Majibu ya makala ya Lula wa Ndali Mwnzela ya "Kila la kheri Zanzibar, bye bye Muungano" | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Majibu ya makala ya Lula wa Ndali Mwnzela ya "Kila la kheri Zanzibar, bye bye Muungano"

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mzenji73, Jul 28, 2012.

 1. M

  Mzenji73 JF-Expert Member

  #1
  Jul 28, 2012
  Joined: Jan 10, 2009
  Messages: 341
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
  Kwa kawaida Lula wa Ndali Mwananzela ni mwandishi mahiri sana na ingawa yeye ni Mtanganyika, makala zake nyingi zinazozungumzia Zanzibar huwa zinaelezea ukweli wa taarikh kwa ujuzi na mantiki na aghlabu bila kupempendelea yeyote hata kuwashinda waandishi wengi wa Kizanzibari. Kwa hili namshukuru na nampa pongezi kubwa sana. Lakini katika makala ifuatayo aliyoichapisha tarehe 18 Julai, 2012 aliyoiita "Kila la kheri Zanzibar, bye bye Muungano!" nastaajabu kuwa ingawa katika vifungu vine vya awali na pia vya mwisho ameelezea mambo kikweli lakini ukisoma vifungu vya kati unagundua kuwa mambo yote yaliyompa sifa njema ya utafiti madhbuti, uandishi na mteremko wa kimantiki na bila mapendeleo kaupoteza katika hoja zake zisizokuwa za haqi. Tuanze na kifungu cha tano kinachosema yafuatayo:

  "Hata hivyo, mazingira makubwa zaidi ya kuondolewa kwa usultani uliodumu kwa karne karibu tatu yalikuwa ni tishio kubwa kwa watawala wapya wa Zanzibar.

  Ukweli ni kuwa, kwanza, kinyume na propaganda zilivyo, kuanzia mwaka wa 1890 Zanzibar ilipoingizwa katika ukoloni wa Kiingereza, Sultani alibakia kuwa wa jina tu maana utawala ulikuwa chini ya Mtawala Mwingereza na "Sultani" aligeuzwa kuwa mfanya kazi wa Serikali ya Kiingereza wa kulipwa mshahara kama alivokuwa Kabaka wa Buganda, Mareale wa Wachaga na wafalme wa Kiafrika wengineo. Kweli kuna Malkia Uingereza, lakini mtu yoyote anayetuelezea kuwa Malkia ndiye anayeitawala Uingereza na ndiye mwenye nguvu za kuendesha serikali au kuandika sharia za Uingereza na kuweza kuwafunga na kuwafungua raia Uingereza, mtu huyo kweli huwa haelewi maana ya ‘Constitutional Monarchy" yani "Ufalme wa Katiba" au "Ufalme Bandia" kuwa sio wenye nguvu za kiutawala. Baada ya uhuru Serikali ya Zanzibar ilikuwa chini ya mikono ya Waziri Mkuu Muhammad Shamte na vyama tawala vya ZPPP na ZNP kama ilivyo serikali ya Uingereza chini ya chama tawala na si ndani ya mikono ya Malkia.

  Mwenye-enzi Mungu Anatuambia katika Qur-an Tukufu, kwa tafsiri, kuwa "Enyi mlioamini! Kuweni wenye kusimamisha uadilifu, mtowao ushahidi kwa ajili ya Mwenye-enzi Mungu, ijapokuwa ni juu ya nafsi zenu, au wazazi wawili na jamaa zenu. Akiwa tajiri au masikini Mwenye-enzi Mungu anawastahikia zaidi. Basi msifuate matamanio, mkaacha kufanya uadilifu. Na mkiupotoa au mkajitenga nao basi Mwenye-enzi Mungu anajua vyema mnayoyatenda. Q:4:135"

  Kuwapa wasomaji wake taswira ya kuwa Sultani ndiye aliyekuwa mtawala mwenye nguvu za kiserikali mikononi mwake ni kuwapa fikra isiyokuwa sahihi. Tunaweza kuelewa iwapo maneno hayo yamesemwa na mwanasiasa aliyekuwa hakusoma au mwenye lengo lake maalumu lisilokhusiana na kusema ya kweli, lakini kwa mtaalamu kama Lula wa Ndali Mwananzela ukweli huu inapasa aujue ila ikiwa naye kakusidia jingine. Jambo hili limeifanya makala yake iwe ina upungufu wa kimsingi na hivyo, kuidhoofisha sana. Lakini mwandishi hakusita hapo katika kifungu hicho, ameendelea kuandika yafuatayo:

  "Hakuna mtu aliyetarajia kuwa usultani ungeweza kuondolewa katika saa chache na watu wenye silaha duni. Tishio la jaribio la kumrudisha sultani kwa wakati ule lilikuwa dhahiri. Kwa watu wanaokumbuka historia Sultan Jamsheed aliomba msaada wa askari kutoka Tanganyika kuzima mapinduzi kitu ambacho Nyerere hakukubali."

  Ulioondolewa kwa saa chache si "Usultani" bali ni serikali ya Shamte na vyama vya ZPPP na ZNP. Angeliondoshwa Sultani na ikabakishwa serikali ya Shamte ndio wanamavamizi wangeliridhika? Lengo khasa lilikuwa ni kuiondosha serikali ya Shamte na kuwaweka Zanzibar watawala wepya ambao watamridhia yule alioteremsha majeshi yake Zanzibar na kuivamia. Kuuficha ukweli huu hakika ni kuwapa wasomaji taswira isiyokuwa kamili na ya uhakika, na jambo hili haliwezi kuufuta ukweli.

  La muhimu pia ni kuwa kuna ukweli muhimu zaidi ambao mwandishi wa makala tunayoyazungumzia ameugubika nao ni kuwa waliohujumu maboma mawili ya polisi – la Ziwani na la Mtoni – si wengine bali ni majeshi kutoka Tanganyika na kwingineko bara pamoja na ndugu zao waliokuwa wanapolisi Zanzibar pamoja na wenzao wengine waliotoka katika mashamba ya mikonge Tanga ambao kazi kubwa waliopewa ni kufyeka roho nyingi za Wazanzibari waliokuwa wanachama wa vyama vya ZPPP na ZNP kwa mapanga na kuzichanja kwa mashoka; na roho za Wazanzibari wengi wa kawaida na wasiokuwa Wazanzibari zilifyekwa wakati wa mavamizi. (Picha za maafa wakiokutishwa raia wa kawaida Zanzibar mnamo January 1964 zimejaa mitandaoni). Wazanzibari wengi sana, tena sana, hawakushiriki katika mavamizi. Iwapo Wazanzibari kutoka Makunduchi mpaka Kizimkazi na Walioko Pemba yote hawakuwa na khabari wala hawakushirikishwa katika hayo mavamizi yaliyofanywa na Watanganyika kwa amri za Julius Kambarage Nyerere, tutayaitaje matokea hayo kuwa ni "mapinduzi"? Mapinduzi hupindua watu wa nchi wenyewe; jambo hili likifanywa na Majeshi kutoka nchi nyingine, hayo hayawezi kuitwa "mapinduzi" bali ni "mavamizi" ya kuivamia nchi isiyokuwa yao.

  Wavamizi hao kutoka bara tuliwaona asubuhi ya usiku wa mavamizi wakipita mitaana mwetu na hakuna Mzanzibari aliyekuwa na shaka yoyote kuwa wavamizi hao walikuwa ni wageni kutoka bara na kwa lafdhi zao walipokuwa wakipita mitaani mwetu wakinadi kwa maneno: "Arabu uwa, Muhindi uwa, Muzungu siguse" ilizidi hakika yetu kuwa hao si Wazanzibari bali ni Wabara.

  Wala si Sultan Jamshid aliyeomba msaada wa askari kutoka kwa Waingereza, Kenya na Tanganyika. Waliofanya hayo ni Shamte na Ali Muhsin aliyekuwa Waziri wake wa Mambo ya Nje. Nyerere hakukubali kwa sababu ni yeye aliyeteremsha majeshi yake kuja kuvamia maboma ya polisi Zanzibar na kuwauwa Wazanzibari kiholela. Inasikitisha sana kuona kuwa katika wakati huo Shamte na serikali yake hawakujua kuwa ni Nyerere ambaye ameteremsha Zanzibar majeshi yake. Ukweli huu tunaujua kwa hakika zaidi leo baada ya baadhi ya wauwaji walioshiriki katika mavamizi na kuuwa Wazanzibari kwa wingi kuelezea visa vyao vya kuwakutisha Wazanzibari maafa. Kwahivyo kuendelea kutuambia kuwa Nyerere alikuwa na nia safi juu ya Zanzibar, jambo hili linamfanya mwandishi-msomi yoyote kujiweka mahala pabaya sana. Sote tunaelewa nini Nyerere mwenyewe amesema kuelezea kuchukizwa kwake kwa Mungu kuiumba na kuiweka Zanzibar karibu na Tanganyika aliposema kuwa angelikuwa na uwezo angeliiburura Zanzibar na kuitokomeza mbali katika Bahari ya Hindi. Kufikiria kuwa Nyerere katika maisha yake yote alikuwa na nia njema na Zanzibar ni kujidanganya pakubwa sana kwa ndoto za mchana.

  Sheikh Muhammad Shamte aliitaka serikali ya Uingereza iipe Zanzibar himaya baada ya uhuru kama zilivyopewa Tanganyika, Kenye na Uganda juu ya kuwa nchi hizi zilikuwa na majeshi yake yenyewe. Serikali ya Uingereza ikakataa kuipa Zanzibar himaya ya zaidi ya mwezi mmoja ingawa Zanzibar ndiyo iliyokuwa inahitajia himaya zaidi ya hizo nchi nilizozitaja kwa kuwa Zanzibar hata haikuwa na jeshi la kijeshi. Baada ya mwezi na siku mbili – yaani baada tu ya kumalizika mkataba wa mwezi na Dola ya Uingereza – Zanzibar ikavamiwa kijeshi. Nakuachilieni wenyewe mjaze mapengo ya kujibu "kwanini Mgereza akazipa nchi jirani himaya ya miaka na kuikatalia Zanzibar kuiipa himaya kama hiyo"?

  Mwandishi ameendelea kusema:
  "Sultani hakupata msaada wowote kutoka bara na msaada wa kutoka kwa binamu zake wa Oman usingeweza kuelekea visiwani hapo bila kusababisha watu wa bara kuingilia kati na hata mataifa ya Magharibi yaliyokuwa na maslahi visiwani humo yasingekaa pembeni."

  Kweli "Sultani hakupata msaada wowote kutoka bara" Atapataje msaada kutoka kwa katili mweyewe aliyepeleka majeshi yake kuivamia Zanzibar na kufyeka roho za Wazanzibari? La kusikitisha pia ni kuwa Shamte na Mawaziri wake hawakumfahamu Nyerere mpaka pale alipokuja kuwafunga kwa miaka mingi bila ya kufikishwa mahkamani. Na hata wakati huo pia hawakuelewa ni nani khasa aliyeyapanga na kutekeleza hayo mavamizi.

  Mwandishi anaendelea kuandika haya:
  "Ili kuiokoa Zanzibar Tanganyika ilijitoa muhanga kwa kila namna hadi kukubali kufa ili Zanzibar iwepo. Narudia sentensi hii, ili Wazanzibar wajue kuwa Tanganyika haijawahi kuwa adui wa Zanzibar bali imekuwa ni zaidi ya rafiki; imekuwa ni ndugu. Tanganyika haikuwa ndugu wa maneno; ilikuwa ni ndugu aliyekuwa tayari kufa ili mdogo wake aishi. Tanganyika imekufa ili Zanzibar iwepo."

  Tanganyika haijawahi hata siku moja kujitolea muhanga kwa ajili ya Zanzibar. Nikisema Tanganyika sikusudii watu wa kawaida, bali namkusudia Kambarage na serikali yake na za wafuasi wake waliokuja baadaye. Si kweli hata chembe kuwa serikali ya Tanganyika iliwahi kuwa na udugu wa dhati na Zanzibar. Ndugu hapangi na kutekeleza mauwaji kiholela kwa mtindo wa Kiruwanda na Kiserbia kama majeshi ya Nyerere walivyowafanyia raia wa Zanzibar kwa kuwateremshia maafa makubwa sana na vilio vya milele. Ni kweli kabisa kuwa Seriakli ya Tanganyika haijawahi kuwa na udugu wala urafiki na Zanzibar wala na Wazanzibari. Nyerere na makatili wenziwe wametenda waliyoyatenda kwa lengo lao la kuifanya Zanzibar koloni lao, na hili si lengo la kidugu wala la kirafiki. Ikiwa udugu na urafiki na Tanganyika wa Rais Nyerere kumesabibisha kuwauwa Wazanzibari kama nguruwe mwitu, sijui Zanzibar ingelikuwa adui wa Nyerere Wazanzibari wangelifanywaje zaidi na wauwaji kutoka Bara!

  Anaendelea kuandika:
  "Leo Zanzibar imekomaa na kunusurika na tishio kubwa ndani yake Tanganyika inaambiwa ni mkoloni. Tatizo ni kuwa Tanganyika kwa kweli haikufa kabisa; ilikubali kulazwa nusu kaputi ili kuokoa uhai wa Zanzibar. Sasa Tanganyika inaamka!"

  Katika historia ya kikatili na ya kikoloni sijui mwandishi anataka ifikiriwe vipi na Wazanzibari! Pengine Wazanzibari, baada ya kukutishwa kila aina ya maafa, kuiita Tanganyika "koloni" tu haitoshi. Inahitajia pia itajwe kwa mengineyo maovu iliyoyatendea Wazanzibari. Wala Tanganyika haijawahi kufa. Kilichokufa hakiwezi kufufuka. Tanganyika imejibadilisha jina tu na kujifanya kuwa Tanzania, ili kujinyakulia nguvu zote muhimu za Tanganyika na za Zanzibar – Nguvu za kuhodhi fedha, kodi, majeshi, mahkama, mambo ya nje na kadhalika na kadhalika. Wala Tanganyika haijawahi kulala ifike leo kuamka! Zanzibar ndiyo iliyokuwa imelazwa na baada ya kuamshwa usingizini kwa kuelemewa na jinamizi la Tanganyika na kupiga makelele ya kuzibwa pumzi ndipo leo baadhi ya waandishi wa Tanganyika wanapobirua maneno na kuyasema yote hayo yasiyokuwa sahihi na yasiyoingia akilini. Waandishi wengi wa Kitanganyika wanaweza kuendelea kubirua maneno wapendavyo, lakini ukweli unabakia palepale. Katka Qur'ani Tukufu Mola Mkwasi Anasema kwa tafsiri:

  "Wala msichanganye kweli na uwongo na mkaificha kweli nanyi mnajua." 2:42

  "Enyi Watu wa Kitabu! Mbona kweli mnaivisha uwongo, na kweli mnaificha na hali mnajua?" 3:71
  Tanganyika imekuwa mkoloni kuliko waliotangulia. Lakini ni dasturi ya mkoloni siku zote kuona ni yeye anayezitendea wema nchi alizozitawala. soma makala hii ambayo inatoa mfano mzuri ‘A lesson in humility for the smug West'; A lesson in humility for the smug West.

  Mwandishi anaendelea kuandika na yafuatayo:
  "Tanganyika ilikubali kuua uhuru wake ili Zanzibar iwe huru nayo. Kujitoa huku muhanga kwa Tanganyika kwa wanaofahamu historia hakukuwa kwa maneno matupu tu. Wengi – wanaofahamu historia- wanakumbuka kuwa Nyerere alikuwa tayari hata kuahirisha uhuru wa Tanganyika ili lipatikane shirikisho la Afrika Mashariki chini ya Mzee Jomo Kenyatta. Na kujitoa huku muhanga kuliendelea katika harakati za ukombozi kusini mwa Bara la Afrika. Lakini hakuna mahali ambapo Tanganyika ilijitoa mhanga zaidi kama ilipokuja suala la Zanzibar. Ili kuiokoa Zanzibar, Tanganyika iliacha Zanzibar ibakie na serikali yake, uongozi wake, chama chake na hata mwelekeo wake."

  Kuakhirisha uhuru wa Tanganyika kuna uhusiano gani na kuja kufanya muungano baadaye? Haya ya Nyerere kutaka kuakhirisha uhuru wa Tanganyika mpaka Zanzibar na Kenya zipate uhuru ili lipatikane shirikisho la Afrika Mashariki ni hadithi za kipaukwa pakawa. Kwanini Tanganyika haikuungana na Kenya baada ya uhuru? Pili, Tanganyika ingeliwezaje "kujitoa huku muhanga kuliendelea katika harakati za ukombozi kusini mwa Bara la Afrika" wakati ingelikuwa Tanganyika bado imetawaliwa na Mwingereza? Tatu, kusema kuwa "Lakini hakuna mahali ambapo Tanganyika ilijitoa mhanga zaidi kama ilipokuja suala la Zanzibar. Ili kuiokoa Zanzibar, Tanganyika iliacha Zanzibar ibakie na serikali yake, uongozi wake, chama chake na hata mwelekeo wake" si maneno ya kisanii tu, bali ni maneno ya kikoloni kabisa. Zanzibar ilikuwa na yote hayo ya nchi huru kabisa mpaka iponyang'anywa uhuru wake na Tanganyika. Kama kweli Nyerere na wafuasi wake wangelitaka Zanzibar iwe nchi huru, kwanza isingeliyaingilia mambo yake ya ndani kwa kuteremsha wauwaji kuja kutoa roho za raia wa Zanzibar kama mijusi. Na baada ya hapo isingelifanya usanii wa kutaka kuimeza. Hoja sizokuwa na msingi kama hizi kurejelewa na mtu msomi ni jambo la kusikitisha sana.

  Anaendelea mwandishi:
  "Kinyume na inavyolalamikiwa na wengi jitihada za kuirejesha Zanzibar katika uhai wake zilianza miaka karibu 30 nyuma. Zanzibar ikapata baraza lake la kutunga sheria, Zanzibar ikapata katiba yake, Zanzibar ikapata wimbo wake wa taifa, na bendera yake na Rais wake mtendaji na hivi karibuni Zanzibar ikajitaja kuwa ni nchi kamili."

  Haya aliyoyaandika mwandishi niliyoyanakili hapa juu yanasikitisha kwelikweli. Narejelea tena kusema: Kwani Zanzibar haikuwa na mambo yote hayo baada ya uhuru? Aliyejaribu kuyaondosha na kuyameza ni nani hata ibidi Zanzibar kuyadai tena upya? Mwandishi hata haoni kuwa kwa maneno yake mwenyewe anakiri kuwa Zanzibar ilitiwa katika ukoloni wa Nyerere na wafuasi wake ndipo ilipokuwa haina budi ya kuyadai tena ili Zanzibar itokane na ukoloni huu!

  Mwandishi anaendelea na hoja ifuatayo:
  "Wakati huu wote Tanganyika imeendelea kuilea Zanzibar ili ipate uhai wake; tulidhania – kwa makosa makubwa – kuwa Zanzibar itatambua kuwa ina undugu na ukaribu na Tanganyika kiasi cha kutaka hatimaye kuwa nchi moja kamili. Walipopata vyote Zanzibar wanasema wanataka kutoka. Sasa ni jukumu la Tanganyika kuwasaidia kutoka."

  Haya ni makubwa sana: Hivyo Zanzibar ilikuwa ni wmtoto mchanga asiyekuwa na akili wala uwezo wowote hata ikabidi ilelewe na Nyerere na wafuasi wake? Kama huku si kuwadharau na kuwatukana Wazanzibari kwa kibri, sijui ni kitu gani hichi alichotuelezea mwandishi huyu!
  Bado anaendelea na haya pia:

  "Tumechoka kunyonywa!"

  "Zanzibar imekuwa kama kupe mgongoni mwa ng'ombe. Haiishi kulalamika kwa nini ng'ombe hali vizuri, kwa nini ng'ombe hatambui uwepo wa kupe, kwa nini ng'ombe damu yake si tamu sana."

  "Imekuwa ni kupe asiyetosheka na sasa anaamini kuwa kwa kujitoa mgongoni mwa ng'ombe anamkomoa ng'ombe. Ati anadai uhuru wake, ili awe kupe kamili. Tatizo ni kuwa hakuna namna yoyote kupe ataweza kukaa bila kunyonya ng'ombe au mnyama mwingine. Zanzibar haiwezi kukaa bila kutegemea nchi nyingine. Ama itategemea bara au itajaribu kutegemea Uarabuni au nchi nyingine."

  Kama mwandishi yu radhi kuilinganisha Tanganyika na "ng'ombe" hilo litakuwa ni lake na la Watanganyika wenziwe. Kuilinganisha Zanzibar na "kupe" hapo ndipo penye kuwafanya Wazanzibari wazidi kuwachukia wafuasi wa siasa za Nyerere. Ukweli ni kuwa baada ya "muungano" na baada ya Nyerere kuifilisi Tanganyika kwa siasa zake mbovu ni Tanganyika iliyoifilisi Zanzibar mamilioni ya madola iliyokuwa nazo katika benki za nje. Ni Tanganyika inayokuja kila leo kuchukua pesa za ushuru kutoka Zanzibar na kuzipeleka Tanganyika na Wazanzibari wanabakia kutumbuliana macho juu ya unyang'anyi wa dhahiri, na kuna na mengi mengineyo ya unyanganyi ambayo tutayazungumzia siku nyingine. Sijui hii propaganda ya Zanzibar kuwa inainyonya nchi fakiri ya Tanganyika imeanziaje! Tanganyika yenyewe haiwezi kujiendeshea mambo yake bila ya ombaomba kutoka nje. Ikiwa Zanzibar ni kupe kwanini ing'ang'aniwe na wafuasi wa siasa za Nyerere ibaki chini ya hukumu ya Tanganyika?

  Mwandishi anaendelea:
  "Haina uwezo wa kusimama yenyewe hata watu wake watamanie vipi. Tumaini pekee kuwa ikipata mafuta itageuka pepo ni ndoto za Alinacha. Hata yakipatikana mafuta kesho inachukua miaka mingi kuweza kubadilisha maisha ya wananchi. Ila yakipatikana mafuta Zanzibar kizazi cha watawala kitanufaika sana hilo halina shaka. Ndio kanuni ya "laana nyeusi". Nani anatawala Zanzibar?"

  Unaziona fikira za mtu aliyekuwa hana imani aliyejazwa kasumba za kikoloni! Zanzibar isiweze "kusimama yenyewe hata watu wake watamanie vipi" Ni maneno ya kikafiri. Wazanzibari wengi wanaamini kabisakabisa kuwa riziki inatoka kwa Mwenye-enzi Mungu Karimu Rahimu. Na ni Mwenye-enzi Mungu Mwenyewe aliyewaambia katika vitabu vyake kuwa kila alichokiumba anakipa riziki. Ni ukafiri kufikiria kuwa riziki za Wazanzibari zinatoka kwa Watanganyika. Kwa hakika ni utawala mbaya wa bara ndio unawaofujia Wazanzibari njia zaidi za kuiendeleza mbele nchi yao si kinyume chake.

  Kuna visiwa vingi tu duniani ambavyo vingine ni vidogo sana, vina uhuru wake na viti vyao katika Umoja wa Mataifa na vinajiendeleza wenyewe bila ya msaada kutoka katika nchi fakiri kama Tanganyika ambayo yo yenyewe haiwezi kuwalisha watu wake bila ya misaada kutoka nje kwa ajili ya siasa mbovu, rushwa, unyang'anyi na utapeli uliozagaa. Kama kweli wafuasi wa Kambarage wanawaona Wazanzibari ni ndugu zao na wanaitakia kheri Zanzibar, basi waiache iwe huru leo kabla yakesho. Zanzibar toka ilovoumbwa haikuwa chini ya rehema ya Tanganyika; jee, kimezidi kipi ili isiweze kujitegemea? Wanaojenga nchi ni watu sio viliyo chini au juu ya ardhi. Soma makala iliyoandikwa kwa Kiingereza niliyokutilia kiungo inayoanza kwa maneno: "The idea that great natural wealth might in fact contribute to keeping a country poor has captured the public imagination precisely because it helps explain a phenomenon that is one of the great paradoxes of our time: Countries blessed with fabulous riches are often also cursed, perhaps inevitably, with grinding poverty" utazidi kutatukiwa. WPR Article | World Citizen: The Norway Model for Exorcising the Resource Curse.

  Mifano ya nchi kama hizo iko mingi duniani. Mfano mmoja unatosha kudhihirisha hoja hii: "Taiwan is a barren rock in a typhoon-laden sea with no natural resources to live off of - it even has to import sand and gravel from China for construction - yet it has the fourth-largest financial reserves in the world. Because rather than digging in the ground and mining whatever comes up, Taiwan has mined its 23 million people, their talent, energy and intelligence - men and women" Countries without rich natural resources tend to educate their children better, OECD finds. Does this explain Taiwan's success? « InvestmentWatch

  Kama kweli wafuasi wa Kambarage wanaitakia kheri na udugu mwema na Zanzibar, basi waiache Zanzibar iwe huru leo kabla yakesho. Wala si kujidanganya nafsi zao na kujaribu kuwadanganya walimwengu kuwa kwa ajili ya kuionea huruma Zanzibar ndipo wakawa hawana budi ila kuitia katika ukoloni wao! Udugu mwema si lazima kufungana kamba wala hauji kwa kupigiana mifano ya ugombe na ukupe. Kama Wafuasi wa Nyerere wanajiona kweli ni ndugu zao Wazanzibari, basi wataudumisha udugu huo pakiwepo pasikuwepo "muungano" bila ya kuwatisha Wazanzibari kuwa wakiuvunja "muungano" watawafanyia makuruhi haya na yale. Kutisha huko si alama ya udugu hata chembe. Ni kuonesha tu kuwa nia zao tokea mwanzo zilikuwa mbaya.

  Mwandishi anaongeza:
  "Sasa sisi wa bara nao tumekuwa wavumilivu mno na uvumilivu wa kutukanwa, kukejeliwa na kudharauliwa na ‘kanchi' kama Zanzibar umetuisha. Kwa nini leo sisi tuliotoa "so much" kwa ajili ya Zanzibar kuonekana leo ati ndio "wakoloni"?"

  "Leo hii tunatajwa kwa kejeli, muasisi wa taifa letu akitukanwa hadharani na mtu pekee ambaye aliiokoa Zanzibar na kuipa uhai wake aonekane ni kituko? Wakati wa kusema "imetosha" umefika. Zanzibar iamue kuondoka, na iondoke mwaka huu! Hakuna haja ya kura ya maoni – wamuulize nani kama hadi mke wa Karume anaposimama na kubeza Muungano? Wamuulize nani wakati leo kitu ambacho kisingiwezekana Zanzibar (Mpemba kutawala visiwa hivyo) kinawezekana kwa sababu ya Muungano na hakuna mwenye ujasiri wa kujibu hoja dhidi ya Muungano?"

  Mwandishi analalamika kuwa wanatukanwa lakini wakati huohuo haoni kuwa kuiita Zanzibar ‘kanchi' au "kupe" anaitukana na kuidharau Zanzibar! Kweli Wabara wametoa mengi sana – Wameanza kwa kuwauwa Wazanzibari, wamewararua wake za watu na wasichana bikra mbele ya waume na baba zao, wamewafundisha wasiokuwa na msingi mzuri wa dini kuwanyang'anya raia mali zao, nyumba zao na mashamba yao, wameleta mabaa kwa wingi, wameteremsha malaya katika nchi iliyokuwa haina vitu hivyo na wanateremsha majeshi kila leo kuwapiga Wazanzibari bure bila ya sababu na wengine kuwashitaki kwa mashitaka ya kinyago… kweli ni mengi tu waliyowatunukia Wazanzibari tokea kabla ya kuundwa muungano huu.

  Lula wa Ndali Mwananzela anafahamu vizuri ukweli wa kitarikh na angefanya vyema kutuandikia maalumati yaliyo sahihi yenye ukweli kuliko huu udanganyifu ulio wazi kabisa ambao kila Mzanzibari aliyesoma na kuielewa historia ya kweli ya nchi yake anaona wazi kuwa ni maneno ya kipropaganda yasiyokuwa na ukweli yenye lengo la kuiipa Tanganyika sura nzuri na kuipaka vinyesi Zanzibar. Kwa mfano, mwandishi kusema "kitu ambacho kisingiwezekana Zanzibar (Mpemba kutawala visiwa hivyo). Anasahau kuwa Muhammad Shamte, Rais wa kwanza kabla na baada ya uhuru, alikuwa ni Mzanzibari kutoka Pemba. Wazanzibari ni wamoja na hawana tafauti, atoke Ole, Fumba, Kojani, Tumbatu, Fundo, Msuka au Makunduchi, angepaswa afahamu kuwa Dr. Sheni kuwepo alipo katika uongozi (Uraisi) wa juu sio kwa sababu ya Muungano.

  Na tuendelee kumsoma mwandishi. Ameongeza na haya:
  "Zanzibar inapewa upendeleo ambao hakuna eneo jingine lolote la Muungano linapewa. Inapewa upendeleo katika elimu, jeshi, ubalozi na hata fedha. Ni wananchi wa mkoa gani wa Tanzania ambao wanaweza kudai vinavyodaiwa na Zanzibar? Tumesikia watu wa Mtwara wakidai upendeleo wa pekee kwa sababu na wao ni sehemu ya Muungano? Tumesikia lini wananchi wa Singida wakisema nao wao wapewe ubalozi, au uwakilishi kwenye taasisi mbalimbali kwa kuangalia asilimia ya makabila mengine (hasa Wanyakyusa, Wahaya, na Wachagga)? Hakuna; lakini Zanzibar wanaweza kusimama na kudai upendeleo huu ati kwa sababu "zilizoungana ni nchi mbili"! Wakati huo huo hakuna mbara hata mmoja ambaye amewahi kusimama kudai kuwa Serikali ya Zanzibar itoe nafasi kwa wabara ili kuimarisha Muungano!"

  Mnaona maneno hayo! Nchi mbili zinazosemekana zimeungana leo tunaambia kuwa "Zanzibar inapewa upendeleo ambao hakuna eneo jingine lolote la Muungano linapewa." Yaani Zanzibar imekuwa jimbo la Tanganyika! Yaani, kama mtu hana fikira za kikoloni hawezi kuilinganisha Zanzibar (nchi) na Mtwara (jimbo). Halafu mambo kama ilimu na kilimo hata hayamo katika muungano… mradi hoja yote ni ya kuiona Zanzibar ni kama jimbo dogo la Tanganyika. Ikiwa msomi alionawirika ana fikra kama hizi, sijui wengine wako vipi! Ndipo Wazanzibari wakafadhili watokane na muungano na nchi yenye wasomi, wanasiasa na wafanya kazi serikalini wengi wenye fikra kama hizi.

  Mwandishi anaendelea:
  "Lini umesikia muswada umepitishwa Zanzibar kutoa upendeleo kwa wananchi wa Mafia? Au wananchi wa Kilwa? Hawawezi kwa sababu mara moja watadai "udogo wa visiwa"!"

  "Sasa cha Tanzania ni cha Watanzania wote (wakiwemo Wazanzibari) lakini cha Zanzibar ni cha Wazanzibari wote na si cha Mtanzania yeyote. Kwa nini tuendelee na mfumo huu wa kinyonyaji? Kwa nini tuendelee kuipa Zanzibar upendeleo usiostahili. Zanzibar ina wasomi wengi na ina watu wengi wako nje na wengi wako Bara; wakati umefika hawa wote warudi Zanzibar na kuanza kujenga nchi yao. Waachilie nafasi zao kwenye Muungano – kwa kuanzia na Dk. Ghaib Bilal na wengine wote ili nafasi hizo zishikwe na Watanganyika."

  Tunarudi palepale: "Zanzibar si nchi" kwa mtizamo wa watawala. Pili, kwani ni nani aliyekuja na huu mfumo wa serikali mbili na si tatu? Si huyohuyo emperor dictator Nyerere? Hata wakili wa Zanzibar hakurukhusiwa kuipa Zanzibar ushauri, na akhasi zaidi, Wazanzibari wenyewe hawakupewa fursa ya kuamua kama wanautaka muungano na Tanganyika au la. Palipitishwa usanii mkubwa sana kama unaopitishwa hivi sasa wa Wazanzibari kutokupewa fursa ya kujiamulia kama wanataka waendelea na muungano au kinyumeche.

  Muungano wa nchi ni jambo kubwa sanasana ambalo lazima watu wapewe fursa ya kusema kama wanautaka au hawautaki. Katika udikteta wa Nyerere na Karume ulifanywa muungano bila ya ridha ya watu wao, lakini, moja katika makubaliano ya muungano ilikuwa baada ya miaka kadhaa watu wa Tanganyika na wa Zanzibar walikuwa waulizwe kama wanataka muungano uendelee ama la. Nyerere alifanya mazingaombwe yake na watu hawakupewa fursa hiyo wakati ulipowadia. Sasa zinasikika sauti kali, tena waziwazi za Wazanzibari wengi kuwa wanadai haki yao ya kupiga kura kusema kama wanautaka muungano ama hawautaki. Kutokuwapa Wazanzibari na Watanganyika fursa ya kuziamulia nchi zao kukhusu hatma ya muungano wenyewe na kulazimisha wachague muungano wa aina gani wanautaka ni usanii wa hali ya juu kabisa kwani ni kuikiuka kwa makusudi khatua na haqi ya wananchi kuamulia mustaqbal wa nchi zao. Kwa Wazanzibari wengi sana kukiuka khatua hii ni udikteta mbaya sana. Kama unazungumzia udugu na Watanganyika kwa kweli si Watanganyika wote walio ni ndugu zao Wazanzibari, si kwa chochote si kwa lolote. Udugu unakuja watu wanapokuwa na mambo yao mamoja.

  Suala: Vipi Wazanzibari wanaweza kufanya udugu na serikali na wafuasi wake waliowateremshia maafa tokea 1964 mpaka leo. Tunaambiwa kuwa Zanzibar imefanya "muungano" na Tanganyika kwa sababu Watanganyika ni ndugu zao. Suala: Watanganyika wepi ni ndugu za Wazanzibari, na ni ndugu zao kivipi? Iwapo ni ndugu zao kwa sababu wengi wao wana rangi "nyeusi" basi na wafanye muungano na Kenya, Nigeria, Congo, Bara Hindi, Australia, Fiji hadi Jamaica na Haiti ambako kumejaa watu "weusi." Kufanya muungano kwa ajili tu ya rangi za ngozi za watu ni uwehu.

  Tunaambiwa kuwa kumefanywa "muungano" kwa sababu Wazanzibari na Watanganyika ni ndugu. Hakuna anayeweza kukataa kwa kusema kuwa hakuna kabisa idadi ya watu Zanzibar ambao wana ndugu zao Tanganyika, lakini tujiulize: Wazanzibari na Watanganyika wepi waliokuwa ni ndugu? Wengi wao licha kuwa hakuna nao ya udugu bali ndani ya nafsi zao Watanganyika wengi wanawachukia Wazanzibari. Maneno ya "kupe" na "ng'ombe" na mengineyo yanadhihirisha kutokuwepo huo udugu. Katika hali hii, udugu umetokea wapi? Kwahivyo, na hii pia si sababu ya kuunganisha nchi; kama ni hivyo, basi kuna ndugu za Wazanzibari kwingi tu Duniani. Kwanini basi wasiziunganishe nchi zote kulikojaa watu waliotoka Zanzibar kwa ajili ya mavamizi na mauwaji ya halaiki yaliyosababishwa na mavamizi hayo – ambayo yalipikwa Tanganyika na kupakuliwa Zanzibar – na kusababisha pia Wazanzibari wengi sana waliokuwa hawajauliwa katika mavamizi kuihama nchi yao?

  Kuna wanaosema kuwa ni ndugu kwa sababu Wazanzibari na Watanganyika wanasema lugha moja. ikiwa hii ni sababu ya kuunganisha nchi, basi na tuuganishe pia na Kenya hadi Congo na kutoka Ngazija hadi Dubai maana kuna wengi tu wanaosema Kiswahili katika nchi hizo.

  Na kuna vijiudhuru vingine tunavyotolewa, lakini kila udhuru tunaopewa kuambiwa kuwa ni sababu ya kuundiwa "muungano" nauona unavuja kama avujavyo mtoto mchanga anaposhikwa na haja, na tukiongezea maneno ya chuki kubwa ya Julius Kambarage Nyerere kuwa angelikuwa na uwezo angeliibura Zanzibar na kutokomeza mbali katika Bahari ya Hindi, tunagundua kuwa wale wanaoona kuwa kweli kuna udugu baina ya Zanzibar na Tanganyika na muungano umefanywa kwa ajili ya udugu huo, watu hao bila ya shaka wanatudanganya na wenye kuukubali udanganyifu wao nawaweka kwenye fungu maalumu la utepetevu wa akili. Nyerere hakufanya "muungano" na Karume kwa sababu akimpenda sana Karume wala kuwa aliipenda sana Zanzibar. Iwapo unayakubali haya ninayokuelezea, basi jiulize: Udugu huo umetokea wapi? Kusema kweli, huu uliokuweko, tokea mwanzo wake, si muungano bali ni mmezo wa kumezwa Zanzibar na Tanganyika, na mazungumzo yote na mijadala ya katiba ya muungano ni mazungumzo ya kupunguza joto tumboni kwa kutoa upepo, mnajua wapi, lakini mambo bado yamebakia tumboni.

  Wafuasi wake Nyerere bado wanaendesha serikali na kuendelea na ukhabithi wao hadi leo. Jana tu Wazanzibari walikusanyika msikitini kuwaombea watu wao waliofariki katika maafa ya kuzama baharini na majeshi ya Tanzania yakawaingilia mpaka msikitini na mabuti na kuwatwanga kwa marungu watu waliookuwa katika ibada. Wengine wakawatupia mabomu yenye madawa, wengine wakaingiliwa mpaka majumbani mwao bila ya sababu na humo pia wakatupa mabomu ya madawa bila ya kujali kuwa mlikuwa na watoto wachanga. Mradi ukhabithi wao juu ya Wazanzibari wa kawaida hausemeki! Soma ya Barazani kwa Ahmed Rajab katika gazeti la Raia Mwema makala yaitwayo "Polisi wanapochafua amani watu walindwe na nani?" Toleo la 251, 25 Jul 2012, utazidi kutatukiwa na yaliyojiri.

  Nikijaribu kuelezea ya ukweli sina budi kusema kuwa chini ya utawala wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Tanganyika ilijipatia sifa kubwa sana ya kuwa msitari wa mbele kabisa katika kujitolea kwa hali na mali kuzisaidia nchi jirani na za mbali kujigomboa kutokana na ukoloni uliowabana sana. Kwa hili lazima tumpongeze Mwalimu na Watanganyika waliomuunga mkono kwa juhudi zao. Lakini wakati huohuo kuna ya kusikitisha aliyoyatenda Mwalimu. La Biafra ni mojawapo na jingine ni hili la kuwateremshia maafa mapevu Wazanzibari 1964 na kuendelea kuwasononesha kwa miaka 48. Ni aibu kubwa kuiona Tanganyika imejiweka pahala pabaya sana kama ilivyojiweka katika mas-ala ya Zanzibar. Tanganyika haitapungukiwa chochote iwapi itaiachilia Zanzibar iwe huru tena, na zote nchi mbili kuwa majirani wema badala ya ubia mbaya. Kuilazimisha Zanzibar ibakie katika "muungano" kwa kila mbinu za usanii na kwa marungu, mabomu na marisasi ni kuzidi kudhihirisha ubaya wa ukoloni huu. Wala hakuna watakaolaumiwa na Dunia ila Tanganyika. Kwahivyo kwanini Tanganyika izidi kujiharibia jina lake Duniani na sifa zake kwa, kama wanavyosema wenywe, "kajinchi kadogo" kama Zanzibar?

  Na kwa upande wa Zanzibar, namaliza sehemu hii kwa kunakili maneno mazito aliyoyaandika Dr, Hassan Omar Ali hivi karibuni:

  "[...] Ukweli ni kuwa hata iwe Zanzibar inapata faida kede wa kede kutoka Tanganyika, hiyo haiwi hoja ya kuendelea kuwa katika mfumo huu wa Muungano kama Wazanzibari wenyewe hawautaki. Lakini zaidi, ni wazi kuwa faida nilizozitaja ni ndogo mno ukilinganisha na hasara zinazosababishwa na kukosekana uhuru wa kujitawala na kujiamulia mambo yetu wenyewe. Uhuru huo thamani yake haina mfano na uzito wake unazidi kila kitu!"

  Yanayofuata aliyoyaelezea Lula wa Ndali Mwananzela nakubaliana nayo kimsingi.
  Ibrahim Noor

  Tuwasaidie Wazanzibari waache maandamano
  Sasa sisi watu wa Tanganyika (Tanzania proper) tunaweza kuwasaidia Wazanzibar kuondoka kwenye Muungano ili waweze kujenga taifa lao jipya lenye maziwa na asali; taifa ambalo wakipiga zumari hadi maziwa makuu wanacheza; taifa ambalo kila mtu anaishi kwa furaha na kula halua na tende huku wakicheza gombe sugu! Tuwasaidie Wazanzibar watoke kwenye Muungano mapema zaidi kuliko ilivyo sasa.

  Tusiwaache wafanye makongamano na maandamano yasiyoisha kudai "uhuru kamili" wakati njia ya kuwapatia uhuru "kamili" ni rahisi sana. Niliandika huko nyuma kuwa njia rahisi zaidi ya kuwaondoa Zanzibar kwenye Muungano ni kuwahamiza wawakilishi wao – kina Jussa na wenzake – waandike sheria ya kura ya maoni ya kutoka kwenye Muungano na waitishe kura yao kabla ya mwisho wa mwaka huu ili hatimaye ifikapo Disemba 31, 2012 Zanzibar iwe taifa huru nje ya Muungano. Miezi imepita na sioni juhudi zozote za Wazanzibari kutoka kwenye Muungano zaidi ya kuendelea kutuambia kuwa wanataka kutoka!

  Sasa kwa vile kina Jussa hawana ujasiri huo na kwa vile wana uamsho hawana uwezo wala ujasiri wa kuwashawishi wawakilishi wao kuitisha kura ya maoni mapema ili watoke kwenye Muungano sisi upande wa Tanganyika inabidi tuwasaidie. Siyo kwa kuidai Tanganyika kama wengine wanavyotaka tufanye; la hasha. Tukiidai Tanganyika maana yake tunataka Zanzibar iwepo na Tanganyika iwepo ili kuwe na serikali tatu. Sasa tukiwa na serikali tatu bado Tanganyika italipa gharama kubwa zaidi ya kuiendesha.

  Kwa sababu huwezi kuwa na serikali tatu ambazo hizo serikali mbili zinachangia 50 kwa 50, kwa sababu mara moja itaonekana Zanzibar inanyonywa. Itakuwaje watu milioni 45 wachangie sawa sawa na watu milioni mbili? Wazanzibari hawa hawa wataanza kulia kuwa Tanganyika inawanyonya bado na watataka tuchangie kwa "asilimia" huku wao wakitaka kuchangia asilimia kidogo kwa sababu ni ‘wachache' na uchumi wake ni ‘mdogo'. Tusikubali mkenge wa kudai Tanganyika.

  Njia pekee ya kuwasaidia Wazanzibari kutoka kwenye Muungano ili wasitusababishie maumivu ya kichwa ya kudumu ni kudai Tanzania moja, nchi moja. Kwa vile Rais Kikwete na CCM wanasema hawataki tuuvunje Muungano bali tujadili "muundo wa Muungano" naomba nipendekeze kuwa muundo pekee unaofaa kwa Muungano ni wa "nchi moja, taifa moja".

  Hakuna mantiki ya kuwa na "nchi mbili ndani Muungano". Haiingii akilini uwe na "nchi ndani ya nchi". Sasa kama nchi iko ndani ya nchi haiwezekani kuwa na nchi mbili; bali moja. Ukiunganisha maji na maji, huwi na maji mawili bali maji tu!

  Sasa njia pekee ya kuwasaidia kuondoka kwenye Muungano ni kudai "nchi moja taifa moja". Inapopita timu ya kukusanya maoni ya Katiba Mpya na linapokuja suala la Muundo wa Muungano watu wa bara wasidai "serikali tatu". Wadai "serikali moja". Yaani kutakuwa na serikali ya Muungano na tawala za mahali au serikali za mahali na mahali. Tayari tumeshakuwa na serikali mbili na zimetuletea matatizo haiwezekani tukafikiria kuwa tukiongeza serikali ya tatu tutakuwa tumepunguza matatizo. Haiwezekani ukiwa na mtoto mmoja uone ni tatizo halafu ukiwa na watatu utakuwa umepunguza!

  Hivyo, watu wa bara tunajua kabisa tukiimeza Zanzibar rasmi – hakuna cha BlW (Baraza la Wawakilishi), hakuna Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, hakuna bendera wala wimbo wa "taifa" la Zanzibar na hakuna Rais wa Zanzibar wala chochote cha ‘Zanzibar". Tunapoamua kuimeza ndani ya taifa moja Zanzibar inakuwa sehemu kweli ya Jamhuri ya Muungano. Hili pendekezo ndilo ambalo watu wa bara tunahitaji kulisimamia na kulidai kwenye mchakato huu wa Katiba Mpya.

  Kwa sababu Wazanzibar wenye uchungu na nchi yao hawawezi kukubali. Hawawezi kukubali Zanzibar imezwe kabisa. Watakataa na wataamua bora watoke. Uchaguzi utakuwa ni kumezwa au kutoka na wao watachagua kutoka – kitu ambacho ndicho tunataka kuwasaidia kufanya. Sasa wakishatoka Zanzibar isifikirie itakuwa na upendeleo maalumu kwa Tanganyika.

  Baadhi ya vitu vya kwanza ambayo serikali ya Tanzania Mpya itahitaji kufanya ni kuweka masharti makali ya ukaazi na uzawa ili kwamba Wazanzibar wasije wakajipitisha kama Watanganyika. Pamoja na hilo kuweka usimamizi mzuri wa kodi ili kuhakikisha vitu vinavyoingia kutoka Zanzibar vinakidhi kiwango cha bara na kodi nyingine muhimu. Tusije tukaacha kuwa baada ya kutoka Wazanzibari wakaanza kupata upendeleo ambao walikuwa bado wanaupata. Tutatumia vigezo vile vile vya kuhusiana na nchi kama Wakenya, Waganda na Wanyarwanda.

  Ndugu zangu katika kuendeleza kampeni hii ya Let Zanzibar Go ambayo tumeiasisi tuanze kuitakia kila la kheri Zanzibar na kusema "bye bye" Muungano. Tuwasaidie watoke kwenye Muungano kwa kuanza kutaka kuundwa kwa serikali moja – na si tatu. Hii ndio njia pekee, ya uhakika ya kuweza kuzungumzia suala la "muundo wa Muungano" bila kutaka kuuvunja moja kwa moja (kitu ambacho sheria ya katiba inakataza). Tukiidai serikali moja Wazanzibar hawatotaka watatoka nasi tutaipata Tanganyika yetu na ili kuzidi kuwaudhi maadui wa Muungano bado itapewa jina la Tanzania; au tukipenda kurudisha jina la kale zaidi la AZANIA!
   
 2. Jagermaster

  Jagermaster JF-Expert Member

  #2
  Jul 28, 2012
  Joined: Nov 6, 2010
  Messages: 656
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 0
  You seems to be colour blind buddy, Mapinduzi yalikuwa purposely kupindua serikali ya kiarabu ambayo asili yake ni Oman na kuweka serikali ya Wabantu na hilo liliwezekana. Hii maneno ya Wanzanzibar as if wazanzabar wote ni wabantu au kama vile hakukwepo na ubaguzi wa rangi Zanzibar, you are missing the salient point about 1964 Revulution. The point is Nyerere na viongozi wengine wa East Africa hawakupenda kuwepo kwa dola ya kiarabu jirani kabisa na nchi zetu katika Pwani ya Africa Mashariki na pia nchi za Magharibi hazikufurahia na mpaka sasa hazifurahii kuwa dora ya kiislam ndani ya Pwani hii na huo ndio ukweli.
   
 3. J

  JokaKuu Platinum Member

  #3
  Jul 28, 2012
  Joined: Jul 31, 2006
  Messages: 12,769
  Likes Received: 4,982
  Trophy Points: 280
  ..hivi hawa wanadhani ASP walikuwa wanafurahia hujuma na ubaguzi uliokuwa ukiendelea Znz?

  ..badala ya kupotosha historia, mwandishi angetueleza faida za kiuchumi na kijamii tunazozipata wa-Tanganyika ktk muungano huu. bcuz he did not touch on that, naamini hakuna.

  NB:

  ..hakuna pesa inayokusanywa Znz na kuletwa Tanganyika. makusanyo yote ya TRA Zanzibar kubakia huko.

  ..uchumi wa Znz umeporomoka kwasababu ya kupungua kwa uzalishaji wa karafuu. Tanganyika wala Nyerere hakuwa na say ktk uendeshaji wa sera za uchumi za Zanzibar.

  ..mwisho, Znz ilikuwa ina full control na akiba yao ya fedha za kigeni. walianza kuitumia vibaya wakati wa Karume ambapo serikali ilifikia kununua peremende-- rejea mgogoro wa Azizi Twala na Karume. Jumbe naye alinunua presidential jet wakati znz kuna uhaba wa chakula. huo ni baadhi ya ushahidi kwamba fedha za znz zimefujwa na viongozi wa znz.
   
 4. d

  dandabo JF-Expert Member

  #4
  Jul 29, 2012
  Joined: Feb 18, 2012
  Messages: 303
  Likes Received: 81
  Trophy Points: 45
  sijawahi kuona kichwa maji kama wewe unayejiita mzenji kumbe mu-omani!
  Kweli wazanzibar mnakubali kupotoshwa kwa kiwango hiki?
   
 5. gollocko

  gollocko JF-Expert Member

  #5
  Jul 29, 2012
  Joined: Dec 20, 2011
  Messages: 2,830
  Likes Received: 1,542
  Trophy Points: 280
  Come on! Wazanzibar maneno meeengi ili mradi hawakosi cha kusema lakini vitendo hakuna. kila siku hatuutaki muungano lakini hamuuvunji, mnasubiri nini? hizi ni sitaki nataka. Chukueni hatua sasa mvunje na mwende zenu!
   
Loading...