Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini(Latra), imefungua milango Kwa wasafirishaji kuanza kupeleka maombi ili yachakatwe kwa ajili ya maandalizi na kujipanga kuanza kutoa huduma kwa saa 24.
Milango hiyo imefunguliwa zikiwa zimepita siku chache tangu Serikali kutangaza kuondoa rasmi katazo la mabasi kusafiri usiku.
Juni 28, mwaka mwaka huu wakati akitoa hoja ya kuahirisha vikao vya Bunge, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza rasmi kuondoa zuio la safari za usiku lililokuwepo tangu Mwaka 1992.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri wa Barabarani kutoka Mamlaka hiyo, Johansen Kahatano imeeleza kuwa, baada ya kupokea maombi hayo hatua itakayofuata ni kuyachakata, ili kujua ukubwa wa maeneo yenye uhitaji na kupanga ratiba za kuanza huduma hiyo.
"Tunatarajia huduma hii haitachelewa sana kuanza kwa sababu uhitaji wa kutoa huduma hiyo saa 24 upo na Wizara zote mbili za Mambo ya Ndani na Uchukuzi kukaa pamoja," amesema Kahatano.
Amebainisha kuwa kama ambavyo walianza huduma ya usafirishaji saa 11 alfajiri na baadae saa tisa, ndivyo watakavyochakata na kupanga ratiba hiyo ya saa 24, na njia gani zianze kutokana na ukubwa wa uhitaji.