MAONI: Je, Demkrasia ya Vyama Vingi Ni suruhu ya Matatizo ya maendeleo Afrika?

Mbogela

JF-Expert Member
Jan 28, 2008
1,384
257
Miaka ya 1960 ilikuwa miaka ya ukombozi wa Afrika. Nchi za kiafrika zilizokuwa kwenye mapambano kujitoa katika utawala wa wakoloni zilijikuta hatimaye zilipata uhuru wake. Vita na mapambano ya Ukombozi sio jambo lilioanza mara moja, bali ni jambo ambalo limekuwepo toka wakati wakoloni wanakuja Afrika.

Vita hii ya Ukombozi iliongozwa na vyama, ambavyo mwanzoni vilikuwa vyama vyenye malengo ya kupigania Uhuru na baadaye baada ya uhuru vikaja vikawa vyama vya kisiasa ambavyo vikaweka malengo yao ya kisiasa ya kushika dola na kutawala.

Huu ulikuwa ni upepo wa uhuru na ilikuwa hamna namna ilikuwa lazima nchi za kiafrika na zingine zilizokuwa bado katika makucha ya wakoloni kupata uhuru. Nchi nyingi zikapata uhuru wake with exception of very few such as Mozambique, Angola etc.

Mwanzoni mwa miaka ya 90 upepo wa mabadiriko ya kisiasa ulivuma kwa nguvu kubwa sana katika bara la Afrika. Nchi nyingi za Kiafrika zilizokuwa zinafuata siasa ya Ujamaa zilijikuta zikibadili mwelekeo na kuchukua siasa ya soko huru (ubepari). Kutokana na kubadirika kwa itikadi kutoka itikadi ya ujamaa kwenda itikadi ya ubepari, mfumo wa vyama vingi ukaanzishwa. Mageuzi haya yalichagizwa zaidi na kushindwa kwa mfumo wa siasa wa nchi za kijamaa za ulaya ya mashariki, kuanguka kwa uliokuwa muungano wa Kisovieti, kuanguka kwa ukuta wa Berlin. Huu nao ulikuwa ni upepo, nchi zote zilizokuwa zinaegemea itikadi ya siasa ya ujamaa zikabadili mwelekeo wake na kushika itikadi ya soko huria na Ubepari.

Vyama Vingi vya Siasa

Kutokana na mabadiriko ya mfumo wa siasa kipindi cha miaka ya 1990 tukaona upepo mwingine ukivuma katika bara la Africa, Upepo wa vyama vya siasa vilivyodai ukombozi kuondoka katika madaraka na dola kushikwa na vyama vya upinzani. Wananchi wengi wa nchi za Afrika Mashariki na Kati waliokuwa wamechoshwa na tawala za Kiimla kutoka kwenye vyama vyao vilivyodai Uhuru, walikimbilia aidha kuanzisha vyama vya upinzani au kujiunga na vyma vilivyokuwa vimeanzishwa kwa malengo ya kuchukua dola na kubadirisha mfumo wa siasa, uchumi, kuongeza upatikanaji wa huduma za jamii, ukuaji wa demokrasia na haki za binadamu na kuboresha maisha ya wananchi wao.

Nchi zilizokumbwa na wimbi hili ukanda wa Afrika mashariki na kati ni pamoja na Kenya, Zambia, Malawi kwa njia ya sanduku la Kura, lakini nchi zingine kama Uganda, Rwanda, Burundi na Congo kwa njia ya mapinduzi ya kijeshi. Lakini Kila nchi ilipita njia yake hata hivyo matokeo ya mwisho yaliekea kufanana, nayo ni vyama vilivyoleta uhuru kuondoka Madarakani na nchi kuongozwa na vyama vya upinzani (waliofanyanya mageuzi kwa sanduku la Kura) au waasi (kwa upande wa nchi zilizofanya mapinduzi kijeshi).

Zambia
Nchini Zambia katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1991 wananchi wakakiamini chama cha upinzani cha Movement for Multparty Democracy (MMD) na kumpa nafasi ya Urais mgombea wake Bwana Frederick Jacob Titus Chiluba kuwa rais wa Pili baada ya kumshinda Baba wa taifa la Zambia Bwana Keneth Kaunda wa United National Independence Party (UNIP).

Chama Cha MMD kiliendelea kushinda chaguzi zilizofuata chini ya Levy Patrick Mwanawasa (2001, 2006) ambaye alifariki mwaka 2008. Mwaka 2008 Rupia Banda alishinda uchaguzi kupitia chama hicho hicho cha MMD. Hata hivyo baada ya Miaka 20 ya kuongozwa na kilichokuwa chama cha Upinzani MMD wananchi walikatishwa tamaa sana na serikali iliyoko Madarakani na kuamua kuiondoa kwa kura kwa kukipa ushindi chama kingine cha upinzani cha Patriotic Front cha Michael Sata katika uchaguzi wa mwaka 2011.

Kwanini wananchi walikatishwa tamaa na MMD pamoja na kuwa kilikuwa chama cha Upinzani walichokiamini na kutegemea kuona mengi kwa chama hicho?. Tafiti mbali mbali zinaonyesha kuwa moja ya sababu ya MMD kushindwa kufanya vizuri kulitokana MMD kushinda uchaguzi wa kwanza kwa bahati tu kutokana na wanachi kukichoka chama kilichoko Madarakani cha UNIP cha Mzee Kaunda. UNIP ilichukiwa na wananchi kwa sababu ya hali ngumu ya maisha iliyowakabili wazambia wakati huo. Wazanvia wengi waliona Matatizo ya kiuchumi na hali ngumu ya maisha waliyokuwa wakipitia ilikuwa imesabababishwa na UNIP.

Kutokana na kuanguka kwa soko la Shaba iliyokuwa njia kuua ya uchumi ya Zambia, maisha ya wazambia yalikuwa magumu sana. Lawama za ugumu wa maisha zilikiendea Chama kilichokuwa madarakani cha UNIP na Serikali ya Bwana Kaunda. Hivyo ulipofika uchaguzi wananchi waliona namna pekee ya kurekebisha mambo yao ni kukiondoa chama Tawala UNIP na kumuangusha mzee Kaunda kwani alionekana ni mzee na hakuwa na solution tena za matatizo yao.

Wakati huo chama kilichokuwa kinafanya active politics kilikuwa ni MMD na Chiluba akaonekana ni an alternate solution. Hivyo tunaweza kusema Chiluba alishinda uchaguzi wa kwanza kwa Ngekewa (bahati) tu na sio kwa mikakati na ushindi wa uzuri wa sera.

Chama Cha Chiluba MMD kilijikuta kinaingia Madarakani bila kujiandaa kikiwa hakina Sera, hakina namna ya kusimamia yale yaliyokuwa maono yao, hakikuwa na watendaji wa kuona kuwa wanafanya yale yanayoendana na itikadi, sera na Imani ya chama. Hivyo chama kikapokea mfumo na watendaji wale wale lakini kwa jina lingine.

Chini ya Utawala wa MMD Hali ya Maisha nchini Zambia ikazidi kuwa ngumu sana, Thamani ya pesa (Kwacha) ikazidi kuporomoka sana, hali ya Rushwa na ufisadi ikaongezeka na kufikia kiwango cha juu sana (kiasi cha watu kumiliki pesa katika mapipa na kuzifukia katika bustani zao za uani).

Wananchi wa Zambia walikatishwa Tamaa sana wakaamua kufanya mageuzi mengine, safari hii hakufikiria tena kurudi kwa UNIP chama cha ukombozi, huko walishatoka, wakasonga mbele na kutafuta matumaini mengine, matumaini ya kweli ya kuwakomboa kutoka minyororo ya ugumu wa maisha, wakampata Mkombozi Michael Chilufya Sata wa Patritic Front mwaka 2011. Sata na Chama Chake wapo madarakani, hatujui itawachukua muda gani kabla ya wananchi wao hawajawa disappointed nao.

Malawi
Mwenendo wa kisiasa kwa majirani zetu Malawi haukuwa tofauti sana na Zambia. Baada ya wananchi kukichoka chama cha Ukombozi cha Malawi Congress Party (MCP) kilichoongozwa na Hastings Kamuzu Banda. Bila kusoma alama za Nyakati masikini Banda akaingia kichwa kichwa kwenye uchaguzi uliohusisha vyama vingi mwaka 1993 na kujikuta akidondokea pua mbele ya Elson Bakili Muluzi na chama chake cha United Democratic Front (UDF) na baadaye kumrithisha swahiba wake Bingu wa Mutharika mwaka 2004.

Kama ilivyo kuwa kwa MMD ya Zambia, UDF ya Malawi ilipewa ridhaa na wananchi kuongoza dola wakati wakiwa bado hawajajiandaa, hawakuwa wanajua wawafanyie nini wamalawi pale baada ya kupewa nchi. Matokeo yake walijikuta wakirithi mifumo ya uendeshaji nchi ile ile, viongozi wa idara zote nyeti walibaki wale wale, na hata utartibu wa namna ya kufanya maamuzi ukawa ule ule. Nchi ikawa haina vipaumbele tena, nchi ikajikuta inayumba yumba kwa kukosa mwelekeo.

Kutokana na wananchi kuipa UDF nchi bila wao UDF kujiandaa, walishindwa kuimudu nchi, kiwango cha rushwa kikapanda na kuongezeka sana Malawi, Thamani ya sarafu yao (Kwacha) ikaporomoka vibaya mno, Hali ya maisha ikawa ngumu.

Kama walivyofanya wananchi wa Zambia, wananchi wa Malawi wakawa hawana Alternaltive bali kubadili chama cha utawala mbapo katika uchaguzi wa mwaka 2009 wakakipa chama cha Democratic Progressive Party (DPP) pamoja na kuwa mwanzilishi wake alikuwa huyo huyoBingu wa Mutharika lakini kilikuwa ni chama tofauti na kile cha Bakilu Mluzi cha UDF ridhaa ya kuongoza nchi.

Kenya
Suala la Kenya ndio liko More complicated kuliko nchi zingine. Siasa za Kenya pamoja na kutawaliwa na hisia za ukabila lakini nazo zilipita katika mlolongo ule ule wa kukatishwa tamaa na watawala wa vyama vya ukombozi na kuamua kuchagua vyama vya upinzani ambao siasa za Zambia na Malawi zilipita.

Lakini tofauti na nchi za Malawi na Zambia Kenya Imekuwa na utitiri wa vyama vya siasa (zaidi ya vyama 190 vilivyosajiliwa), na sheria ya vyama vya siasa Kenya inaruhusu Vyama kuungana wakati wa uchaguzi na hii inasababisha unapofika wakati wa uchaguzi kuanza kusikia jina lingine maarufu ambalo hujawahi lisikia. na hivyo kuvifanya vyama vinavyoungana wakati wa uchaguzi huingia mkataba wa kuongoza.

Miaka ya 90 baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi wananchi wa Kenya walionyesha disappointment kubwa kwa chama chao kilichowaletea Uhuru cha Kenya African National Union (KANU). Hivyo wakaamua kuwekeza nguvu zao kwa vyama vya upinzani.

Mwaka 2002 Mzee Mwai Kibaki alishinda uchaguzi kupitia muungano wa upinzani wa The National Rainbow Coalition (National Alliance of Rainbow Coalition - (NARC). Mwai KIbaki na Muungano wake wa NARC hawakuwafikisha Wakenya kwenye matamanio yao, na wakenya walijikuta wameaangushwa mapema zaidi kuliko walivyotegemea Kwani baada ya kura ya maoni ya katiba ya mpya ya mwaka 2005 Serikali ilishindwa katika kura hiyo. Wananchi walitaka serikali ijiuzuru/ivunjwe, hata hivyo badala ya serikali kujiuzuru alichofanya Kibaki ni kuwatimua wenzie waliounda wote ushirika wa NARC.

Waliofukuzwa wakatoka nje na kuunda muungano wa Orange (ODM) ambao baadaye ukaja ukavunjika nao na kuunda makundi mawili yenye kusigana, ODM (Raila Odinga) na ODM-Kenya (Kalonzo Msyoka). NARC nayo ikagawanyika katika makundi mawili, Kundi la Charity Mwilu (NARC) na NARC-Kenya ya Mwai Kibaki.

Wakenya wakasubiri uchaguzi mwingine wa 2007 ufike baada ya miaka mitano ya utwala wa Mwai Kibaki ili wafanye marekebisho baada ya kuwa dissapointed na hawa wapinzani walioingia kwa mwavuli wa NARC kushindwa kufikia maatarajio yao.

Ulipofika uchaguzi wa mwaka 2007 Mwai Kibaki ilimlazimu kutumia nguvu ya ziada kubakiza kiti chake cha urais. Na mbaya zaidi Kenya ilijikuta inaingia katika machafuko makubwa. NARC (Asili) ya Charity Mwilu kilichokuwa kimeshinda kwa asilimia 61% dhidi ya KANU (31%) ya Uhuru Kenyatta mwaka 2002 ilijikuta inapata viti 3 tu kimoja kati ya hivyo kikiwa cha Charity Mwilu mwenyewe.

Baada ya machafuko ya baada ya uchaguzi ilisababisha kuundwa kwa serikali ya kitaifa, ambayo ilisababisha wanasiasa maarufu kuingia ndani ya serikali. Katika uchaguzi mwingine wa 2013 wakenya walifanya mageuzi baada ya kumpigia Uhuru Kenyata na Muungano wake wa Jubilee.

Tanzania

Majirani wa Tanzania wote kasoro Msumbiji wamebadirisha vyama vya siasa kutoka vile vilivyoleta uhuru kwenda vile vyama vya upinzani. Kwa vile upepo huu wa kuviondoa vyama vilivyoleta uhuru umekuwa mkubwa sana kwa Afrika hata zile nchi ambazo hazikuwa na siasa za vyama za moja kwa moja kama Libya, Misri, Algeria zilijikuta zinafanya mapinduzi makubwa kuwaondoa watawala na vyama vyao vilivyoleta Uhuru. Nchi kama Afrika ya kati na Guinea nazo hazijasalimika kwa upepo huu unaovuma wa kuondoa vyama vya vilivyoleta Uhuru na kuingiza vyama vya upinzani au makundi ya upinzani.

Kwa kuangalia haraka haraka unaona kabisa upepo huu unavuma kuielekea Tanzania. Wahenga walishasema ukiona mwenzio ananyolewa wewe kichwa tia maji. Wapembuzi wa mambo ya kisiasa wanaonyesha wasi wasi kama CCM itasalimika kwa upepo huu wa kung'oa vya vya siasa vilivyoleta Uhuru ambao unavuma kwa kasi kubwa kuanzia miaka ya 90.

Ukifikiria kuondoa chama tawala lazima ufikirie chama cha upinzani unachoweza kukiamini na kukikabidhi nchi. Lakini watu wanaviangalia vyama vya upinzania ambavyo vinapewa nafasi ya kupewa ridhaa ya kuongoza nchi. Kufuatia idadi ya wabunge na idadi ya Kura wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2010 CHADEMA inaonekana ina nafasi Kubwa. Ukiongeza na hali ya kisiasa ilivyo kwasasa nchini (hatujui hali itakuwaje baada ya mvutano wao na Zitto Kabwe kuisha) inaonyesha CHADEMA kinaweza kuaminiwa na wananchi katika UCHAGUZI wa 2015 kuongoza dola.

Lakini watabiri wa mambo ya kisiasa wanasema kuwa CHADEMA nayo inaweza kubahatika kushinda uchaguzi huo kwa mazingira na sababu zile zile za vyama vya siasa vya upinzani vilivyoaminiwa huko Kenya, Zambia na Malawi kama nilivyoonyesha mwanzoni mwa andiko hili. Wachambuzi wa mambo ya kisiasa Wanaona kuwa wananchi wataichagua CHADEMA sio kwasababu ya sera zake nzuri, sio kwasababu ya mkakati wake madhubuti wa kuwaondoa watu kwenye matatizo yao. Wanaona CHADEMA itachaguliwa kwa bahati tu na kwasababu kubwa ya watu wameichoka CCM.

Kutokana na hilo CHADEMA nayo inaweza ikaingia katika makosa ambayo vyama vingine vya upinzani vilifanya Afrika Mashariki na kati ya kujisahau mpaka vinakabidhiwa nchi bila kujiandaa kuongoza nchi. Hivyo basi kutokana na hilo CHADEMA itachukua nchi ili hali haina maandalizi, haijui nini ifanye, iwapeleke wapi watanzania.

Kama CHADEMA itapewa nchi pasi kujiandaa nini kitatoea? Ninaona kuwa kutokana na CHADEMA kukabidhiwa nchi kwa ushindi wa ngekewa katika muda mfupi tu Watanzania wataweza kukatishwa tamaa na maendeleo yanayopatikana kwa CHADEMA. Watu wanaiona hali ya maisha magumu kwa watanzania kuongezeka, wimbi la umaskini, ujinga na maradhi kukua. Hivyo baada ya hapo watanzania watahitaji kutafuta chama kingine mbadala.

Hivyo basi kutokana na hilo inakuwa muhimu sana kwa aidha NCCR-Mageuzi au CUF au chama kingine kuanza kujipanga kwa Take-over kutoka kwa CHADEMA. Ndio maana ni muhimu kuanza kuandaa chama kingine mbadala mbacho kitabeba matumaini ya kweli ya watanzania, Chama kitakachokuwa kimetengeneza mkakati wa namna ya kuwaondoa watanzania hapa walipo kuwapeleka kwenye hatua ya juu zaidi. Chama ambacho kitaweza kuruhusu ustawi wa Demokrasia, kuheshimu haki za Binadamu na utawala wa sheria. Chama ambacho kitakuwa na malengo maridhwa ya kiuchumi na kijamii. Chama ambacho kitatumia rasmali za nchi kwa ajili ya watanzania, Chama kitakachokuwa na maono ya kuona living standard ya kila Mtanzania inakuwa that of acceptable level.

Watanzania wanapaswa kujiandaa kisaikolojia ili kupokea matokeo ya dissapointment lakini wakati huo huo wanaohusika na active politics za vyama waanze kuandaa vyama vyao ambavyo vitafufua matumaini ya watanzania. Vyama ambavyo vinaweza kuja kutuliza munkari wa watanzania wa kupata maendeleo sawia, maendeleo ya watu, maendeleo yanayoweza kuwafanya wajisikie wapo kwenye nchi yao ya kuzaliwa.

Mungu Ibariki Tanzania.
 
Back
Top Bottom