30.
Naam, ilikuwa sura ambayo ilitosha kabisa kuufariji ubongo uliochoka kwa kusoma aina mbalimbali za vitabu, uso ambao ulibebwa na umbo ambalo ni burudani kamili kwa fikra za mtu ambaye muda mwingi wa maisha yake aliutumia kuandika burudani za watu wengine, mtu kama hayati Patauli Kongomanga. Hayo yalipita katika kichwa cha Joram pindi akiendelea kujiuliza ama hisia zake zilikuwa kweli kuwa huyo ndiye
aliyekuwa hawara au mpenzi wa Patauli. Kadri anavyowafahamu waandishi walivyo watu wanaoishi katika ndoto za ajabuajabu, na wanaopenda kufanya maisha halisi kuwa ndoto na dunia sehemu tu ya ndoto hiyo; aliamini kuwa hata mapenzi kwao ni ndoto ya mahaba, ndoto isiyo na upande wa pili ambao ni dhiki na maudhi. Nani ambaye angefaa kuikamilisha ndoto hiyo zaidi ya mwanamke, mzuri aliyehitimu katika kila fani ya kumstarehesha mwanaume? Mwanamke ambaye kula yake inategemea jitihada na mafanikio yake kitandani. Na ni yupi mwanamke huyo katika baa hiyo zaidi ya Betty?
Betty ambaye sasa alikuwa kajilaza chali kitandani, macho kayalegeza huku kwa sauti ndogo ya huba akinong’ona, “Njoo… Nadhani naweza kukuamini… Malipo baadaye…”
Ilikuwa picha ya aina yake, picha inayotisha na kupendeza kwa wakati mmoja, picha inayoshawishi na kuvutia, moja kati ya zile picha ambazo hufanya akili ya mwanaume ihamie kisogoni na kujikuta ikifuata matakwa ya mchezaji katika jukwaa, badala ya akili yake timamu. Hata hivyo, haikuwa picha mpya kiasi hicho kwa Joram Kiango. Alichofanya ni kuendelea kusimama katikati ya chumba hicho, akiimalizia sigara yake. Kisha, kwa sauti tulivu alisema, “Vipi Betty… sikujua kama nawe hu shemeji kula.”
“Kwani vipi jamani?” Betty aliuliza kwa mshangao kidogo. “Mimi ni shemejio,” alieleza. “Nilichohitaji ni kuzungumza
nawe tu.”
“Kuzungumza!” Betty alifoka kike. “Kuzungumza! Wakati wenyewe wanasubiri nusu ya chochote utakacholipa! Wewe vipi kaka! Unajua niliondokea kukuheshimu sana?” akasita kidogo. Kisha, “Kwanza yamekuaje hayo ya shemeji! Kwa nani?”
“Hayati Patauli… alikuwa rafiki yangu mpenzi…”
Betty alimkatiza kwa ukali kidogo, “Mwongo! Nipishe niende zangu. Kumbe nawe u mmoja wao! Hamchoki kunifuatafuata? Nipishe…”
Kiasi Joram alishangaa kidogo. Hakutegemea kama ingekuwa rahisi kiasi hicho. Alichotegemea hasa ungekuwa ubishi mwingi na Betty kujifanya hamfahamu kabisa marehemu. Baada ya ubishi huo angeambulia kununua ukweli au uongo ambao angeuchambua na kuungaunga hata apate uchochoro aliokuwa akiuhitaji. Hata hivyo, hiyo pamoja na urahisi huo, hisia fulani zilimfanya Joram ahisi kuwa ukali katika sauti ya Betty ulikuwa
wa bandia na hata maneno hayo aliyatamka kama aliyeyakariri kwanza. Hivyo, alimtazama kwa makini pindi akijifunga vazi lake taratibu na, hatimaye, kuanza kutoka.
“Usiwe na haraka kiasi hicho bi Betty,” Joram alimshika mkono. Akamwambia taratibu, “Nimekuita tuzungumze tu juu ya marehemu, mpenzi wako. Nipo tayari kuilipia kila dakika ambayo nitakupotezea. Au hujui kuwa alikupenda sana?”
Betty alimbetulia macho na kumtazama Joram kwa makini zaidi, “Alinipenda ndiyo… mie pia nilimpenda… lakini wewe ni nani? Watu wengi sana wamekuwa wakinifuatafuata kwa maswali ambayo hata sielewi yanaelekea wapi. Hata nahofia maisha yangu sasa. Sijui wanataka kuniua kama walivyomwua yeye…”
Ilikuwa nafasi ambayo Joram asingeipoteza. “Unadhani ni kweli walimwua?”
“Bila shaka,” Betty alifoka. Kisha, dalili za hofu ziliurudia uso na sauti yake alipouliza tena, “Wewe ni nani? Sijisikii vizuri kuzungumza na mtu nisiyemfahamu.”