Masikini hatuna maendeleo kwa sababu ya chuki dhidi ya matajiri

mpasta

JF-Expert Member
Jan 17, 2011
917
1,997
Chambilecho,"mbaazi zikikosa maua, husingizia jua", ndio hivyo hivyo silka ya mwanadamu, akikosa majibu ya baadhi ya shida zake zinazomsibu hutafuta mtu wa kumuangushia nyumba bovu. Vijiji vingi vya TANZANIA mvua zikikataa kunyesha, watu wakifa ovyo kwa magonjwa ya ajabu, utaskia anaitwa Mganga "LAMBALAMBA" kwa baraka za viongozi wa kijiji kuja kutoa watu uchawi. Unaweza kudhania ni waswahili tu ndio tuna tabia hizo lakini hata wazungu nao wamepitia maisha hayo ya kuwategemea waganga "LAMBALAMBA". Ukisoma katika historia ya nchi za Ulaya,katika miaka ya 1450-1750 kulikuwa na mauaji ya watu wanaohisiwa ni wachawi "Witch Hunt/Witch Purge". Watu walikuwa wakiingia ugonjwa wa ajabu, hamna tiba basi hitimisho kuna wachawi wanaroga watu msako unaanza. Inakadiriwa takribani watu elfu 50 waliuliwa kipindi hicho.

Ulaya walivyoachana na ujinga huo wa "WITCH HUNT", wakahamia kwenye "FINANCIAL WITCH HUNT". Tatizo la umasikini limeshitadi katika jamii, badala ya kutafuta suluhisho la kweli, chuki inahamishiwa kwa matajiri kuwa ndio wanatunyonya na kusababisha uwepo wa masikini. Chuki hiyo ndio ikazaa "French Revolution 1789".

Inaweza kuwa kweli wapo baadhi ya Matajiri wanatajirika kupitia njia haramu kama uuzaji wa mihadarati, ujambazi, dhuluma, n.k lakini kwanini itumike kanuni ya samaki mmoja akioza wote wameoza?. Wakati kwa mtazamo wangu wapo matajiri kibaoo ambao ni wema. Wamezalisha maelfu ya ajira kwa watu masikini, wanasaidia masikini kupitia miradi ya elimu na afya, n.k??. Hivi leo ukimtafakari tajiri kama Bakhressa namna alivyozalisha ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja. Tafakari maelfu ya vijana wauza maji baridi Mijini, bila yeye huenda tungekuwa tunakunywa togwa tu. Tafakari MAMALISHE wangapi wanategemea ngano yake asubuhi kwa ajili ya kuandaa vitafunwa, n.k

Hizi chuki hata hapa Tanzania zipo sana, ndio enzi zile Wanasiasa akina Mtikila na chama chake DP wakaanzisha msamiati wa "MAGABACHORI" wakiwaita Watanzania jamii ya Wahindi, wakiwatuhumu kunyonya wazalendo. Matokeo yake, masikini wakaandamana mitaani Jijini Dar es Salaam na kuharibu mali za Wahindi.

Sasa chuki dhidi ya Matajiri ni upofu mkubwa, Mwanafalsafa mmoja anasema "Anger and Ignorance causes blindness"(Chuki na ujinga vinasababisha upofu). Maadamu tumechagua mlango wa chuki dhidi ya Matajiri, madhara yake ni kuwa kwanza tunakosa kuzipa akili zetu nafasi ya kujifunza mbinu walizotumia mpaka wakatajirika. Tena tunajifariji kwa maneno sijui vitabu vitakatifu vya dini,utaskia masikini ananukuu kitabu cha Mathayo kwa tafsiri anayotaka yeye kuwa YESU kasema;
"Tena nawaambieni, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko kwa tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”
Pili tunawatia hofu matajiri na kuwafanya wafiche utajiri wao nje ya nchi. Kama tungewapenda huenda wangewekeza zaidi na zaidi hivyo kumaliza tatizo la ajira. Ndio utakuta Wahindi wengi wanaishi Majumba ya NHC hawajengi, pesa zao wengine wanahifadhi nchini CANADA, USWIZI na kwingineko, wakichuma utajiri wao wakatosheka, wanahama nchi wanatuacha masikini tuhangaishana wenyewe kwa wenyewe.

Screenshot_20220417-165658.jpg
 
Back
Top Bottom