Nimeshangaa sana majimbo yaliyowatupa wabunge walioitishia sana serikali kwa madai kuwa hawakufanya lolote kwao na kuwatafuta watu ambao ni "marafiki" wa serikali ili wawe wabunge wao.
Kazi ya Mbunge siyo kusimamia au kuanzisha miradi ya maendeleo jimboni kwake, bali ni kuwawakilisha wananchi wake katika kusimimamia na kuikemea serikali ihakikishe kuwa inafanya mambo yake kama ambavyo jamii inavyotaka. Ukishakuwa mbunge mkali unayefanya kazi yako sawasa kiasi cha kuogopwa na serikali, basi serikali hiyo itahakikisha kuwa miradi yote iliyopangwa kufanyika jimboni mwako itatekelezwa kusudi usije ukaikaba koo.
Watanzania tumekuwa na tabia ya utegemezi sana kiasi kuwa tunategemea mbunge eti ndiye atufanyie mambo, kwa mfano niliwahi kusoma ripoti ya mbunge mmoja huko Singida kuwa alitumia pesa zake binafsi kufanya mambo mengi sana pale jimboni mwake. Hiyo ni vizuri lakini alikuwa akifanya hivyo kama sehemu ya philanthropy yake kwa vile ni mtu tajiri, siyo kama mbunge; anaweza kufanya hivyo bila kuwa mbunge, na inaweza kuchukuliwa kuwa hiyo ilikuwa ni hongo.
Niliwahi kusoma ripoti ya mbunge wa Musoma inayoonyesha jinsi gani anavyochangiwa na matajiri duniani ili kujenga miradi ya mendeleo ya hali ya juu sana jimboni kwake, ingawa hilo ni jambo zuri, ni jambo ambalo angeweza kulifanaya bila kuwa mbunge vile vile; kufanya hivyo kama mbunge ni namna ya hongo pia. Iwapo utakuwa na mbunge ambaye ni lobbyist mzuri wa kuleta miradi jimboni hata ambayo haiko kwenye mipango ya serikali, ni vizuri kwa jimbo lakini ni kinyume cha sheria na haitusaidii katika jitihada zetu za kujenga mfumo wa kidemokrasia unaoheshimu sheria; ni hongo pia kwa wapiga kura wake.
Ni vizuri tuwapime wabunge kwa jinsi walivyotekeleza wajibu wao kama wabunge wetu kuliko kuwapima kwa jinsi walivyotuhonga.