Hongera Rais Samia: DUNIA inashuhudia kufunguliwa kwa siasa za vyama vingi na shughuli zake katika ardhi ya Tanzania

MIMI BABA YENU

JF-Expert Member
Mar 1, 2019
295
679
DUNIA inashuhudia kufunguliwa kwa siasa za vyama vingi na shughuli zake katika ardhi ya Tanzania, si kwa kauli bali vitendo hasa baada ya wiki nzima kuwa na mvutano juu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutangaza maandamano ya amani.

Jina la Rais Dk. Samia Suluhu Hassan litaendelea kutajwa kwenye midomo ya wapenda haki, wanaojua maana ya uhuru wa kujieleza na kutumia mbinu za maridhiano kuleta maendeleo ya nchi.

Wakati wa vuguvugu la kuanza upya mfumo wa vyama vingi nchini mnamo mwaka 1992, mambo kama haya yalikuwepo, mivutano, maandamano, askari kuwazuia wafuasi wa vyama vya siasa kwa mabomu ya machozi, risasi bandia au virungu.

Katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vya siasa mwaka 1995, kiongozi wa upinzani Augustino Lyatonga Mrema aliyegombea urais kwa tiketi ya Chama cha NCCR-Mageuzi ndio alikuwa na wafuasi wengi. Kauli zake zilisikika na kufuatwa na kundi kubwa la wananchi kwa wakati huo.

Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), walijawa hofu; wakaona dhahiri mgombea wao Benjamin William Mkapa hatafua dafu. Wakaenda kwa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere kushitaki.

Majibu ya Mwalimu Nyerere yaliwanyong’onyeza wote waliomfuata, ambao walilalamika Mrema anabebwa mabegani, akifika kwenye mkoa anatandikiwa khanga na gari kuzimwa huku akisukumwa.

Waliona hiyo ni ishara ya kuwavutia hata ambao walikuwa hawajui siasa ni nini wala nguvu au uwezo wa Mrema ni upi. Walitaraji majibu yatakayowapa faraja. Lakini Mwalimu aliwaambia kuwa Mrema aachwe abebwe, akasisitiza kuwa na yeyote anayetaka kubebwa kama maiti basi asizuiwe.

Masuala ya upinzani katika eneo lolote la nchi hayazuiliki, wakati Mwalimu Nyerere na wenzake wanapambana kupata uhuru wa Tanganyika kutoka kwenye makucha ya Waingereza katika miaka ya 1950; bado kulikuwepo na Waafrika waliozaliwa na kukulia Tanganyika waliunda vyama vya upinzani.

Baadhi ya vyama hivyo ni pamoja na African National Congress (ANC) cha Zuberi Mtemvu, All Muslim National Union of Tanganyika (AMNUT) ambacho kilikuwa chama cha Waislamu wazalendo wa Tanganyika pamoja na Tanganyika Democratic Party (TDP) cha Balozi Kasanga Tumbo huku vyama hivyo vikipewa nguvu na chama cha United Tanganyika Party (UTP) kilichoanzishwa na Gavana wa Tanganyika wakati huo Edward Twinning mwaka 1956 huku baadhi ya Waafrika wakiwa wanachama.

Utaona ni namna gani kina Mwalimu Nyerere walipata tabu kupambana na nguvu iliyotokana ndani yao (Waafrika),lakini baada ya kupata uhuru Disemba 9, 1961na kufanyika uchaguzi wa vyama vingi baadaye, ilipofika mwaka 1965 Mwalimu Nyerere akiwa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliamua kufuta mfumo wa vyama vingi nchini ili kuleta utulivu wa kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Baadaye kutokana na takwa la kimataifa Tanzania iliamua kurejea kwenye mfumo wa vyama vingi mnamo mwaka 1992.
Hakuna kipindi kigumu katika uongozi wa Tanzania kama kuanzia mwaka 1992 hadi 2005. Mtikisiko mkubwa wa kisiasa ulipatikana, viongozi wa juu wakiongozwa na Mzee Ali Hassan Mwinyi (Rais wa Awamu ya Pili), Benjamin Mkapa (Rais wa Awamu ya Tatu) na baadaye Jakaya Kikwete (Rais wa Awamu ya Nne) walitumia uvumilivu wa hali ya juu kuhakikisha nchi inavuka salama; na walifanikiwa.

Hata hivyo, Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Pombe Magufuli alikuja na falsafa yake – alitaka utulivu wa kisiasa ili afanye maendeleo. Alichoshwa na kelele za wapinzani kudai mambo ambayo pengine aliona hayana msingi. Akazuia shughuli za kisiasa kuanzia maandamano, mikutano ya hadhara isipokuwa kwa wabunge wa jimbo husika pekee.

Kwa kipindi chote cha uongozi wake madarakani kuanzia Novemba, 2015 hadi mauti yalipomkuta Machi 18, 2021. Tanzania haikuwa na vuguvugu la kisiasa. Ingawa minong’ono ilikuwa mingi.
Dk. Samia Suluhu Hassan alichukua kijiti na kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania manmo Machi 19, 2021. Matumaini mapya yakaanza kuonekana kwenye sura za Watanzania hasa viongozi wa vyama vya kisiasa.

Kila aliposimama kuzungumza na wananchi matarajio ni lini vyama vya siasa vitatoka kifungoni. Ndipo Januari 3, 2023 akatangaza kuruhusu mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa nchini na kuondoa marufuku iliyokuwepo kwa muda mrefu.

Rais Dk. Samia kauli hiyo aliitoa mbele ya viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa alipowaita Ikulu ya Dar es Salaam, alisema: “Uwepo wangu mbele yenu leo ni kuja kutangaza kwamba lile tangazo la kuzuia mikutano ya hadhara sasa linaondoka.”

Hiyo ilikuwa habari njema mbele ya viongozi wa vyama vikuu vya siasa za upinzani nchini akiwemo Freeman Mbowe wa CHADEMA, Profesa Lipumba wa C.U.F na Zitto Kabwe wa ACT-Wazalendo.

Pengine tamko lile lilionekana na kawaida, lilionekana la kisiasa au kuondoa ungo juano, kama wasemavyo Waswahili. Lakini tukio la jana kuruhusiwa wafuasi wa CHADEMA kufanya maandamano kwenye jiji kubwa lenye shughuli nyingi kama Dar es Salaam, ilithibitisha haikuwa porojo.
Jana Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA na mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi alimpongeza Rais Dk. Samia wa uongozi wake wa maridhiano kwa kuruhusu maandamano.

“Big up kwa Polisi, tunawaahidi amani mwanzo mwisho. Big up sana pia kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa hili,” amesema Mbilinyi.
Sugu ameongeza kuwa Rais Samia ameonesha kuwa hana hulka ya kutumia vyombo vya ulinzi na usalama kuminya demokrasia.

Naye Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, amewapongeza Polisi chini ya Rais Samia kwa ushirikiano wao kwa chama chake.
“Nalipongeza Jeshi la Polisi kwa busara hii. Karibuni Watanzania wote, tuandamane kwa amani,” Mbowe amesema.

Falsafa ya R4 (Reconciliation, Resilience, Reforms na Rebuilding of the Nation) ya Rais Samia imebadili upepo wa siasa nchini.
Hii siyo mara ya kwanza kwa Serikali ya Rais Samia kuruhusu maandamano ya upinzani. Mei, 2023, Polisi jijini Dar es Salaam waliruhusu maandamano ya Umoja wa Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) kwenda Ofisi za Bunge na kuwapatia ulinzi.

Kama hiyo haitoshi Rais Dk. Samia pia ameongeza uhuru wa wananchi wa kuongea, uhuru wa vyombo vya habari na asasi za kiraia.

Wananchi kadhaa wakitoa maoni yao kupitia kwenye mitandao ya kijamii wamemtaja Rais Samia kama “Mama wa Demokrasia” wa Tanzania kwa uongozi wake wa maridhiano
-------------------
 
Back
Top Bottom