Waomba hukumu ya Mahakama ya
Rufaa ipitiwe upya
Makada watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliopinga ubunge wa Mbunge
wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema na kufanikiwa kumvua ubunge
kabla ya Mahakama ya Rufaa kumrejesha wadhifa wake, wamewasilisha maombi
ya kutaka hukumu ya mahakama hiyo ipitiwe upya.
Kwa mujibu wa
taarifa za kimahakama, makada hao waliwasilisha maombi yao Februari 13,
mwaka huu chini ya hati ya dharura wakitaka yasikilizwe
haraka.
Desemba 21, mwaka
jana Mahakama ya Rufaa ilimrejesha tena Lema bungeni baada ya kukubali
rufaa yake dhidi ya hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha iliyomvua
ubunge wake.
Makada hao
waliolalamikia ushindi wa Lema wakiwa ni wapigakura wa Jimbo la Arusha
Mjini, wanadai kuwa na sababu sita za kutaka mahakama hiyo ipitie uamuzi
wake kwa madai kuwa kuna maeneo ambayo hayakuamuliwa vizuri. Jana
NIPASHE ilizungumza na Wakili wa Lema, Method Kimomogoro, ambaye
alithibitisha kuwa na taarifa za maombi hayo na kuahidi kutoa ufafanuzi
baadaye.
Naye wakili wa
wanachama wa CCM, Alute Mughway, jana alithibitisha kuwa wateja wake
wamewasilisha maombi hayo Mahakama ya
Rufaa.
Wanachama hao wa
CCM, ambao ni Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel, walifungua
kesi dhidi ya Lema katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, kupinga ushindi
wake alioupata katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2010.
Walikuwa wakidai
kuwa katika kampeni zake, Lema alikuwa akitumia lugha za matusi, kejeli
na ubaguzi wa kijinsia dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk. Batilda
Buriani.
Kufuatia kesi
hiyo, Lema alivuliwa ubunge na mahakama hiyo, Aprili 5, mwaka huu,
katika hukumu iliyotolewa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga,
Gabriel Rwakibarila, aliyesikiliza kesi hiyo. Jaji Rwakibarila
aliisikiliza kesi hiyo baada ya Jaji Aloyce Mujulizi aliyekuwa
amepangiwa kuisikiliza kesi hiyo kujitoa kufuatia ombi la Lema kuwa
hakuwa na imani naye.
Hata hivyo,
baadaye mwishoni mwa mwaka jana, Lema kupitia mawakili wake, Kimomogoro
na Tundu Lissu, alikata rufaa kupinga hukumu hiyo iliyomvua ubunge
wake.
Hukumu ya
kumrejeshea ubunge Lema ilitolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama
ya Rufaa, wakiongozwa na Nathalia Kimaro. Wengine ni Salum Massati na
Bernard Luanda.