Mapokezi ya Dk. Slaa yatikisha Arumeru | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mapokezi ya Dk. Slaa yatikisha Arumeru

Discussion in 'Chaguzi Ndogo' started by nngu007, Mar 19, 2012.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Mar 19, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145
  JUMATATU, 19 MACHI 2012 07:24 NA MWANDISHI WETU, ARUMERU

  [​IMG]  KATIBU MKuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbrod Slaa, jana alitikisa Jimbo la Arumeru kutokana na mapokezi makubwa aliyoyapata kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), hadi viwanja vya Soko la Ndizi.
  Mamia ya wananchi wakiwa wanakimbia mchakamchaka na kushika matawi ya miti na bendera za chama hicho, walisababisha magari yaliyokuwa yakitumia barabara kuu ya Arusha-Dar es Salaam kupata usumbufu mkubwa wa kupita.

  Msafara wa Dk. Slaa, ulipambwa na waendesha pikipiki na magari zaidi ya 70, yakiwa yamepambwa bendera za chama hicho. Vijana na wazee walikuwa wamejipanga pembeni mwa barabara hadi eneo Tengeru na muda wote walionekana kupagawa. Kitendo hicho kilisababisha Dk. Slaa asimame juu ya gari la wazi na kuanza kuwasalimia kwa kuwapungia mikono wafuasi hao wa Chadema.

  Akihutubia mkutano wa kampeni katika eneo la Soko la Ndizi, Dk. Slaa alisema taifa limekumbwa na matatizo mengi yakiwano ya uchumi kutokana na viongozi waliopewa dhamana kushindwa kusimamia kile walichotumwa na wananchi.

  Alisema hali hiyo, imesababisha wananchi kuendelea kupata maisha magumu, kutokana na rasimali za taifa kunufaisha watu wachache.

  "Nawaambia ndugu zangu, mmepigika mno, viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia rasimali za taifa, wamegeuka matajiri na kuwaacha ninyi mkipiga miayo tu, hali hii Chadema haiikubali hata kidogo,"alisema Dk. Slaa.

  Kuhusu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wasira, ambaye juzi alitoa kauli za kumkashfu, Dk. Slaa alisema anashangazwa na uongo mkubwa wa waziri huyo ambao ameamua kwenda kuwadanganya wananchi wa Jimbo la Arumeru.

  "Nimesikitika sana na uongo wa Wassira, amekuja kusema uongo, badala ya kueneza sera za chama chake, anaanza kunichafua mimi.

  "Kwanza naona huyo si saizi yangu kujibizana naye, hana jipya, nimesikia anakuja kuwambia kwamba mgombea wangu Joshua Nassari hajabarikiwa na famili yake na hataki kuoa.

  "Jamani huu ni uongo wa mtu mzima, kama anaona ameshindwa uwaziri ni bora ajiuzulu tu,"alisema Dk. Slaa.

  Alisema amesikitishwa na kauli za Waziri Wasira, kuwa aliiba fedha za

  ujio wa Papa Yohana Paul wa II ambaye alikuja nchini mwaka 1991.

  Alisema kama kiongozi wa kitaifa anasimama kusema uongo hadharani, anaweza akawa chanzo cha kuligawa taifa na kuisababisha nchi kuingia kwenye machafuko.

  "Ndugu zangu, naona umefika wakati ambao siwezi kujibu ‘ujinga', unaotolewa na watu waliolewa madaraka serikalini, namtaka Rais Jakaya Kikwete amwajibishe au ajiuzulu kwa kusema uongo usiokuwa na msingi kwa madai eti ananadi sera za CCM," alisema.

  Alisema kama mgombea wa Chadema akichaguliwa, atahakikisha anamtua bungeni kwenda kuondoa panya ambao wamekuwa wakitafuta mamilioni ya fedha za walipa kodi katika halmashauri mbalimbali ambako wizi umekithiri.

  Alisema Serikali inahitaji kurekebisha mwenendo wake haraka, kutokana na mambo kuharibika yakiwamo kushuka kwa kiwango cha elimu.

  "Mchagueni Nassari ili akomboe jimbo hili kwa sababu akipiga kelele na kusimamia hoja na akiandamana na wabunge wengine watasaidiana kupigania haki za Watanzania na haki haziombwi na maandamano yanasaidia japokuwa wenzangu wanatushutumu" alisema Dk. Slaa.

  Alimtaka Nassari asimamie sera na utii kwa chama chake ili kupeleka mabadiliko kwa wananchi wa Arumeru, kwa kufuata nyayo za watangulizi wake.

  "Taifa letu lina matatizo makubwa mno, nawaambia kila kukicha napokea simu nyingi kutoka kwa walimu wakilia kwamba hawana fedha, wanakabiliwa na maisha magumu.

  "Mbali na walimu, nimepokea barua kutoka kwa askari polisi ambao wameletwa hapa kwenye kampeni, wanalipwa Sh 10,000, hii ni haki kweli ndugu zangu?, hebu niambieni kiongozi gani wa Serikali analipwa kiasi hiki? alihoji.

  Mchungaji Natse
  Kwa upande wake, Meneja Kampeni wa mgombea huyo, Mchungaji Israel Natse, alisema uchaguzi wa Arumeru Mashariki unapima joto la uchaguzi mkuu kwa kuwa unaonekana kuichanganya CCM.

  "Juzi tumemsikia Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, akizungumza familia ya Mwalimu Nyerere, jana (juzi), Wasira naye kaibuka akizungumzia familia ya mgombea, watu sijui ni wa aina gani.

  "Sasa leo (jana), naomba wazazi wa mgombea wasimame hadharani wamuumbue waziri huyu ili watu wote wafahamu CCM ni waongo wa kutupwa," alisema Mchungaji Natse na kushangiliwa na maelfu ya wananchi waliokuwa mkutanoni hapo.

  Vincent Nyerere

  Meneja mwingine wa kampeni za Chadema ambaye pia ni Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere (CHADEMA), akimnadi mgombea wa chama hicho, Joshua Nassari, alisema anamheshimu mtu mzima anayejiheshimu, lakini mtu akiamua kuvunja heshima yake makusudi, anamshughulikia.

  "Hawa CCM wanagawa rushwa shuleni wanafundisha taifa baya la wala rushwa, halafu wakipata kazi wanaomba rushwa wanawalaumu wakati wamewafundisha wenyewe, dawa ya hawa ni kuwaondoa madarakani," alisema Vincent.

  John Heche
  Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (BAVICHA), John Heche, aliwataka wananchi wa jimbo hilo kumchagua Nassari ili akawasemee matatizo yao bungeni na katika vikao husika.

  Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), alisema CCM hawastahili kuachwa wakitembea usiku kama popo na kwamba wanatakiwa kuzuiwa wasitembee usiku.

  "Naomba msiruhusu watu kutembea usiku kama popo, mkiwaona hawa watu wanagawa fedha, fanyeni mambo, sisemi mambo gani kwa sababu mnajua wenyewe," alisema Lema.

  Alisema wiki ijayo atahamia Arumeru Mashariki ili kushughulikia mafisadi na anamtahadharisha, Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowasa, asiende Arumeru kwa kuwa akienda huko, wataanika madhambi yake.

  Baba Mzazi wa Nassari


  Akijibu hoja Wasira, aliyesema kuwa mgombea wa Chadema hajapata baraka na wazazi wake kwa sababu ni mtoto mtukutu na amekataa kuoa, baba mzazi wa mgombea huyo, Mchungaji Samuel Nassari alikanusha vibaya tuhuma hizo.

  "Mwanangu hajawahi kunivunjia heshima hata siku moja na tangu asome shule ya msingi hadi Chuo Kikuu, hajawahi kurudishwa kwa kukosa nidhamu.

  Alisema suala la kuoa sio sawa na vitunguu ambavyo mtu anakwenda kuvinunua sokoni na kwamba wakati wa kuoa Nassari ukifika baada ya Mungu kumuonyesha hivyo, ataoa.

  Mchungaji Samuel, alisema familia yao walimpa baraka zote kijana wao na Machi 5, mwaka huu, viongozi wa Chadema walifika nyumbani kuomba baraka na walimpatia na kusema kuwa maneno mengine ni propaganda ambazo hazimsumbui.

   
 2. Muke Ya Muzungu

  Muke Ya Muzungu JF-Expert Member

  #2
  Mar 19, 2012
  Joined: Jun 17, 2009
  Messages: 3,451
  Likes Received: 30
  Trophy Points: 0
  rais wa ukweli. mwacheni yule feki wa magogoni
   
Loading...