Makinda, Ndugai wametuharibia Bunge

Makinda, Ndugai wametuharibia Bunge

Dingswayo

JF-Expert Member
Joined
May 26, 2009
Posts
4,019
Reaction score
2,932
Prudence Karugendo
​

FIKIRIA mbunge anasimama bungeni na kutamka kwa kujiamini, akimlenga mbunge mwenzake, kuwa mimi siongei na mbwa bali naongea na mfuga mbwa! Mwendesha Bunge, spika au naibu spika, anaridhia tamko hilo bila kumchukulia hatua yoyote ya kimaadili msemaji!


Mbunge mwingine anaamka na kufyatua matusi ya nguoni huku akilindwa na kiti cha spika au naibu spika. Yaani Bunge linageuzwa mahali pa watu kukomoana kwa kutumia itikadi za kisiasa huku upande mmoja ukiwa unalindwa kwa kile kinachoonekana kuwa mmoja na wahusika wakuu!


Ila wakiamka wabunge waungwana, hasa wa upande wa pili, kwa lengo la kutekeleza majukumu yaliyowapeleka bungeni, wanaonekana wasumbufu na wakaidi. Wanatolewa kwa nguvu nje ya Bunge na kupewa adhabu kulingana na anavyojisikia spika au naibu spika na wakati mwingine wenyeviti wa Bunge, kinyume cha kanuni za Bunge!

Hivi sasa wananchi tumeduwaa, hatuelewi ameingia shetani gani katika jumba hilo la wawakilishi wetu. Maana miaka yote tangu wawakilishi wetu waamue kujipandisha hadhi na kujiita waheshimiwa huku sisi tuliowatuma tukibaki ndugu, tumekuwa tukiamini kwamba bungeni ni mahali pa kukutania waheshimiwa wabunge wetu, watu waungwana na waadilifu wanaowawakilisha wapiga kura wao. Sidhani kama kuna mwananchi yeyote aliyewahi kufikiria kwamba bungeni anaweza kuingia mbwa.

Mbwa ataingiaje bungeni? Anamwakilisha nani? Lakini kwa vile mbunge alitamka bungeni kwamba yeye haongei na mbwa, na aliyekuwa anaongoza Bunge akanyamaza, ni wazi alikubaliana naye kwamba mle bungeni kuna mbwa.

Hivyo wananchi wangetaka kujua huyo mbwa ameingiaje bungeni na anamwakilisha nani. Ni jukumu la spika au naibu spika kuwafafanulia wananchi jinsi mbwa alivyoingia bungeni na kuachiwa ashiriki mijadala ya vikao vya Bunge.
Hilo likishindikana itabidi wananchi tuwatake spika na naibu wake wawajibike kwa kulidhalilisha Bunge letu, hivyo kuidhalilisha nchi na wananchi. Hayo ndiyo yatakayokuwa madhara ya kulichukulia Bunge kama kijiwe cha wahuni. Mtu kutoa kauli asiyojua kiwango cha madhara yake na ikaruhusiwa bila kuhojiwa na wahusika wakuu, inaweza kuwa dawa ya kutufundisha umakini wa useme nini, wapi na wakati gani.

Maana duniani kote hakuna mahali ambako mbwa, hata wawe wamefundishwa kwa kiwango gani wanaachiwa washiriki vikao vya bunge. Hiyo inaweza kuifanya Tanzania iwe nchi ya kwanza duniani yenye ‘ansadi' inayoonesha malumbano ya mbunge na mbwa ndani ya vikao vya bunge!


Kwa hiyo kwa kulifuta hilo ili lisionekane lilikuwa kweli, ndipo inapomlazimu aliyeruhusu kauli hiyo ibaki kama ilivyotamkwa bungeni awajibike kiuzalendo kwa manufaa ya nchi.

Sababu si kitendo cha kizalendo hata kidogo mtu kuiacha nchi ikadhalilika kwa lengo la kuilinda nafasi anayoishikilia au kwa mategemeo ya kupanda ngazi. Uzalendo wa mtu ndio unaopaswa umpandishe ngazi na si vinginevyo. Na mzalendo wa kweli, kama tulivyo baadhi yetu, hawezi kuacha nchi yake idhalilike kwa matarajio ya yeye binafsi kupata kitu fulani. Kumwachia mbunge amwite mbunge mwenzake mbwa, tena ndani ya Bunge, ni kitendo kinachokinzana moja kwa moja na uzalendo.

Katika hatua nyingine, tutaona kwamba wapo wabunge wasioelewa kilichowapeleka bungeni. Baadhi yao wamejigeuza wasemaji wa serikali na chama tawala! Mfano, mbunge analalamikia uchochezi wa kidini unaoanza kuota mizizi hapa nchini, anatoa ushahidi ulio katika CD alioupata katika taasisi fulani.


Badala ya hoja hiyo kujibiwa na serikali iliyo na dhamana ya kuwahakikishia wananchi kitu kama hicho hakitokei katika jamii yao, anajitokeza mbunge eti kujibu hoja husika! Je, mbunge huyo anaelewa kilichompeleka bungeni kweli?

Pamoja na kuelewa ubaya wa mfumo tulionao wa kuipata serikali ndani ya wawakilishi wa wananchi, kwa maana ya wabunge kuteuliwa kuwa mawaziri, hivi kweli mbunge anapaswa kujikomba kwa serikali kiasi hicho akiwa amewasaliti kabisa wapiga kura wake? Sababu wapiga kura wanamtaka mbunge wao aisimamie na kuiwajibisha serikali ili iweze kuendesha nchi kiuadilifu, lakini si mbunge kujigeuza msemaji wa serikali.
Ni katika hatua hiyo ya wabunge kutaka kuiwajibisha serikali, katika nchi za wenzetu, wabunge hucharuka kiasi cha kufikia hata kumrushia mayai viza waziri mkuu. Hiyo yote ni kuonesha kwamba hawana mchezo katika kuwawakilisha wananchi.

Wabunge wanaweza kutoleana maneno makali na hata kuchapana ngumi ikibidi, yote hiyo ni katika kukitetea na kukilinda walichotumwa na wapiga kura wao. Hiyo ni tofauti kabisa na Peter Serukamba aliyetoa matusi ya nguoni bungeni. Sijui yeye alikisimamia kipi. Hivi kweli Kigoma Mjini wanaweza kusema walimtuma mbunge wao akafyatue matusi yale bungeni? Na je, matusi hayo yana lolote la kuwaongezea wananchi wa Kigoma Mjini?

Hata kama Serukamba atakuwa ameomba radhi, nataka nimjulishe mtani wangu huyo kwamba Wahaya wanasema kwamba "Ekiruga kanwa tikishubamu." Kwa maana kwamba neno likishatoka mdomoni halirudi. Hivyo wananchi wa Kigoma Mjini inawabidi wawe makini katika kumpata mwakilishi wao kusudi wasije wakaonekana wote ni watu wa matusi, tena matusi ya nguoni. La sivyo wataendelea kulivunjia heshima Bunge, nchi yao, wao wenyewe pamoja na Watanzania kwa ujumla.

Jambo jingine ni kauli za maudhi za naibu spika. Hapa namnukuu Mheshimiwa Job Ndugai. "Lissu sijui ni huo ushamba wa ubunge, hii ni mara ya 20 unataka kuongea wewe tu. Wewe ni kiongozi lakini umekuwa kinara wa vurugu."

Bila kusita naiona hiyo kama kauli ya maudhi iliyotolewa na mtu anayepaswa kuhakikisha kanuni za Bunge zinafuatwa na kutekelezwa. Ushamba wa ubunge maana yake nini? Ina maana yeye Ndugai ubunge alizaliwa nao?

Je, kuchacharika kwa Lissu ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda kwa mujibu wa kanuni za Bunge wakati wa uendeshwaji wa vikao ndizo vurugu anazozisema Ndugai? Kumbe Ndugai anawafurahia wabunge wanaonogewa na kiyoyozi na kuuchapa usingizi kwenye masofa yanayozunguka akiwaona kuwa ndio wasiokuwa wasumbufu wala kuwa na vurugu!


Je, kwa mwonekano huo anaoutaka Ndugai, wa kuwataka wabunge wauchape usingizi ili wasionekane wenye vurugu, Ndugai anawatendea haki Watanzania? Na je, Kanuni za Bunge zinamwekea mbunge kikomo cha kutaka mwongozo? Kama sivyo iweje Ndugai amsakame Lissu kiasi cha kumuita mshamba wa ubunge wakati Lissu akitimiza wajibu wake?


Inabidi wananchi tuelewe kwa hali yetu ilivyo kwa sasa hatuwatumi wabunge kwenda Dodoma kufanya mandali (pikniki), kula, kunywa na kuchapa usingizi. Tunawatuma wakachacharike kama anavyofanya Lissu na wenzake wanaodaiwa wanafanya vurugu. Ieleweke kwamba neno vurugu, kama linavyotumiwa na Ndugai, ni pilika pilika dhidi ya starehe.


Mtu yeyote aliye kwenye starehe zake ukimwambia tufanye hili na lile ataona unamwaribia uhondo wake, kwa kumvurugia starehe zake. Kwa maana nyingine unamfanyia vurugu.


Kama Ndugai hakubaliani na tafsiri yangu hiyo basi atueleze kwa ufasaha maana ya vurugu anazozisema zinazofanywa na Mheshimiwa Tundu Lissu bungeni mpaka kufikia kumpa adhabu iliyo nje ya kanuni za Bunge.

Nimalizie kwa kusema kwamba taswira ya Bunge letu imechafuliwa na ibilisi anayeonekana kufugwa kwa malengo maalumu na spika na naibu spika. Kwa maneno mafupi ni kwamba spika na naibu wake wametuharibia Bunge letu.
 
Back
Top Bottom