Maoni ya kambi rasmi ya upinzani bungeni kuhusu hali ya uchumi wa taifa, mpango wa maendeleo wa taifa na makadirio ya mapato na matumizi 2019/2020

Goliath mfalamagoha

JF-Expert Member
Aug 3, 2012
602
2,505
MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KUHUSU HALI YA UCHUMI WA TAIFA, MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2019/2020
Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016


MAENEO YA KIPAUMBELE KATIKA BAJETI MBADALA
210. Mheshimiwa Spika, Bajeti mbadala ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni itakua na vipaumbele katika sekta zafuatazo;



Jedwali Na. 2 : Mgawanyo wa Fedha katika Sekta za Kipaumbele
Na. Sekta Kiasi (Tshs.) Asilimia (%)
1. Elimu 4,354,671,556,500.00 15
2. Kilimo 5,806,228,742,000.00 20
3. Viwanda 4,354,671,556,500.00 15
4. Maji 2,903,114,371,000.00 10
5. Afya 2,903,114,371,000.00 10
6. Mengineyo 8,709,343,113,000.00 30
7. JUMLA 29,031,143,710,000.00 100


ZE. HITIMISHO

211. Mheshimiwa Spika, naomba kumalizia hotuba yangukwa kusema kwamba kusuasua kwa uchumi wetu kumetokana na kutokuwa na mfumo wa uchumi unaoeleweka. Serikali hii ya awamu ya tano, haijui inafuata mfumo gani wa uchumi. Nimeeleza kwa kirefu hapo awali jinsi ambavyo mfumo wetu wa uchumi umepitwa na wakati na jinsi ambavyo hauendani na mahitaji ya dunia ya sasa; Aidha, nimeeleza madhara ya uchumi kuhodhiwa na Serikali jambo ambalo limeua nguvu ya soko katika kuamua mustakabali wa uchumi. Kutokana na madhaifu hayo ya mfumo wetu wa uchumi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeniimependekeza mfumo wetu wa uchumi kufanyiwa marekebisho makubwa ikiwa ni pamoja na kupendekeza mfumo mpya wa uchumi ujulikanao kama Mfumo wa Uchumi wa Soko Jamii (Social Market Economy) – Mfumo ambao ni wa kisasa kabisa duniani; ili Taifa liweze kujinasua na matatizo ya kiuchumi ambayo yamelifanya taifa hili kuwa masikini kwa miongo yote mitano toka tupate uhuru.
212. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imeeleza pia kwamba ukuaji wa uchumi na ustawi wa watu ni matokeo ya utawala bora. Hivyo, ujenzi wa uchumi imara ni lazima uende sambamba na utawala bora. Kama kuna tishio la usalama – kwa maana ya watu kutekwa na kuteswa wakiwemo wafanya biashara wakubwa; kama kuna ukandamizaji wa demokrasia na haki za binadamu; kama hakuna uhuru wa habari; kama hatuna mahusiano mazuri ya kidiplomasia na Jumuiya ya Kimataifa n.k tusitegemee uwekezaji wa maana katika nchi yetu.
213. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imeonyesha pia namna bajeti hii ya nne ya Serikali ya awamu ya tano ilivyojikita kwenye maendeleo ya vitu badala ya maendeleo ya watu. Takriban asilimia 40 ya fedha za maendeleo zimetumika kugharamia miradi mitatu tu iliyopo katika Wizara mbili; yani wizara Nishati na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Miradi hiyo ni SGR, Stieglers Gorge, na Ufufuaji wa Shirika la ndege. Jambo hili limesababisha fedha za maendeleo katika sekta nyingine zinazoguza moja kwa moja maisha ya wananchi kama vile afya, kilimo, elimu maji,mifugo na uvuvi kupungua sana.
214. Mheshimiwa Spika,naomba nimalizie kwa kusema kwamba; “hili taifa ni letu sote” Hakuna Mtanzania mwenye sifa za utanzania zaidi ya mwingine – wote ni watanzania. Kwa hiyo, kitendo cha watawala kuona kwamba wao ni bora zaidi na kutuita sisi wenye mawazo mbadala kwamba si wazalendo na kwamba tunapinga maendeleo ni kauli za kibaguzi na hazilijengi taifa bali zinalipasua. Serikali iwe inapokea changamoto na mawazo mbadala kutoka upinzani na kuyafanyia kazi.
215. Mwisho kabisa Mheshimiwa Spika, Serikali iache kufanya propaganda katika mambo ya msingi hasa katika bajeti ya Serikali. Tumeeleza kwa kirefu jinsi Serikali inavyowahadaa wananchi kwa kuweka makisio makubwa ya ukusanyaji wa mapato ambayo inajua kabisa kuwa haiwezi kukusanya na hivyo kuwapa wananchi matumaini hewa! Kwa kuwa Serikali hii ya awamu ya tano ilikuwa bingwa sana kukabiliana na vitu hewa – kuanzia wafanyakazi hewa na madai hewa ya watumishi; ijisafishe na yenywe kwa kuacha kupanga bajeti hewa kwa maendeleo ya taifa hili.
216. Mheshimiwa Spika,baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.


David Ernest Silinde (Mb)
KNY:WAZIRI KIVULI WA FEDHA NA MIPANGO
NA MSEMAJI MKUU WAKAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI,
KATIKA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO
17 Juni, 2019
 
Back
Top Bottom