Marekebisho ya katiba ya kenya yana mafunzo mengi kwetu. | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Marekebisho ya katiba ya kenya yana mafunzo mengi kwetu.

Discussion in 'Kenyan News and Politics' started by Rutashubanyuma, Oct 6, 2010.

 1. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #1
  Oct 6, 2010
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 158,613
  Likes Received: 419,787
  Trophy Points: 280
  Zoezi la kuirekebisha katiba ya Kenya limepitia mitihani mingi ambayo ina mafunzo mengi kwa nchi yetu ambayo hadi sasa imefanya marekebisho kumi na nne ya katiba ambayo ni batili machoni pa mahakama za Kenya kulingana na hukumu ya Mchungaji Dr. Timothy Njoya na wenzake saba kesi namba 82/2004 iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Kikatiba ya Kenya, Nairobi chini ya Jaji Mary Kasango. Maamuzi ya Mahakama za Kenya ambayo ni moja ya nchi ya Jumuia ya Madola huheshimiwa hapa nchini.

  Marekebisho ya Katiba ya Kenya yalianza katika utawala wa Moi kutokana na mashinikizo ya asasi mbalimbali huria ambazo zilikuwa zimechoshwa na utawala tajwa kutokana na Rais Moi kuhodhi madaraka mengi na hivyo kuiendesha nchi yao atakavyo. Hivyo lengo kuu la wana mageuzi tajwa waliokuwa wanadai marekebisho ya katiba ya Kenya walikuwa wanataka kumpunguzia Rais madaraka na kwa kumdhoofisha Rais mtajwa walitarajia kuwa na nguvu ya kumwondoa madarakani. Hii ilithibitika zaidi mwaka 1997 wakati wa uchaguzi kwani Bwana Kenneth Matiba aliyeshika nafasi ya pili kwenye uchaguzi wa Rais wa Kenya wa mwaka 1992 aligoma kujiandikisha uchaguzi tajwa na hivyo kupoteza haki ya kugombea nafasi yoyote kwenye uchaguzi tajwa wa mwaka 1997 au kupiga kura. Bwana Matiba alidai sababu ya mgomo tajwa ilikuwa marekebisho madogomadogo ya katiba yaliyofanyika punde kabla ya uchaguzi huo yaliyosimamiwa na Bunge la Kenya yalikuwa na mapungufu mengi na uchaguzi tajwa usingekuwa wa huru na haki na hivyo upinzani usingeweza kushinda na ushiriki wao kwenye uchaguzi tajwa ulikuwa ni kuhalalisha utawala wa Bwana Moi.

  Utawala wa Moi uliamini zoezi la kuirekebisha katiba lazima lidhibitiwe na wanasiasa ili kulinda masilahi yao kwanza kwa kupitia kivuli cha kumtetea mlalahoi ambaye wao walimbatiza jina la “Wanjiku”. Akina Kibaki na Wenzake wakiwa kwenye upinzani ili kuhalalisha kukubalika na jamii ya wakenya walipinga kwa nguvu zote umiliki wa wana siasa tajwa wa zoezi hilo bila mafanikio ingawaje baada ya kuikamata dola wamekuwa ni wanafunzi wazuri wa shule ya Nyayo ya Rais Mstaafu Bwana Moi kwa kutekeleza yote aliyoyataka Bwana Moi. Baadhi ya mambo ambayo Moi aliyasisitiza ni kutopunguza madaraka ya Rais, kuwa na Waziri Mkuu butu kama wa Tanzania ambaye atateuliwa na kutimuliwa kazi na Rais na atathibitishwa na Bunge lakini kuwajibika kwa Rais ili amsaidie kuiongoza serikali Bungeni kwa niaba yake, Bunge kudhibiti marekebisho ya kikatiba na wala siyo Raia wenyewe na kura ya maoni iwe ni kubariki tu mapendekezo ya marekebisho ya katiba yaliyoandaliwa na Bunge. Yote haya aliyoyataka Moi yamepitishwa hivi karibuni na utawala wa mrithi wake wa Bwana Mwai Kibaki.

  Katika kitabu cha maisha ya Rais Moi kiitwacho “Moi: The making of An African Statesman.” kwenye sura ya mwisho inayozungumzia suala la urithi wa Urais wa Kenya, Rais Moi alibainisha kijuujuu watu wawili tu ambao wangeweza kumrithi na ambao walikuwa ni Mwai Kibaki na Uhuru Kenyattta. Katika kumjenga Bwana Mwai Kibaki kwenye kitabu tajwa Moi alimsifia sana Mwai Kibaki ambaye wakati huo alikuwa ni kiongozi wa upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party kuwa siyo mkabila kama Bwana Kenneth Matiba na ni kiongozi mzuri. Pengine mbali na sifa tajwa Moi alielewa Mwai kibaki endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Kenya ataendeleza siasa za Nyayo kwa kuvaa ngozi ya kondoo ya mwanamageuzi hewa kulingana na rekodi ya kinafiki ya Bwana Kibaki ambayo Bwana Moi aliielewa vyema tangu Bwana Kibaki akiwa ndani ya KANU na baadaye ndani ya upinzani.

  Rais Mwai kibaki alipokuwa kiongozi wa upinzani Bungeni alijijengea umaarufu kuwa ni mwana mageuzi haswa kutokana na taaluma yake ya uchumi na hoja nzitonzito alizokuwa anazitoa bungeni juu ya kuurekebisha uchumi wa Kenya hata wakenya wengi walimtarajia atakapoingia madarakani angefanya miujiza. Lakini kama tufahamuvyo sote maneno matupu hayavunji mfupa. Alidai rushwa kwake haivumiliki lakini baada ya kuikamata dola hata wasaidizi wake wa karibu kwenye vita tajwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Utawala Bora Bwana John Githongo na Mwenyekiti wa Tume Dhidi ya Rushwa Bwana Ahmednassir Abdullahi wamemkimbia baada ya kuona siyo mkweli katika kurekebisha Katiba au kupambana na rushwa. Na hata jitihada za Rais Kibaki za kuanzisha Wizara ya Sheria na mambo ya kikatiba kama ilivyokuwa wakati wa mwasisi wa taifa hilo Bwana Jomo Kenyatta zilibeza zoezi zima la kurekebisha katiba baada ya Rais Kibaki kuendelea kumteua Bwana Amos Wako kuwa mwana sheria mkuu wa Kenya ikizingatiwa kuwa hata Bwana Moi alimteua Bwana Wako siyo kutokana na uwezo wake wa masuala ya sheria ila kwa sababu ya kuwa mtiifu kwa utawala uliopo madarakani na uteuzi tajwa wa Bwana Wako chini ya utawala wa Kibaki ulilenga kubeza marekebisho ya Katiba ambayo yalitarajiwa kujenga mazingira mazuri ya kumkomboa Mkenya wa kawaida kutoka kwenye minyonyoro ya unyonge ya wanasiasa tajwa. Alipokuwa Makamu wa Rais chini ya utawala wa Moi, Rais Kibaki aliwahi kudiriki kutamba hadharani ya kuwa KANU ingetawala Kenya milele na alikuwa mstari wa mbele katika kukiuka sheria zinazolinda haki za asili alipoliongoza Bunge la Kenya katika kumwangusha Waziri shupavu wa wakati huo Bwana Charles Njonjo kwa kutumia hoja bunifu ya kuwa Bwana Njonjo alikuwa ni msaliti na mwenye mipango ya kuipindua serikali ya Bwana Moi.

  Wakenya wengi walitupwa kizuizini chini ya sakata la Mwakenya na kuteswa sana huku Bwana Kibaki akifumbia macho ili kulinda masilahi yake binafsi wakati yeye akiwa ni Makamu wa Rais na msaidizi wa karibu wa Bwana Moi. Mapenzi ya Kibaki na KANU yalizimika mara tu ambapo Bwana Moi alipomshusha cheo kwa kumpokonya Umakamu wa Rais na kumpa cheo tajwa Dr. Karanja na kumteua Bwana Kibaki kuongoza wizara isiyo nzito ya afya. Kuanzia hapo Bwana Kibaki baada ya kuona masilahi yake binafsi yameanza kuathirika chini ya utawala wa aliyejivika uprofesa wa siasa za Kenya Bwana Moi alijitoa KANU hasa baada ya kuona upepo wa vyama vingi unavuma na KANU haikuwa njia ya pekee ya yeye kuukwaa Urais nchini Kenya. Katika uchaguzi wa Urais Kenya wa mwaka 1992 wachunguzi wa masuala ya siasa ya Kenya walio wengi wanaamini ya kuwa pamoja na kuvunjika kwa umoja wa vyama vya siasa uliokuwa unaitwa FORD kuwa ni chimbuko la upinzani kushindwa uchaguzi tajwa, Mwai Kibaki kwa kupitia chama chake cha Democratic Party aligawa kura za wakikuyu alipogombea Urais huku akielewa hatashinda na hivyo kumnyima mkikuyu mwenzie Kenneth Matiba nafasi ya kuun’goa utawala wa kimabavu wa Bwana Moi. Katika uchaguzi wa mwaka 1997 Bwana Kenneth Matiba alipojitoa kugombea Urais kwa madai kuwa katiba inakipendelea chama cha KANU na upinzani ushiriki wake kwenye uchaguzi tajwa ulilenga kumnufaisha Moi kwa kumpa uhalali asioustahili wa kisiasa, Bwana Kibaki kwa tamaa ya kuzikomba kura za wakikuyu zilizoachwa na Bwana Matiba hakumwuunga mkono Bwana Matiba ila akashiriki kwenye uchaguzi tajwa na alipoona ameshindwa na Moi akadai uchaguzi tajwa ulikuwa batili akaenda Mahakamani na aliposhindwa kumpa hati za kuitwa shaurini Bwana Moi akaanguka katika kesi tajwa. Katika uchaguzi wa mwaka 2002 alipoona kuna ugomvi ndani ya KANU juu ya demokrasia ndani ya chama tajwa katika uteuzi wa mgombea Uraisi akawa mstari wa mbele katika kuwashawishi akina Bwana Raila Odinga na wenzie kuanzisha muungano wa NARC na kuwekeana mkataba wa makubaliano wa kugawana madaraka nusu kwa nusu na chama cha siasa cha akina Raila kiitwacho LDP au Labour Democratic Party. Raila Odinga na wenzake wakamkubali Bwana kibaki kuwa mgombea Urais wa NARC kwa matarajio ya kuwa naye atatekeleza makubaliano ya mgawanyo wa madaraka baada ya kuwa Rais. Sote tunafahamu mgogoro mkubwa kati ya LDP na washiriki wengine kupitia muungano wa NAK au the National Alliance Party of Kenya ulianza tu baada ya Rais Kibaki kubeza makubaliano ya vyama tajwa kwenye uteuzi wa mawaziri, wabunge wa kitaifa, makatibu wakuu na viongozi wengi waandamizi. Kutokana na Rais Kibaki kuwasaliti washiriki wake wakuu kisiasa baada ya kukamata dola, mgogoro kati ya LDP na NAK ulisambaa hadi kuingia kwenye zoezi zima la kurekebisha katiba tajwa na hivyo kuwacheweleshea wakenya kuwa na katiba yao mapema.

  Bunge la Kenya chini ya utawala wa Moi ili kuhakikisha linadhibiti marekebisho ya Katiba tajwa liliunda chombo cha kisheria kilichojulikana kama CKRC au Tume ya kukusanya maoni ya wananchi juu ya marekebisho ya Katiba tajwa. Tume tajwa ilikusanya maoni tajwa chini ya uenyekiti wa Profesa Yash Pal Ghai na Katibu wake Bwana Patrice Lumumba. Kabla ya kuondoka madarakani Rais Moi ambaye alikuwa anatarajia chama chake kushinda uchaguzi wa mwaka 2002 aliashiria kuwa Tume ya kukusanya maoni tajwa kuongozwa na mkenya akimaanisha ya kuwa Profesa Ghai hakuwa Mkenya jambo ambalo siyo kweli. Bwana Moi kwa kumbeza Profesa Ghai ilitokana na yeye na wanasiasa wengi ndani ya KANU kutoridhika na mwenendo mzima wa Tume tajwa kwani ilionekana ikifanya kazi kwa uhuru zaidi na bila kujali sana azma ya wanasiasa ya kuidhibiti Tume tajwa. Wakati wa uchaguzi Bwana Kibaki akielewa kuwa suala la katiba mpya ni nyeti machoni pa wakenya ili kujihakikishia ushindi wa kishindo akawaahidi wapiga kura kuwa endapo watamchagua yeye kuwa Rais basi atawapatia Katiba mpya katika siku mia moja tu za utawala wake jambo ambalo hadi leo karibu miaka mitatu imepita bila kutekeleza ahadi yake tajwa. Baada ya Tume tajwa kumaliza kazi yake ya kukusanya maoni yake kutokana na nguvu ya sheria iliitisha mkutano wa Boma au National Constitutional Conference (NCC) ambao uliundwa na wabunge wote na wateule kutoka asasi huria mbalimbali pamoja na majimbo yote nane. Tume tajwa ilipitisha Rasimu ya Katiba tajwa huku Rais Kibaki na serikali yake ikiyapinga baadhi ya maeneo yanayopingana na matakwa yao niliyoyataja awali kwa kumtumia Makamu wa Rais Bwana Awori ambaye aliongoza msafara wa mawaziri walio upande wa Rais kibaki katika kujitoa kwenye Mkutano wa Boma na hivyo kuendelea kuchangia kuchelewesha kupitishwa marekebisho ya Katiba tajwa. La ajabu maeneo ambayo yalikuwa yanamkera Rais Kibaki na wenzake yalikuwa ni maeneo ambayo waliyashabikia sana walipokuwa upinzani lakini walipoingia madarakani maeneo tajwa wakayaona ni kikwazo katika azma yao ya kuikamata dola kwa milele. Walipoona Rasimu ya Katiba ya Boma itakabidhiwa kwa Mwanasheria mkuu tayari kufikishwa Bungeni ili kupitishwa timu ya Rais Kibaki ikawa mstari wa mbele katika kumhamasisha Mchungaji Dr. Timothy Njoya na wenzake saba katika kuipinga Rasimu ya Boma Mahakamani wiki moja tu tangu ilipopitishwa na Mkutano tajwa!!! Matukio yote haya yaliendelea kuwacheleweshea wakenya kuwa na Katiba yao.

  Katika hukumu ya kesi ya Njoya na wenzake dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Kenya na Tume ya Kikatiba tajwa, Jaji Mary Kasango wa Mahakama Kuu ya Kikatiba ya Kenya aliamua yafuatayo:- (1) Bunge la Kenya halina mamlaka ya kuandaa au kupitia mapendekezo ya katiba tajwa, (2) Mkutano wa Kikatiba wa Boma (NCC) ulikuwa ni batili kwani uteuzi wa wajumbe wake haukuzingatia tofauti ya idadi ya watu katika majimbo kwani majimbo yenye watu wachache yaliwakilishwa na wajumbe wengi na kinyume chake. Mahakama tajwa iliona kuna ubaguzi ulifanyika katika kuteua wajumbe wa mkutano tajwa kwa kupendelea majimbo yenye watu wachache, (3) Raia wa Kenya ni lazima waipigie kura ya maoni Rasimu itakayopitishwa.

  Rais Kibaki badala ya kuyatangaza mapendekezo ya katiba tajwa ni batili chini ya hukumu tajwa akafanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri na kuwaadhibu mawaziri aliwaona wakorofi kutoka chama mshiriki cha LDP na kuteua mawaziri kutoka chama chake cha DP na NAK na vyama vilivyoshindwa uchaguzi vya KANU, FORD (PEOPLE) na FORD (KENYA) kwa malengo ya kupata msaada wa kurekebisha katiba atakavyo kupitia Bunge ambalo tayari lilikwisha kupigwa mkwara na Mahakama ya Kikatiba. Baada ya hapo Rais Kibaki akaingia makubaliano na kiongozi asiyekubalika wa KANU Bwana Nicholas Biwott katika kuigawa zaidi KANU na kupata msaada wa kura Bungeni ili kupitisha mabadiliko ya kikatiba ambayo alishindwa kuyapata kwenye mkutano wa Boma. Bwana Biwott naye ambaye serikali ya Bwana kibaki tayari ilikwishamfungulia kesi ya madai ili kumnyang’anya jengo lake la biashara la kifahari la Yaya Center lililopo Nairobi hakuwa na la kufanya ila kuingia makubaliano tajwa ili kulinda utajiri wake alioupata kwa njia zenye utata mkubwa. Ili kukamilisha lengo la kupata marekebisho ya kikatiba atakayo na ambayo yatazingatia mahitaji binafsi ya Rais Kibaki kwenye uchaguzi ujao wa mwaka 2007 sheria zikaundwa ili kulipa Bunge madaraka ya kupitisha marekebisho ya kikatiba katika sura ya watawala watakayo na kutengua maoni ya ‘wanjiku’ ambayo ndiyo lilikuwa lengo kuu la marekebisho tajwa.

  Kwa kuubeza mhimili mkuu wa katiba ya Kenya ambayo ni Mahakama Kuu ya Kikatiba tajwa, utawala wa Kibaki umejenga mazingara ya vurugu na vurugu zinazoendelea nchini Kenya ni matunda ya ubinafsi wa viongozi tajwa.

  Kutokana na hukumu tajwa marekebisho 14 ya Katiba ya Tanzania yaliyofanywa na Bunge letu tangu tupate uhuru ni batili. Kwanza Bunge liliundwa kutunga sheria na wabunge huapa kuilinda katiba iliyopo hivyo kazi ya kuirekebisha katiba tajwa siyo yao. Bunge tajwa halipaswi kuinyambulisha Katiba ambayo wabunge tajwa wameapa kuilinda na kuiheshimu kwa muda wote wa utumishi wao bungeni. Vile vile Bunge tajwa halikuundwa kwa kazi tajwa na ndiyo maana lina matatizo ya kimuundo ambayo yanafanya matatizo tajwa ya kimuundo kulibatilisha Bunge tajwa kwa kazi tajwa. Pili muundo wa Bunge letu una upendeleo kwa majimbo yenye watu wachache hususan Tanzania visiwani. Hivyo uundaji wa Rasimu ya Katiba tajwa unahitaji chombo huria kama vile constituent assembly au chombo cha kurekebisha katiba ambacho kitazingatia idadi ya watu kutoka kila jimbo ambapo majimbo ya uchaguzi yalivyo sasa yametoa upendeleo kwa majimbo yenye watu wachache kuwa na wabunge wengi wenye kuwawakilisha watu wachache hivyo kulifanya Bunge tajwa kuwa ni batili kwa kazi ya marekebisho ya katiba tajwa. Hata Tume mbalimbali zilizoundwa kukusanya mapendekezo ya marekebisho tajwa zimeundwa bila ridhaa ya moja kwa moja ya watanzania kwa ajili ya kuifanya kazi tajwa na uteuzi wa wajumbe wake haukuzingatia majimbo yenye uwiano sahihi wa uwakilishi wa raia nchini hivyo tume tajwa ni batili na taarifa za mapendekezo yake vilevile ni batili kutokana na ubatili wa tume tajwa. Tatu, kama tulivyoona awali kwa wenzetu wanasiasa wa hapo Kenya kwa vile wanasiasa ndiyo wenye masilahi mazito kwenye marekebisho yoyote ya kikatiba hawapaswi wawe mstari wa mbele katika kuirekebisha katiba kwani watatanguliza masilahi yao mbele badala ya masilahi ya taifa kwenye marekebisho tajwa. Kwa maoni yangu binafsi, yeyote atakayechaguliwa kwenye Constituent Assembly anapaswa kuzuiwa kwa nguvu ya sheria kugombea nafasi yeyoye ya siasa angalau kwa miaka kumi ijayo baada ya kupitishwa katiba tajwa ili kuzuia masilahi binafsi ya muda mfupi ya wajumbe wa Tume tajwa kupewa kipa umbele kwenye marekebisho ya katiba tajwa na hivyo kuhatarisha masilahi ya Taifa zima. Nne, marekebisho yote kumi na nne ya katiba yetu hayana ridhaa ya wananchi ambao ndiyo ni walengwa wakuu wa marekebisho tajwa kwani mbali ya ukweli nchi yetu haina sheria ya kura maoni siyo sababu ya kukwepa kuiunda sheria tajwa ili kuitumia kuhalalisha marekebisho yeyote ya kikatiba kupitia kura ya maoni tajwa. Tano, kazi ya Bunge ni kuunda sheria ambazo zitajenga mazingira ya kukidhi yote niliyoyataja kwenye maeneo manne hapo juu na wala siyo vinginevyo.

  Vinginevyo nchi yetu itaendelea kuwa na Katiba batili kama ilivyo sasa yenye kuzingatia mahitaji ya viongozi wanasiasa wabinafsi wachache na jitihada za Taifa hili masikini katika azma yake ya kupambana na umasikini litakuwa ni zoezi lisilotekelezeka. Watanzania wenzangu mpo hapo, jamani?
   
Loading...