MARIJANI RAJABU: Miaka 18 sasa Jabali bado lipo imara

MARIJANI RAJABU: Miaka 18 sasa Jabali bado lipo imara

sulphadoxine

JF-Expert Member
Joined
Nov 1, 2010
Posts
2,257
Reaction score
649
MARIJANI Rajabu ingawa hatunaye tena hapa duniani, wapenzi wa muziki wa dansi hapa nchini hata nchi za jirani hawatamsahau kamwe.

Alikuwa miongoni mwa wanamuziki waliotoa mchango mkubwa wa maendeleo ya nchi, ikiwamo elimu kupitia tungo za nyimbo zake maridhawa zilizokuwa zikiendana na wakati.
Marijani Rajabu, kesho Jumamosi Machi 23, 2013, Watanzania tutakuwa tukiomboleza kutimia miaka 18 tangu kifo chake.
Alifariki dunia Machi 23, 1995 na mwili wake ukazikwa siku iliyofuata Machi 24, 1995 katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.
Nguli huyo aliyekuwa na sauti yenye mvuto wa aina yake, alizaliwa Machi 3, 1955 Kariakoo, jijini Dar es Salaam. Lakini kwa mapenzi yake Mungu, alimchukua akiwa na umri mdogo wa miaka 40.
Marijani alikuwa akitunga na kuimba nyimbo zilizokuwa zimejaa maudhui mema kwa jamii, ikizingatiwa kwamba, takriban zote zilikuwa ni za visa vya ukweli.
Ubora wa mashairi katika nyimbo hizo ni sababu kubwa ya kuendelea kupendwa na wapenzi wa muziki hapa nchini, hadi kufikia kuitwa ‘Jabali la Muziki’.
Kila kumbi za starehe utakazoingia hapa nchini nyimbo zake hazikosi kusikika zikirindima. Halikadhalika, bendi zetu za muziki wa dansi haziwezi kumaliza onesho lao pasipo kupiga wimbo japo mmoja wa ‘Georgina’.
Hata ukiwa kwenye daladala, unaweza kusikia miito ya simu za abiria zikiita kupitia wimbo wa Marijani Rajabu.
Marijani alikuwa na sifa nyingine, kuweza kutunga na kuimba wimbo wa papo kwa papo, kumuonya mtu yeyote anapofanya jambo lisilo la kistaarabu ukumbini.
Wasifu wa nguli huyu unaeleza kuwa baba yake alikuwa na shughuli za uchapishaji na mama yake alikuwa mama wa nyumbani.
Maisha yake ya utoto yalikuwa ni ya kawaida, ila alipenda sana jinsi ya uimbaji wa nguli mashuhuri kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Tabu Ley na mwimbaji kutoka Guinea, Sorry Kandia.
Marijani alilelewa katika misingi bora ya dini ya Kiislamu, hivyo alihudhuria madrasa, ambako alijifunza vema Kurani na kughani Kaswida tangu akiwa mdogo. Alipokaribia takriban miaka 18, nuru yake katika muziki ilianza kung’aa, baada ya kujiunga na bendi ya STC Jazz (State Trade Corporation).
Bendi hiyo ilikuwa chini ya mpiga gitaa maarufu wakati huo, Raphael Sabuni. Kabla ya hapo, bendi hiyo ilikuwa inajulikana kama The Jets.
Akiwa na bendi hiyo, Marijani aliweza kusafiri nje ya Tanzania kwa mara ya kwanza, ambapo alikwenda Nairobi nchini Kenya. Aliambatana na bendi yake kwa madhumuni ya kwenda kurekodi nyimbo, ambazo zilitoka katika chapa ‘label’ ya Phillips.
Mwaka 1972, Marijani alihamia bendi ya Safari Trippers. Hapo ndipo ubora wake ulifunguka hasa, kwa kuweza kuinyanyua Trippers, kuwa miongoni mwa bendi maarufu hapa nchini wakati huo.
Waliweza kutoa vibao vilivyopendwa mfululizo, pia walifanya ziara ya kuzunguka nchi nzima.
Vibao kama ‘Rosa Nenda Shule’, ‘Georgina’ na ‘Mkuki Moyoni’ viliweza kuuza zaidi ya nakala 10,000 za santuri, hivyo kuwezesha bendi kununua vyombo vyake vizuri.
‘La kuvunda halina ubani’, msemo huu ulijionesha wazi pale maelewano mabaya kati ya wanahisa wanne wa Safari Trippers yaliposababisha kusambaratika kwa bendi hiyo, licha ya kuwa juu kimuziki wakati huo.
Miezi michache baadaye, Marijani na wenzake waliibukia katika bendi ya Dar International. Huko waliwakuta wanamuziki wengine wazuri. Kwa mshikamano wa pamoja, wakaongeza nguvu na kuifanya bendi hiyo kupata umaarufu wa hali ya juu. Vibao vya ‘Zuwena’ na ‘Mwanameka’ vilitamba katika vipindi kadhaa vya salamu vya Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD), wakati huo.
Kwa wakati ule, bendi yao ilirekodi vibao hivyo katika studio hizo za RTD, iliambulia kupata sh 2,500 tu.
Kati ya mwaka 1979 na 1986, Dar International ilipita kila wilaya hapa nchini kupiga muziki, kwa ajili ya kutoa elimu sambamba na kuwaburudisha wananchi, wakipiga katika mtindo wao wa ‘Super Bomboka’.
Uchakavu wa vyombo hatimaye mwaka huo wa 1986 ukamaliza mbio za bendi hiyo.
Historia inaeleza kuwa Marijani Rajabu ‘Jabali la Muziki’ alikuwa mmoja wa wanamuziki 57 waliounda kundi la wasanii likijulikana kama Tanzania All Stars mwaka 1987.
Kundi hilo lilitia fora kwa wimbo wake wa ‘Fagio la Chuma’. Wimbo huo ulikuwa ni kuitikia kaulimbiu ya Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, juu ya uwajibikaji.

Kundi hilo lilirekodi vibao vingine vinne, ambavyo si rahisi kwa bendi zilizopo sasa kufikia ubora wake kimuziki.
Rekodi ya mwanamuziki huyu inaonesha kwamba aliwahi kupitia bendi iliyokuwa ikimilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Mwenge Jazz, ambako alipiga muziki kwa muda mfupi.
Marijani Rajabu alipiga hodi katika Jiji la Arusha na akajiunga na bendi ya Kurugenzi Jazz, ambako alidumu kwa mwaka mmoja.
Baada ya kuhangaika huku na kule, baadaye Marijani Rajabu akaamua kuthubutu kuanzisha kundi lake likiitwa Africulture.
Kundi hilo lililotamba katika mtindo wake wa ‘Mahepe’, halikudumu muda mrefu kutokana na ukosefu wa vyombo vya muziki. Hatimaye mambo yakawaendea kombo, tofauti na walivyotarajia.
Maisha ya mwanadamu yana majaribu mengi sana. Inaelezwa kwamba, kufikia mwaka 1992, hali ya maisha ya Marijani ilikuwa ngumu mno. Alifikia kuendesha maisha yake kwa kuuza kanda za nyimbo zake.
Pamoja na nyimbo nyingi za kuimbia chama tawala na serikali, hata tungo yake ‘Mwanameka’ kutumiwa katika mtihani wa kidato cha nne.
Marijani Rajabu hakuwahi kukumbukwa rasmi kama mmoja wa wasanii bora Afrika Mashariki, hadi mwishoni mwa mwaka jana, alipotunukiwa nishani ya heshima ya Muungano na Rais Jakaya Kikwete, siku ya maadhimisho ya miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania Bara, zilizofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru Desemba 9, 2012 jijini Dar es Salaam.
Wasanii wengine waliotunukiwa siku hiyo ni pamoja na kiongozi wa zamani wa Msondo Ngoma, Muhidin Gurumo, mwimbaji mkongwe wa taarabu, Fatuma Baraka ‘Bi. Kidude’, msanii wa maigizo ya filamu, Fundi Said ‘Mzee Kipara’ na mwanariadha mkongwe, John Steven Akwari.
Hapana shaka utakuwa unazikumbuka nyimbo za nguli huyu kama vile ‘Masudi’, ‘Habari yako’, ‘Sauti Yako Nyororo’, ‘Baba Anna’, ‘Kitinda Mimba’ na ‘Salama Nakuita’. Marijani alifyatua vingine vya ‘Tabu Ni Hali ya Dunia’, ‘Ndoa ya Mateso’, ‘Namsaka Mbaya Wangu’, ‘Tamaa Mbele’ na ‘Baba Watoto’.
Marijani Rajabu hakuishia hapo, kwani alitoka na nyimbo nyingine zilizogusa hisia za wapenzi wa muziki na wale wa kawaida waliokuwa wakisikiliza redio.
Wimbo wa ‘Uke Wenza Una Mambo’ ulifanya ndoa nyingi za mitara kujirekebisha kitabia. Nyingine alizotoka nazo zilikuwa ‘Mama Watoto’ na ‘Tamaa Mbele’.
Wimbo wa Georgina, ulikuwa ni kisa cha kweli cha binti aliyekuwa akisoma Zanaki Sekondari, wakati yeye Marijani akisoma Sekondari ya Tambaza miaka ya 1970.
Marijani alimpenda binti huyo, lakini wazazi wake walipogundua, wakamhamishia bweni ‘kimzobe mzobe’.
Ndipo hapo Marijani huku akiwa amekunja madaftari yake na ‘kuyasunda’ mfuko wa nyuma wa kaptula yake, huku shati la shule amechomolea, alipita kwenye baraza ‘corridors’ akipandisha ngazi kuelekea ghorofani, akilalama kwa kuimba; “Umeondoka Georginaaa, umeniachia masikitikooo....”. Baadaye akakaa chini na kutengeneza mashairi yake na kuwa wimbo kamili wa ‘Georgina’.
Kipaji cha Marijani kilikuwa kikubwa, aliweza kutunga nyimbo za matukio mazuri na akayasifia, kwa yale mabaya, aliyakemea pasipo kujali kama yanamhusu aliyekaribu naye.
Alikuwa na uwezo wa kurekebisha tabia kwa watu, wanaokiuka taratibu za maisha kupitia nyimbo zake.
Gwiji Marijani alithubutu kukemea tabia mbovu ya ndugu yake wa karibu kupitia wimbo wa ‘Chakubanga’. Wimbo huo ulikuwa ni kisa cha kweli, ambacho kilimhusu ndugu yake huyo, ambaye baada ya kutoka Ulaya, akajiita John Smith badala ya jina lake la Chakubanga.
Kwa ridhaa yako wewe msomaji wa makala hii nakupa sehemu fupi ya shairi la wimbo huo.
“Leo kijana ninasema eeh, hayo mambo yako unayofanya eeh, mwisho wake bwana, mambo yatakuwa mabaya, wala usidanganyike na cheo ulichokipata, kudharau wazazi, kuhadaika na dunia, mwana vibaya eeh, vibaya mwana vibayaa. Fikiri kwanza ulikotokaa, usijifanye huna baba wala mama walio kulea, kwa tabu nyingi na mashaka, wakakusomesha ukahitimu mafunzo, mbona unawanyanyasa na matusi kuwatukanaa, mwana vibayaa vibaya mwana vibayaa. Mambo ya ajabu uliyofanya eeh, ulipochaguliwa kwenda ng’amboo, uliporudi bwana, na jina umebadilisha, jina lako Chakubanga unajiita John Smith, na mwendo umebadili bega moja umelishusha…” Marijani mwana wa Rajabu, alikuwa akiona mbali, kwani aliyoyaimba wakati huo ndiyo yanayoonekana kwa vijana wa sasa. Aliwahi kutunga wimbo wa kukemea mwanamume kusuka nywele, kupaka wanja, kupaka Ambi na mengine mengi.
Nyimbo za nguli huyu zitaendelea kusikika vizazi na vizazi kwa kuwa zina ujumbe mzito kwa jamii yoyote ile.
Hivyo basi, iwe changamoto kwa wanamuziki wengine kuiga mema yaliyofanywa na watangulizi wao.
Mungu aiweke roho yake pahala pema peponi. Amina.
 
Inna lillahi wa inna illahi rajiuun. Allahu maghfirahum warhamahum waskaanahum fii jannah. Hakika bila kumung'unya wala kutafuna maneno Tanzania haijawahi na wala haitawahi kupata mwanamuziki mahili kama Marijan Rajabu. Inasikitisha sana amekufa akiwa masikikabisa. Wapenzi wa muziki hatuna cha kumlipa zaidi ya kumuombea dua. Na natoa wito kwa bendi zote zinazopiga muziki aina ya sebene kama vile Kalunde, Machozi, Banana na nyinginezo ambazo yinapiga na kunufaika na nyimbo za marehemu wanaweza kushirikiana na vyombo mbalimbali vya habari na kuandaa tamasha maalum la kumkumbuka marehemu huku wakimualika kiongozi mpenda sanaa kama JK ili waendeshe harambee ya kukusanya pesa na kuipa familia yake kuwafuta machozi, kwa kweli jamii ya wapenda dansi naamini tutaitikia wito huu. Nawakilisha.
 
Hakika bila kumung'unya wala kutafuna maneno Tanzania haijawahi na wala haitawahi kupata mwanamuziki mahili kama Marijan Rajabu.
Kweli alikuwa ni gwiji la muziki Tanzania na nilikua nikiziimba nyimbo zake lakini nadiriki kusema kuwa Mbaraka Mwinshehe alikuwa mahiri zaidi ya Rajabu kwa kiwango kikubwa.
 
Historia ya wimbo wa georgina sikupata kuijua. Kama namuona dah. Rip
 
Pamoja na kuwa mwanamuziki na mtunzi mzuri lakini historia yake inaonyesha hakufaidi matunda ya sanaa yake. Pumzika kwa Amani.
 
picha yake please sisi wengine si wapenzi wa miziki hiyo
r.i.p
 
hakuna nyimbo ya marijani ninayoipenda kama Salama

jamaa alilia kama anaomba mbingu aisee
 
RIP "DOZA" as you were famously known to us of the legendary GETWAYS BAR IN 1970s along Uhuru Street
marijani+rajab.jpg






 
RIP "DOZA" as you were famously known to us of the legendary GETWAYS BAR IN 1970s along Uhuru Street
marijani+rajab.jpg







Dah we mkali mkuu, kwa picha hii uliyoweka ni ushahidi tosha kuwa hamkufahamiana barabarani. Jamaa namkubali sana hasa nnaposikiliza nyimbo za Siwema namba 1 na 2 pamoja na Salama. Apumzike kwa amani.
 
pia alikuwa anafahamika kwa umimi....mara zote alipenda kuimba peke yake, na hakuwa akipenda kuwapa wanamuziki wenzake nafasi....sifa anazopewa ni kubwa sana, lakini angethubutu kwenda bendi kama Sikinde ile iliokuwa na Chidumule, Hamis Juma, Maalim Gutumo na Rehani Bichuka kisha afanye balaa na vichwa hivyo...all in all rest in eternal peace
 
Duh uzi wa siku nyingi lakini si vibaya tukauamsha tena.Nani alitunga na kuimba wimbo unaitwa"Siyo mm ni sababu ya mapendo?"Wimbo mzuri,Sauti nzuri na nzito.
 
Back
Top Bottom