Malecela aitikisa CCM mara nyingine

Status
Not open for further replies.

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,029
Malecela aitikisa CCM mara nyingine

na Martin Malera
Tanzania Daima

SASA ni dhahiri kuwa John Samuel Malecela ndiye mwanasiasa anayeshikilia kwa nafasi kubwa hatima ya mshikamano na uimara wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati huu chama hicho kikikabiliwa na changamoto nyingi na nzito za kisiasa dhidi ya wapinzani wake.
Vikao vikubwa vitatu vya juu vinavyokutana makao makuu ya chama hicho Dodoma kuanzia kesho, ndivyo ambavyo vitatoa mwelekeo mpya ambao ama utasaidia kukiimarisha au kukimega kutokana na kuwa na ufa wa makundi unaokiandama kwa miaka mingi sasa.

Jina la Malecela mwenye umri wa miaka 73 sasa aliyeshikilia nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara kwa miaka 17 sasa kuanzia mwaka 1992 akichukua nafasi hiyo kutoka kwa Simba wa Vita, Rashid Kawawa ndilo linalotajwa pengine kuliko majina yote ya vigogo wa chama hicho.

Wanaomtaja Malecela wakiwamo watu wanaomuunga mkono na wale wanaompinga wana swali moja kubwa vichwani mwao. Je, ataendelea na wadhifa wake huo au ni nani aliyejiandaa, au kuandaliwa kuichukua nafasi yake hiyo ambayo mwaka 2002 jitihada za kumng’oa ziligonga mwamba?

Wakati watu wakifakari kuhusu suala hilo huku wakijua fika kwamba, siri ya suala hilo anayo Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, baadhi ya wachambuzi wa mambo wanamuangalia kama nguzo ya uimara wa chama hicho, huku wengine wakimuona kuwa kikwazo cha dhamira ya kundi moja la chama hicho linalofanya jitihada za kujenga kile wanachokiita CCM- Mpya.

Tayari wachambuzi kadhaa wa mambo wakitumia vyombo vya habari, wameanza kuyataja majina ya wanasiasa kadhaa kama Waziri Mkuu Edward Lowassa, Katibu Mkuu Yussuf Makamba, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, mwanasiasa wa siku nyingi, Kingunge Ngombale-Mwiru na Abdulrahman Kinana kuwa wanasiasa wanaopewa nafasi kubwa kumrithi Malecela katika nafasi hiyo.

Hata hivyo, kila mwanasiasa anayetajwa pamoja na kuonekana kuwa na sifa za kuchukua nafasi hiyo kutokana ama na ukaribu wake na Rais Kikwete, uwezo wake wa kisiasa au rekodi yake ya utendaji, bado kila anayezungumzwa anaonekana kuwa na mapungufu kadha wa kadha yanayoweza yakawa kikwazo cha mmoja wao kuchukua nafasi hiyo muhimu.

Hata hivyo, kundi la watu wanaotetea mshikamano ndani ya chama hicho, wanataka kuona Malecela yeye mwenyewe akipewa nafasi ya kuchagua hatima yake badala ya kutaka kuchukuliwa kwa hatua zitakazomlazimisha kung’oka kwa namna ile ilivyofanyika wakati wa mchakato wa kumsaka mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Mei mwaka 2005.

Wale wanaomuunga mkono Malecela, wanasema ukongwe wake katika nafasi hiyo uliomjengea mtandao wa kukubalika ndani ya CCM, hata kukisaidia chama hicho kukabiliana vilivyo na upinzani, ndiyo sifa kuu ya kuendelea kumwacha aendelee kushika wadhifa wake huo, katika kipindi kingine cha miaka mitano.

Watu wa kundi hili wanaamini kuwa Rais Kikwete akitumia hekima zenye mwelekeo huo, huku akiwa na dhamira ya kudhihirisha kifo cha kundi la mtandao ambalo limekuwa likimpiga vita kisiasa Malecela, anaweza kumpa tena wadhifa huo ili kurejesha heshima iliyopotea wakati wa mchakato wa urais mwaka 2005.

Si Kikwete tu, bali hata ndani ya CCM kundi moja linalomuunga mkono Malecela linafanya hivyo, likitetea haja ya kukifanya chama kuendelea kuwa na Makamu Mwenyekiti wa Tanzania Bara mwenye uwezo wa kufanya kazi kwa uhuru na asiye na majukumu ya kiserikali.

Sifa hii aliyonayo Malecela, ndiyo ambayo kwa upande mwingine inawafanya wanasiasa wengine kama Makamba na Kinana kuonekana nao wakiwa na nafasi kubwa ya kupendekezwa kuchukua nafasi hiyo ya Malecela.

Wanaomtaja Malecela pia wanaweka bayana hofu waliyonayo kuwa iwapo atalazimishwa kuondoka katika wadhifa huo safari hii tena, kama alivyofanyiwa mwaka 1995 na 2005 kwenye urais, basi kuna uwezekano mkubwa wa yeye na wengine wenye mtazamo kama wake, kuchukua maamuzi yanayoweza kukigharimu chama hicho.

Hata hivyo, wale wanaompinga Malecela, siku zote hoja yao kubwa imekuwa ni umri wake kuwa mkubwa hata kumfanya alazimike kuchukua uamuzi wa yeye mwenyewe kung’atuka kama walivyopata kufanya wanasiasa wengine kama Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na baadaye Kawawa.

Kwa hakika, Malecela atakuwa na bahati iwapo wanasiasa kama Kingunge na Emmanuel Nchimbi, wote wajumbe wa Kamati Kuu ambao mwaka 2002 walijaribu kumg’oa bila mafanikio, watarejesha makali yao yaliyoshindwa miaka mitano iliyopita.

Kama ilivyokuwa mwaka 2002, Malecela atakuwa akitarajia kutumia turufu yake ya kutetewa na wakongwe wengine kama walivyofanya Benjamin Mkapa, Ali Hassan Mwinyi na swahiba wake wa siku nyingi, Dk. Salmin Amour, wakati huo, hata kumwezesha kuendelea kuwa Makamu Mwenyekiti.

Katika siku za hivi karibuni, kundi linalompinga Malecela limekuwa likisema kuwa changamoto mpya zinazokikabili chama hicho tawala kutoka kambi ya upinzani kutokana na hoja za wanasiasa chipukizi wa kariba ya akina Zitto Kabwe na wengine, ni mambo yanayoweza kutumika kuwa chachu ya kumng’oa mkongwe huyo.

Watu wenye mtazamo huu wanasema, wanasiasa wa aina ya Zitto wanapaswa kujibiwa na wanasiasa wenzao wa rika lao ndani ya CCM, ambao hivi sasa wanashindwa kupata fursa ya kuwa na sauti kutokana na kutokuwa na nafasi za kiuongozi ndani ya CCM.

Hoja hii inaifanya CCM sasa ianze kuangalia uwezekano si tu wa kumng’oa Malecela, bali kuanza kuiona nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Tanzania Bara ikipaswa kwenda kwa wanasiasa wa rika la akina Nchimbi, Frank Uhahula na wenzao wa umri huo, ambao wanaweza kukabiliana na changamoto mpya ndani ya chama hicho.

Kimsingi kundi hili la wale wenye mtazamo huu, wanafikia mahali pa kutokuwa tayari kuona wanasiasa kama Lowassa wakipewa nafasi ya Makamu Mwenyekiti kumrithi Malecela na hivyo kupendekeza kuwa pengine Kinana au Makamba ndiyo walio na sifa zaidi.

Kundi hili la wachambuzi wanasema, kwa upande mwingine, Lowassa anapaswa kuwa mwangalifu sana kuukwepa wadhifa huo kwani iwapo ataingia katika mtego wa kuukubali, basi kuna uwezekano mkubwa kuwa mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yanayotarajia kutokea kabla ya mwishoni mwa mwaka huu yanaweza yakamkumba.

Maoni ya kundi hili bado yanaweza yakakosa nguvu kutokana na mtazamo binafsi wa Kikwete kwa rafiki yake huyo wa kikazi ambaye mahusiano yao binafsi yanaonekana kuendelea kushamiri hata baada ya baadhi ya watu kuanza kudai kuporomoka kwa ukaribu wao kisiasa katika siku za hivi karibuni.

Pamoja na baadhi ya watu kuanza kudai kuwapo kwa dalili za Lowassa kuwekwa kando na Kikwete katika wadhifa wake wa sasa, matukio ya wazi yameendelea kuonyesha kuwa, ukaribu wa wanasiasa hao wawili ambao ubia wao kisiasa ulianza kuonekana mwaka 1995, haujatetereka tofauti na baadhi ya wadadisi wa mambo wanavyodai.

Nje ya makada hao, kwa miezi kadhaa iliyopita, jina la Sumaye nalo limekuwa likitajwa kuwa miongoni mwa wanasiasa wanaopewa nafasi ya kuchukua nafasi hiyo ya Malecela.

Pamoja na Sumaye kuwa na sifa za kustaafu serikalini akiwa na umri mdogo na uzoefu mkubwa alioupata katika kipindi cha miaka 10 akiwa Waziri Mkuu, bado kuna nafasi finyu sana kwa Kikwete kulitaja jina lake kama pendekezo lake la kuwa Makamu wa Mwenyekiti kwenye kikao cha Kamati Kuu kama ilivyo ada ndani ya CCM.

Nje ya homa hiyo ya nafasi ya Malecela, mchuano mkubwa zaidi unaofananishwa na ‘vita ya kisiasa’, unaonekana kuwa katika ‘kapu’ la ‘vigogo’ 59 linalopaswa kutoa watu 20 tu! Kabla ya kifo cha Salome Mbatia, kapu hilo lilikuwa na watu 60.

Pengine ni kutokana na ugumu huo, kwa takriban miezi miwili ziara za viongozi wengi wa chama na serikali mikoani zilikuwa hazikauki - lengo kubwa likiwa kujinadi kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa (CCM).

Katika kapu, kuna wazito kama Waziri Mkuu, Lowassa, Sumaye, waziri mkuu aliyemwachia ‘ziwa’ Lowassa, Katibu Mkuu wa CCM, Makamba, naibu wake, Jaka Mwambi, naibu katibu mkuu wa zamani, Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Emmanuel Mwambulukutu, orodha ndefu ya mawaziri na manaibu waziri pamoja na wabunge mashuhuri wote wanakabiliana kusaka nafasi 20 za Tanzania Bara kupitia kundi hilo la kifo.

Wengine waliopitishwa katika kundi hilo ni pamoja na mkongwe wa siasa tangu enzi za TANU, Kingunge Ngombale-Mwiru anayekabana koo na wajukuu zake katika kapu la CCM akijivunia ukaribu wake na Rais na kundi la mtandao kwa ujumla.

Kwa sasa, Kingunge mwenye umri wa zaidi ya miaka 70 hivi (si takwimu rasmi), ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia siasa na uhusiano wa jamii.

Wengine ni Tarimba Abbas, Filbert Bayi, Shy-Rose Bhanji, Enock Chambiri, John Chiligati, Siwajibu Clavery, Dk. David Mathayo, Said Masoud Fundikira, Christopher Mwita Gachuma, Arbogast Godogodo, David Holela, Jared Kadunga, Charles Kagonji, Dk. Deodorus Kamala, Constantine Kanyasu, Profesa Juma Kapuya na Alhaj Said Kilahama.

Wengine katika kundi hilo ni Haidah Kilua, Kinana, Lukas Kisasa, John Komba, William Lukuvi, Pascal Mabiti, Dk. Milton Mahanga, Amos Makala, Novatus Makunga na Mohamed Yakub Mamoon.

Pia wamo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Wilson Masilingi, Maurus Mhimbira, Mohammed Mkumbwa, Dk. James Msekela, Dk. Ibrahim Msengi, Jackson Msome, Profesa Idrisa Mtulia, Profesa David Mwakyusa, Aggrey Mwanri, Abeid Mwinyimsa na Job Ndugai.

Orodha ni ndefu kwani inawahusisha pia William Ngeleja, Dk. Banda Salim, Salim Khamis Salim, Abdul Adamu Sapi, Isidore Shirima, George Simbachamwene, Amos Siyantemi, Dk. Hashim Twaakyondo, Frank Uhaula, Profesa Samuel Wangwe, Stephen Wassira ‘Tyson’ na Nicholaus Mateso Zacharia.

Hata hivyo mtazamo uliopo ni kwamba, wakubwa wengi kama Shein, Lowassa na Makamba wanaweza kujikuta wakipata kura za kiitifaki kutokana na utamaduni wa chama hicho kutoa picha ya kuwaunga mkono viongozi wao kama ilivyokuwa mwaka 2002.
 
Status
Not open for further replies.
Back
Top Bottom