Norbert Mporoto
Member
- Jul 18, 2020
- 14
- 12
Na: Norbert Mporoto
Tanzania.
Katika karne ya leo kuna michezo ukichezewa hata kama ni ya kuudhi au kuumiza bado inatia hamasa kuendelea kuchezewa, kwani maumivu yake kwa asilimia tisini huja kwa mfumo wa furaha. Michezo ya namna hii huwa naiona ni sawa na ile ya paka na panya kucheza mchezo mmoja pasipo kudhuriana wala kuhitilafiana. Au la, hufanana na shauri la mwewe kwa mama kuku ya kwamba awaache vifaranga watembee peke yao ili wapate nguvu na uzoefu wa kujimudu na kuyamudu mazingira.
Popote pale penye uwepo wa michezo ya namna hii basi amini kuna upande mmoja kati ya hizi unapoteza haki yake ya msingi; cha kushangaza ni kwamba upande huo huwa haulioni jambo hili kiasi cha kuendelea kuucheza mchezo huu pasipo kupoteza ari, kasi na nguvu ya kushiriki. Na zaidi ni kwamba sheria za mchezo huwa zipo wazi kwa kila mmoja, huwa inaudhi na kusikitisha pale unapobaini ukweli wa makosa ya mchezo huu ni ya makusudi kabisa. Mbaya zaidi, timu pinzani ikakiri mapungufu hayo kwa lugha nyepesi kabisa ya kusamehe saba mara sabini japo ushindi huo batili unabaki mikononi mwao.
Inaumiza sana kuchezewa akili kana kwamba mabega yetu yametwika maboga na si vichwa, inaumiza sana kushuhudia mapinduzi haya anuai yenye lugha nyepesi za kutubembeleza tulale mchana kweupe, kana kwamba sisi ni watoto tusiojua uhalisia. Na haya ni mapinduzi ya kimawazo. Wapo ambao husema ni fedheha kuzianika habari au sifa mbaya zinazomhusu marehemu mbele ya ndugu zake! Labda! lakini kama ni ukweli je tuufiche kwa kumpamba marehemu asiyekuja fufuka? Au tuweke bayana na kutoa kipaumbele ili mambo haya yaeleweke vichwani mwa kila mmoja wetu ili tu kulinusuru kundi kubwa la ‘wafu hai’ ambao wako njiani kupotelea njia ileile ya marehemu wa kwanza? Kama mabega yetu yamejitwika vichwa basi mbadala wa pili ni sahihi zaidi.
Afrika leo hii inakabiliwa na janga la mapinduzi ya kimawazo (na ifahamike kuwa si jambo geni) kipindi tukiendelea kuhesabu miaka ambayo hesabu zake hazijawahi kamilika kufikisha muongo wala karne. Hofu inatanda zaidi pale inapotubidi kuzihesabu hatua za mraba ili kuikamilisha safari hii tukiwa hatujui hata idadi ya vidole mikononi mwetu viliyoshikilia vitendea kazi; basi wakati tukiendelea kufikiri juu ya majawabu ya hesabu hizo si vibaya nikisawili na kuaangazia baadhi ya mambo ambayo yanaweza leta majibu ya kwanini, ili kuielewa dhana ya mapinduzi ya kimawazo ilivyojikita barani Afrika.
Kwanza, kutafunwa na kudhoofishwa kwa mihimili ya kiutawala na sekta adhimu kiasi kwamba haifai tena kuwa mwegamo wa mataifa yetu katika kunusuru walio wanyonge. Kama ambavyo wengi wetu tunavyoamini kwa asilimia kubwa bara la Afrika ni bara huru, lakini katika uhalisia wake bara hili si huru. Ni ajabu kujiita bara huru au nchi huru wakati hadi sekunde hii Afrika haina uamuzi wake, Afrika bado inaamuliwa, Afrika inachochea maafa ya kuuana ndugu kwa ndugu kupitia tawala za viongozi wetu, na zaidi viongozi wa Afrika wanatuongoza wakiwa na sura mbili (moja ya ukoloni mamboleo na nyingine ya uzalendo wa kinafiki machoni petu) zilizojengeka kwa kile kinachoitwa ufadhili, urafiki na uhisani.
Je ni kwamba nchi zetu zimeshindwa kuyamudu mambo yetu hadi tuwe tunaamuliwa kama familia yatima zisizo na walezi? Labda! Ila palipo na ndimi mbili ukweli hupita kama pambo la kinywa na si kweli itokayo moyoni. Endapo hali hii itabaki hivi pasipo kuzisimamia ndwele za mataifa yetu itatuchukua muda usiojulikana hadi pale tutapothubutu na kuamini kwamba jukumu la kuziendesha na kuzijenga nchi zetu (ili zilete maana ya uhuru halisi na sio ile ambayo wengi wetu wenye vichwa vyepesi kama manyoya ya sufi wamekuwa wakiamini) ni la kwetu sisi waafrika na si vinginevyo.
Afrika inajengwa na kuandaliwa kuwa bara tegemezi kupitia nchi zake zisizo na umoja. Utegemezi ni kitu kibaya sana kisichofaa kuendekezwa mahala popote pale. Kuna ile hadithi ya kipofu na kiwete, wote hawa wana mapungufu. Siku moja kiwete alikaa sana na kuwaza namna na njia rahisi ya kuwa anatembea sehemu mbalimbali bila kusumbuka. Baada ya kuichosha sana akili yake alikuja na majibu akimtaka kipofu waungane kulingana na mapungufu yao ili waweze kusaidiana kuzimudu changamoto za mapungufu yao, basi kiwete akamtaka kipofu awe anambeba mabegani na yeye atakuwa akimuongoza kwa kuelekea, na zaidi atakuwa akimpa chakula cha siku kama malipo ya ridhaa yake kuwa pamoja na kiwete. Ikawa hivyo, kipofu pasipo kufikiri faida na hasara zake akaridhia makubaliano hayo, mwishowe alijikuta ni mtu wa kumtembeza kiwete kila uchao! Kadri siku zilivyokwenda kipofu alidhoofu kwa sababu nduguye alizidi kuwa mzito kupita kiasi.
Kama ambavyo kiwete aliona mbali, basi na mataifa ya ulaya leo hii fikra zao zinaishi karne ya thelathini, na wanaona dhahiri mataifa ya Afrika yamekuwa juu yao. Hivyo jitihada zao kila kukicha ni kuzidhoofisha akili zetu kwa kila namna, na wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa maana leo hii Afrika tunafikiri ila mawazo yetu hayavuki urefu wa pua zetu (ashakum si matusi, kiukweli inakera) na tunategemea mambo mazuri kwa hisani ya watu fulani.
Mwalimu Nyerere alishawahi kusema “siku moja akitokea kiongozi wa Taifa letu, akatuambia huko nje kuna hela nyingi kuliko hapa nyumbani, mwambieni wewe ni mpumbavu” Mantiki yake ni kuwa suala la utegemezi ni zaidi ya donda ndugu au ukoma, ni jambo la kulipinga na kulikwepa. Sisi kama hatulioni hilo, basi tufikiri pia wale waliotufanya kuwa watumwa hawawezi kutusaidia kiasi tukawa juu yao hata siku moja. Wanachoweza kutufundisha ni kuwa tegemezi kwao, kwa dini yao, kwa utamaduni wao, kwa mila na pesa zao kama tunavyoshuhudia leo hii. Tumenasa mtegoni na kuona kuwa hatuwezi kuendelea sisi kwa sisi, katika mchezo huu wa mapinduzi ya kimawazo nakiri na kutanabaisha kuwa uwezo wetu wa kufikiri mbinu za wapinzani wetu ni mdogo kiasi kwamba ni ngumu kuibuka na ushindi, japo tukishikamana tunaweza.
Ufikiri wa watu wetu umegeuka na kuwa mzigo kwa taifa, kizazi kilichopo ni cha kipekee chenye unasaba wa kudai na kulaumu. Ni matokeo ya kukumbatia mapinduzi ya fikra tegemezi katika dunia ya vita, watu wetu wapo kufani! Kama ambavyo binadamu hafi mara mbili basi wameshakufa kwani hakuna hata mmoja aliyekufa na akakumbuka kufufuka au kujifufua. Bado naamini kuwa tunachezewa michezo ya maudhi isiyoudhi kwa wakati kwani hata ukichezewa rafu basi unapenda uchezewe tena. Ni akili za wapinzani tu! Huu ni msiba wa kujitakia, kanuni nitaivunja na sitoacha kulia nanyi.
Imani yangu ni kwamba yule anaemjua mbwa kwa jina lake (hata awe mwizi) huwa hahangaiki kutimua mbio. Shida yetu ni kwamba tumekuwa wepesi wa kuiga baadhi ya mambo pasipo kuzingatia na kuyatizama vema hatima yake, Amerika wanafanya hayo wakijua nini maana yake, Ulaya wanafanya hivyo wakijua nini wanahitaji, hata Ujerumani, Japan, na mataifa mengi wanafanya wakitambua wazi nini muafaka wake. Tatizo lipo kwetu sisi tunaoiga, na kufanya hayo bila kusawili na kuelewa hatima yetu.
#Makala #AfrikanaUtawala #Mapinduziyakimawazo