimu wengi wanakosa ujuzi wa mambo mbali na taaluma zao kulingana na malezi waliyoyapata kwenye jamii zao ambayo hayawaendelezi kuwa na mawazo mbadala wa elimu.

“wahitimu wengi hawana ujuzi mbali na taaluma zao hivyo wanapohitimu hushindwa kujihusisha na mambo mengine hivyo kujikatia tamaa kuwa hawawezi kuanza maisha yao kwa kujitegemea”.

Anasema kuwa yeye haoni ugumu wa kujihusisha na shughuli mbalimbali ikiwemo fani yake ya ususi pindi anapopata muda wa ziada baada ya masomo, kwani akitengeneza bidhaa zake huwatumia watu wanaomzunguka kama mtaji muhimu ambapo wao ndio hununua bidhaa zake na kumtangazia kwa wengine ambao wanaweza kuzinunua.

Pia Mbuba anasema kuwa idadi kubwa ya wahitimu huwa na fikra za kuogopa kujaribu kufanya mambo mbalimbali kwa kuhofia kuingia hasara kutokana na wao kukosa uzoefu wa kuendeleza fursa hizo na kujiona wachanga zaidi.

Nae Daudi Jeremiah ambaye ni muhitimu wa chuo kikuu cha Stella Maris mjini Mtwara anasema kuwa jamii bado ina mtazamo hasi kwa wahitimu wa elimu ya juu kwakuwa inawabagua na kuwaona kama watu wa tabaka lingine ambao hawapaswi kujisumbukia bali wasubirie nafasi za kazi serikalini jambo ambalo linawafanya wahitimu wengi kujiona wanatengwa hivyo kuishia kukata tamaa.

Pamoja na hayo Venance Makirika ambaye ni mhadhiri na mbobezi wa masuala ya kiuchumi kutoka chuo kikuu cha kikatoliki Mbeya, CUCoM anasema kuwa elimu inayotolewa kwenye vyuo vingi vya juu na kati nchini haimjengi muhitimu kujitegebali inamjenga kuwa tegemezi wa kusubiria ajira za kuajiriwa.

Aidha Makirika anasema kwa kiasi kikubwa elimu hiyo haiendani na uhalisia wa jamii ambayo ni ya watu wa hali ya chini ambao hawawezi kuwa na kazi nyingi rasmi za kuajiri wengine licha ya uwepo wa rasilimali za kutosha ambazo zinahitaji kuendelezwa kwa msaada wa rasilimali fedha.

Hivyo Makirika anapendekeza vyuo kumuandaa vizuri mwanafunzi ikiwemo kuweka kipaumbele kwenye masomo ya ujasiriamali na ubunifu ili kuwandaa wanafunzi kulingana na fursa zilizopo kwenye jamii ili waweze kujiajiri pindi wanapohitimu
elimu hiyo.

Makirika anaunga mkono mpango wa serikali kukusanya maoni juu ya mabadiliko ya mitaala ya elimu nchini, akibainisha kuwa iwapo mtaala wa elimu utaboreshwa katika ngazi ya elimu ya chini italeta msukumo kwa taasisi za elimu ya juu na kati kubadilika na kutoa elimu yenye manufaa.
Mtazamo wa makirika na watu wengine unasawiri hali halisi ya maisha ya wahitimu wengi ambao huishi kwa kutegemea ajira.

Kuna haja ya wahitimu kujitambua na kufuata yale yenye manufaa kwao ikiwemo kuzingatia elimu ya kujiajiri na ujasiriamali unaotolewa na wasizifanye taaluma zao kuwa kifungo cha kutojihusisha na mambo mengine.

Peter Mwaihola
Photo_1693039769539.jpg
 
Back
Top Bottom