Mwananchi Source: 01/02/2009BAADA ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushinda uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbeya Vijijini, Katibu Mkuu wake, Yusuph Makamba amesema muungano wa vyama vya upinzani hauna mwelekeo sawa paka wanne waliofungwa kamba mikiani.
Makamba alitoa jana katika uwanja wa Pasua, mjini Moshi wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 32 ya chama hicho ambayo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Aman Abeid Karume.
Makamba ambaye hupenda siasa za vijembe, kama kawaida yake alisema kwa ukiwafunga paka wanne pamoja mikiani na kisha kuwawekea panya mbele yao, wote watakatika mikia kwa kila mmoja kukimbilia panya huyo.
Alisema hayo akimaanisha kuwa, muungano wa upinzani sasa umevunjika kutokana na kila chama kutaka maslahi katika uchaguzi huo.
Hata hivyo, aliwaagiza wanachama na wakereketwa wa CCM kutokubali chama chao kuhusishwa na ufisadi na kutangaza rasmi kwamba, kuanzia sasa watakula sahani moja na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
"Hoja yao kubwa sasa (Chadema), ni ufisadi, wanasema CCM mafisadi na kila tukipita na nguo zetu za kijani wanasema mafisadi haooo Tuwaombe wanachama na wakereketwa wetu wakatae kuitwa mafisadi," alisema Makamba huku akishangiliwa.
Makamba alirejea maagizo ya Karume alipozungumza na wanachama wa Umoja wa Vijana wa CCM (UV-CCM) mjini Dodoma, ambako aliwataka wasihofu Operesheni Sangara iliyotangazwa na Chadema kwani wako imara kujibu mapigo.
Makamba alitumia mifano ya dini ili kuhakikisha anafikisha ujumbe wake pale alipohoji iwapo kama yeye atazini lawama zitamwendea Sheikh au Mungu?
"Hivi Yusuph Makamba akizini lawama zitapelekewa Mungu au Sheikh? Au akizini mkatoliki lawama zitaenda kwa Kadinali Pengo au Mlutheri lawama ni kwa Askofu Malasusa? Lawama atabeba aliyezini, hivyo na ufisadi usihusishwe na chama," alisisitiza na kuongeza akitoa mfano:
"Kama Mbowe anatuhumiwa kwa ufisadi, Sisi hatusemi Chadema ni mafisadi bali tutasema Mbowe na kama ni Mrema, atatuhumiwa kukwapua mabilioni akanunua nyumba, basi fisadi si TLP bali ni Mrema".
Kwa upande wake Rais Karume, alisema licha ya kuwepo kwa majimbo na kata zenye wabunge au madiwani wa upinzani, ni lazima viongozi hao wafahamu kuwa Tanzania inaongozwa na serikali zote mbili ya Muungano na ile ya Mapinduzi Zanzibar(SMZ), ambazo zitahudumia majimbo yote bila kuchoka.
Alisema upinzani wa Tanzania bado haujakomaa na ni wa kupinga kila jambo jema linalofanywa na serikali ya CCM na kwamba, chama hicho hakitakoseshwa usingizi na kauli zisizo za kweli za viongozi wa vyama vya upinzani nchini.
Katika sherehe hizo zilizohudhuriwa pia na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa, Katibu Mwenezi, John Chiligati, Rais Karume alipokea wanachama wapya 1,321 waliojiunga na chama hicho na jumuiya zake.
Katika tamko lake lililosomwa na Katibu wa mkoa, Mauldine Kastico, CCM mkoa Kilimanjaro ilisema imejipanga kikamilifu na kiko makini kushinda chaguzi za serikali za mitaa mwishoni mwa mwaka huu na uchaguzi mkuu wa 2010 kwa kishindo.