Mapanki ya Mwanza sasa yatua Feri Dar | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mapanki ya Mwanza sasa yatua Feri Dar

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Rutashubanyuma, Dec 26, 2010.

 1. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #1
  Dec 26, 2010
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 158,613
  Likes Received: 419,254
  Trophy Points: 280
  Mapanki ya Mwanza sasa yatua Feri Dar
  Saturday, 25 December 2010 21:26

  Salim Said
  SOKO Kuu la samaki Feri jijini Dar es Salaam, limeanza kupoteza uhalisia wake baada ya kutawaliwa na vichwa na mifupa ya sangara (mapanki), kutoka ziwa Viktoria.

  Sakata la mapanki liliibuka nchini kwa mara ya kwanza mwaka 2006 baada ya Mtengeneza Filamu wa Australia, Hurbert Sauper kutayarisha mkanda wa filamu ya ‘Darwin’s Nightmare’ (mapanki), ukionyesha jinsi watanzania wanavyokula mapanki na minofu kupelekwa ulaya kwa ndege. Kufuatia hali hiyo, serikali na bunge lilitoa maoni yao huku Rais Jakaya Kikwete akipinga vikali maudhui ya filamu hiyo na kusema kwamba kama hoja ni umasikini basi umasikini upo kila mahali duniani.

  Lakini uchunguzi wa Mwananchi Jumapili umebaini kuwa, mapanki yamepata soko kubwa jijini Dar es Salaam kutokana na kupanda kwa gharama za maisha , hivyo watu wengi kushindwa kumudu gharama za kununua samaki wabichi. Mapanki hayo huuzwa kwa Sh1,000 kichwa au mfupa wa Sangara wanaoingizwa sokoni hapo kupitia wafanyabiashara wakubwa na kuwauza kwa wachuuzi ambao huuza rejareja. Mwananchi Jumapili imebaini kuwa, kwa kila mwezi soko la Feri hupokea kilogramu 1,000 hadi 3,500 za mapanki kutoka Mwanza.

  Afisa Uvuvi wa soko hilo, Fidelis Ntima aliiambia Mwananchi Jumapili kuwa mapanki wanaingizwa kwa wingi katika soko la Feri na kwamba wamewekwa katika kundi la samaki wa barafu (Frozen fish) wanaoingia kutoka nje.

  “Vifua na vichwa vya sangara kutoka Mwanza (mapanki), vinaingia kwa wingi hapa na takwimu zetu zinaonyesha kuwa kila mwezi huingia kati ya tani moja hadi tatu na nusu,” alisema Ntima na kuongeza: “Julai tulipokea mapanki kilogramu 1,500, Agosti kilo 3200, Septemba kilo 2,100, Oktoba kilo 900 na Novemba kilo 800.” Mchuuzi mdogo wa samaki safi wa baharini sokoni hapo, Amir Issa alisema kuingia kwa mapanki sokoni hapo kunawaathiri sana kibiashara kwa kuwa watu wengi huamua kununua mapanki kwa sababu wanapatikana kwa bei rahisi.

  “Wanatuathiri kwa sababu wanauzwa bei rahisi, sasa watu wengi hawahitaji wanakula nini kwa ubora gani, wanahitaji kula wanachopata kwa ubora wowote,” alisema Issa ambaye pia ni katibu wa Chama cha Wachuuzi cha Vusha. “Lakini kama mtu ukitaka samaki basi samaki wetu ni wazuri kwa sababu hawajakaa katika barafu kwa muda mrefu, lakini pia ladha yake ni nzuri.” Kwa upande wake Mvuvi, Ramadhan Mwigah alisema hivi sasa katika soko hilo wanakabiliwa na mgogoro na ushindani mkali kutoka samaki wa viwandani kutoka Mwanza na China, India na Yemen.

  “Hawa wanauzwa kwa bei rahisi sana, hii inasababisha hata bei ya samaki wa mvuvi wa hapa kuanguka mwisho wake mnapata hasara. Kwani wanaletwa kwa wingi mno, makontena kwa makontena,” alisema Mwigah. Mwananchi imebaini jumla ya makontena tisa ya futi 40 yanayotumika kuhifadhia mapanki na samaki hao kutoka nje ya nchini. “Wale wa Mwanza si samaki bali ni makapikapi tu au mapanki ya sangara lakini wanatuathiri sana kibiashara,” alisema Mwigah.

  Mwigah aliongeza, “Kama viwanda hivi na wafanyabiashara wakubwa wanaoingiza mapanki na samaki kutoka nje, wana nia ya kusaidia jamii, basi watuwezeshe sisi kwa kutupa mikopo ya zana za kisasa za kuvulia halafu wanunue samaki tunaovua. Hili linawezekana, kama Mwanza limewezekana kwa nini lishindikane Dar?” Alisema soko la Feri limopeteza uhalisia wake badala ya kuwa soko la samaki halisi wabichi kutoka baharini limekuwa soko la biashara mchanganyiko na samaki kutoka nje na mapanki kutoka Mwanza.

  “Halina tofauti na soko la Buguruni, Tandale, Tandika au Magomeni kila kitu kinapatikana hapa,” alilalamika Mwigah. Kwa upande wake Meneja wa Soko hilo, Hemed Mdoe alikiri kuwepo kwa athari kubwa ya kibiashara na kisekta inayosababishwa na mmiminiko wa samaki wa barafu kutoka nje pamoja na mapanki.

  “Hii inadumaza sekta nzima ya uvuvi wa Tanzania. Unapoingiza samaki kutoka nje au mapanki kutoka Mwanza wakati una samaki safi wa ndani ‘automatic’ (moja kwa moja), kutakuwa na ushindani,” alisema Hemed. “Sasa hoja ni je wavuvi wako wataweza kukabiliana na ushindani huo? Hii utakuta inadumaza sekta lakini kutokana hali halisi huwezi kuwakataa.” Alifafanua kuwa, samaki hao aidha wanapitia bandari kuu au mipakani lakini serikali kupitia wizara husika ina taarifa zote juu ya usalama na faida ya samaki hao.

  “Sisi hapa hatuna mkataba wowote na wafanyabiashara hawa wanaoingiza samaki hawa, ila kuna mabwana afya nadhani wanafanya ukaguzi na serikali inajua kupitia wizara husika,” alisema Hemed.
   
 2. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #2
  Dec 26, 2010
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 158,613
  Likes Received: 419,254
  Trophy Points: 280
  Nionavyo mimi mwakani hali ya uchumi itakuwa mbaya sana hata hayo mapanki tutayatafuta na tusiyaone maana yatakuwa yakiuzwa kwa bei mbaya na yatakuwa nje ya uwezo wa kiuchumi wa watanzania wengi....................
   
Loading...