Mataifa dhaifu ni mataifa yaliyokosa maarifa

Shayu

Platinum Member
May 24, 2011
608
1,655
Kwa wenye hekima maisha ni fumbo ambalo linapaswa kufumbuliwa. Na Dunia ni chuo ambacho binadamu anatakiwa kujifunza kila siku ili kufikia ukuaji wake wa mwisho kiakili. Chuo hiki ni kikubwa kuliko chuo chochote na wahitimu wake huvikwa tuzo ya ufalme.

Kwasababu hatukuumbwa tuishi pekee, bali tuliumbwa tuishi ili tujifunze na ili tukue. Tena Binadamu hakui kama mti tu kwa mfumo wa kimaumbile bali akili yake lazima pia ikue. Na aweze kuwa na nguvu ya kuchanganua jema na baya. Aondokane na ujinga. Na AFUATE njia iliyo sahihi. Kwasababu ni katika njia iliyosahihi ndio kwenye misingi iliyo imara. Ni wajibu wetu kukusanya maarifa kadiri ya uwezo wetu. Ni katika maarifa binadamu hupata STRENGTH na sio katika ujinga. Ujinga ni udhaifu. Mataifa dhaifu ni mataifa yasiyo na maarifa.

Tunakamata samaki kwasababu tuna uelewa mkubwa zaidi yao. Vile vile kuku, mbuzi na Ng'ombe tunafuga, Kwasababu uwezo wa akili zetu ni mkubwa zaidi yao ndio maana tunawatawala.

Na binadamu na mataifa wanatofautiana katika uelewa pia na utumiaji wa akili zao kutafuta na kukuza maarifa. Mataifa yenye watu wenye uwezo mkubwa wa kufikiri watayatawala mataifa ya watu wajinga. Wana nguvu ya kuvumbua vitu na silaha kutawala wajinga. Watu waliowekeza katika mambo ya kijinga yasiyo na manufaa watatawaliwa.

Kama kuna ulafi ambao binadamu anapaswa kuwa nao, ni ulafi wa kutafuta maarifa ili yamuongoze katika maisha yake. Na kuuvamia na kuuteka kisha kuufunga kamba ujinga na upumbafu, ambao una madhara makubwa kwa maisha ya binadamu na hata katika mataifa. Ni heri kuwa maskini kuliko kuwa tajiri mpumbavu na mjinga ambae njia zake sio nzuri.

Makosa mengi tunayofanya yanatokana na kukosa maarifa ya kutosha na busara ya kuongoza maisha yetu. Kwahiyo ni muhimu kwetu kutafuta maarifa ambayo yatatusaidia kufanya maamuzi yenye hekima. Roho nyingi zimeangamia kwa kutenda matendo ambayo sio sahihi na kujikuta kwenye majuto. Na majuto ni mjukuu.

Tunaweza kubadilika tunaweza kubadili njia zetu. Na njia pekee yenye matumaini ni njia ya mwanga. Ni muhimu kwetu kutafuta tochi ambayo itamulika maisha yetu na tochi hiyo ni maarifa. Hakuna kiza ambacho kitafunika tochi ya maarifa.

Kwa uwepo wetu katika dunia hii tuna wajibu mmoja mkuu. Kutafuta mwanga ambao utaongoza maisha yetu kwa kizazi hiki na kinachokuja na huo ndio wajibu wetu mkuu. Kufanya jitihada kadiri ya uwezo wetu kuwa karibu na Mungu na kuacha matendo ya gizani.

Na tujue kwamba mataifa dhaifu yote duniani ni mataifa yaliyopungukiwa maarifa. Ni wajibu wetu wa dhati kabisa kutafuta maarifa ili yatukomboe.

Shepherd of the Lord.
 
Back
Top Bottom