Majambazi yateka kijiji yaua Mfanyabiashara

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
WA T U k u m i w a n a o s a d i k i w a kuwa majambazi wamemuua kwa risasi mfanyabiashara mmoja na kujeruhi wengine kadhaa katika kata ya Buselesele wilayani Chato, mkoani Kagera kisha kuwapora zaidi ya sh. milioni 7. Majambazi hayo
yaliendesha operesheni hiyo kwa zaidi ya saa mbili katika vijiji vya Buselesele, Mapinduzi na katika kijiji cha Katoro kilichoko wilayani Geita ambapo kabla ya tukio hilo yalifyatua risasi kadhaa angani na kurusha bomu la moto.
Aliyeuawa katika tukio hilo lililotokea jana saa 8 usiku, ni Bw. Joseph Munis (40) mfanyabiashara wa viatu ambaye alipigwa risasi mgongoni na nyingine kisogoni ambapo licha ya kumuua yalimpora sh. milioni 3.2.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Bw. Henry Salewi katika mahojiano kwa njia ya simu na gazeti hili, alithibitisha kuwepo tukio hilo ingawa alisema alikuwa hajapata taarifa kamili.
“Ni kweli tukio hilo lipo hivi sasa nasubiri taarifa kamili kutoka kwa RCO aliyeko kwenye eneo la tukio, hivyo nipigie baadaye, “alisema kamanda huyo lakini hata hivyo Majira lilipomtafuta baadaye, simu yake ilipokelewa na msaidizi wake ambaye alieleza kuwa kamanda huyo alikuwa kwenye kikao cha dharura kwa Mkuu wa Mkoa.
Wakizungumza na Majira katika eneo la tukio, baadhi ya wananchi walisema kuwa majambazi hayo kabla ya kupora na kuua, yalifyatua risasi kadhaa angani pamoja na kurusha bomu la moto ambapo watu walijificha majumbani na hakuna aliyethubutu kutoka nje.
Mmoja wa wafanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina la Bw. Robert Elias (28) ambaye chumba chake kipo jirani na cha marehemu alisema; “Nilisikia risasi nje, nyingine ikasikika jirani kabisa na mlangoni, nikataka nitoke lakini roho ilisita niliingia uvunguni na kumwacha mke wangu peke yake.”
Aliendelea kueleza baada ya muda kidogo, alishtukia watu hao wakiingia chumbani kwake na kumwamuru mkewe awape fedha na kudai hana ndipo wakaanza kupekua chumba kizima na walipokosa wakaondoka ndipo alisikia kelele kwa mpangaji mwenzake.
Naye Bi.Anna Masanyiwa ambaye ni shemeji wa marehemu alisema kuwa watu hao walipofika walivunja mlango wa chumba alimokuwa amelala na kuuliza mahali alipo Bw. Munis ambapo aliwaonesha.
Wakati akiwaonesha kumbe marehemu na mkewe tayari walikuwa wamesikia sauti hizo, yalipofika alijaribu kuzuia mlango ndipo yalimfyatulia risasi na kufa papo hapo kisha kupora kiasi hicho cha fedha. Majambazi hayo yalimjeruhi pia mfanyabiashara mwingine katika nyumba hiyo aliyetajwa kwa jina moja la Bw. Sadiki na kumpora zaidi ya sh.laki nane na baadaye yalipora tena kwa Bw.Tawaqal Charles.
Mbali na kumpora Bw. Charles ambaye ni mfanyabiashara wa duka la nyama katika kijiji cha Mapinduzi ,yalimjeruhi kichwani na sehemu mbalimbali za mwili huku yakimtishia kumkata kwa shoka ambapo pia yalimjeruhi mkewe Bi. Naomi Emmanuel na mtoto aitwaye Matokeo ambapo yalikuwa yakidai kupewa sh. milioni 10.
Diwani wa Kata ya Buselesele, Bw. Chrispine Kagoma, aliliambia Majira kuwa alijikuta akidondosha simu yake ya mkononi kutokana na mlio wa bomu lililorushwa na kusababisha hofu kwa wananchi. Diwani huyo alisema kuwa ipo haja kwa wananchi kuanza kufanya doria za mara kwa mara kudhibiti uhalifu huo huku akilitaka Jeshi la Polisi kuongeza juhudi za kuwalinda raia wake badala ya kulinda vituo pekee.
Habari zinasema kuwa majambazi hayo yaliendesha uhalifu huo katika kijiji cha Katoro ambacho ni jirani na Buselesele na kupora zaidi ya sh.laki 5 kabla ya kutokomea baada ya polisi kutoka kituo cha Buselesele na Katoro kufika eneo hilo.
 
Back
Top Bottom