Bei ya mahindi katika masoko mbalimbali katika Mkoa wa Songwe imeporomoka katika kipindi cha mwezi mmoja ikilinganisha na bei zilizokuwepo mwezi Juni na Julai mwaka huu.
Irine Nahaonga, Mkulima na Mkazi wa Kijiji cha Sumbaluwela, Kata ya Ihanda, wilayani Mbozi, ameiambia Mwananchi Digital kuwa amestaajabishwa nan a kushuka kwa bei ya mahindi kutoka Sh85000 hadi 66,000 kwa gunia la kilo 100.
Aidha katika kipindi cha mwezi Juni na Julai mwaka huu, mahindi yalikuwa yakiuzwa kwa bei ya kati ya Sh80, 000 na Sh84, 000 kwa gunia lenye ujazo huo.
Katika soko la mazao Mlowo, wilayani Mbozi, Tumaini Enson, amesema kushuka kwa bei hizo mwezi Agosti, kunatokana na wanunuzi kutofika, jambo lililosababisha kuwa na mahindi mengi na bei kushuka.
"Kuanzia juzi walau bei imeanza kuongezeka kidogo kutoka Sh66, 000 hadi Sh72, 000 siku ya leo, hivyo kuna nafuu kidogo,β amesema Tumaini.
Meneja wa Soko la Kimataifa la Mazao Katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Edward Silwimba, amesema sokoni kwake bei ya mahindi kwa gunia ni kati ya Sh72, 000 na Sh78, 000.
Silwimba amekiri kuwa, kukosekana kwa wanunuzi kumechangia hali hiyo japo ana matumaini kwani sasa wanunuzi wameanza kufika sokoni hapo.
Kwa upande wake Johnson Kayange, Mkazi wa Ihanda, analaumu kuyumba kwa bei ya mahindi akisema: β...kipato kupunguza sana, tukienda kuuza, tunapata fedha kidogo ukilinganisha na siku za nyuma bei zilipokuwa juu.β
Hata hivyo bado anakiri kuwa, japo bei ni ndogo, haziwezi kulinganishwa bei za kuanzia 2019 kurudi nyuma, kwani kipindi hicho, gunia la kilo 100, liliuzwa kati ya Sh36, 000 na Sh42, 000.
Kutoka Kijiji cha Itaka wilayani Mbozi, mkazi wa Kijiji hicho Aida Mwasenga, amesema wanunuzi kutoka maeneo ya mjini wanafika kijijini hapo na kununua mahindi kwa bei ndogo ya kati ya Sh54000 na 60000 kwa gunia.
Ili kupata kauli ya Serikali, Mwananchi Digital imewatafuta viongozi wakuu wa Wizara ya Kilimo, ambao ni pamoja na Waziri Hussein Bashe, naibu wake Davidi Silinde, na Katibu Mkuu Gerald Mweli, hata hivyo simu zao ziliita bila majibu.