Majambazi waua mwanamke, saba mbaroni | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Majambazi waua mwanamke, saba mbaroni

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Sumbalawinyo, Jan 28, 2010.

 1. Sumbalawinyo

  Sumbalawinyo JF-Expert Member

  #1
  Jan 28, 2010
  Joined: Sep 22, 2009
  Messages: 1,286
  Likes Received: 25
  Trophy Points: 0
  Majambazi yameendelea kutingisha nchi na katika tukio la kuhuzunisha watu wawili wakiwa na silaha wamemuua kwa kumpiga risasi kichwani mke wa mfanyabishara maarufu wa madini ya tanzanite aliyetajwa kwa jina la Jacqueline Deo (28) mkazi wa Lemara mjini Arusha.
  Akizungumzia tukio hilo ambalo ni kati ya matatu yaliyotingisha nchi jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Basilio Matei, alisema kuwa lilitokea juzi saa 3:30 usiku wakati mwanamke huyo akirejea nyumbani kwake akiendesha gari namba T125AUW
  Alisema kuwa baada ya mwanamke huyo kusimama mbele ya geti la nyumba yao, alivamiwa na watu hao waliokuwa nyuma yake wakiwa na pikipiki aina ya Toyo na kumwamuru afungue kioo cha dirisha cha gari upande wake.
  Kamanda Matei alisema baada ya mwanamke huyo kutii amri ya watu hao wanaodaiwa kuwa majambazi waliokuwa wamemwelekezea bastola katika paji la uso, mmoja wao alimmiminia risasi kadhaa kichwani na kufa papo hapo. Alisema muda mfupi baada ya milio ya risasi kusikika, ndugu zake walitoka nje kuangalia kulikoni na kumkuta marehemu na walipojaribu kumkimbiza hospitali ikawa tayari ameshakata roho.
  Baada ya watu hao kumuua walitoweka bila kuchukua kitu chochote zaidi ya simu yake ya kiganjani.
  “Tunaendelea kuwasaka wahusika wa tukio hili, tunafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wahusika wa tukio hili wanatiwa mbaroni na kupelekwa mbele ya vyombo vya sheria,” alisema.
  Alisema baada ya watu hao kumpiga risasi mwanamke huyo, walikimbilia kusikojulikana wakitumia pikipiki.
  Alifafanua kuwa Jeshi la Polisi linafanyia uchunguzi wa kina kuhusiana na mazingira ya mauaji hayo hasa baada ya wauaji kutochukua chochote kutoka kwa marehemu zaidi ya simu ya mkononi.
  Alisema kuwa taarifa za awali zinasema kuwa mwanamke huyo alitoka msibani katika eneo la Moivaro, nje kidogo ya mji wa Arusha.
  “Tukio hili lina sura mbalimbali tunafanya uchunguzi wa kina, kwanza mwanake huyu ni mama wa nyumbani tu na mume wake ndiye pengine angelengwa na majambazi kwa kuwa ni mfanyabiashara wa madini,” alisema na kuongeza: “Tunafanya uchunguzi kwa kila shaka iliyopo.”
  Matukio ya mauaji ya aina hiyo yamekuwa yakitokea mara kwa mara mjini hapa. Katika siku za hivi karibuni, mfanyabiashara wa madini aliuawa katika mazingira ya aina hiyo na wauaji hawakuchukua chochote zaidi ya simu ya mkononi.
  Katika tukio la pili, Polisi mkoani Pwani imewakamata majambazi saba wakiwa na silaha wakijiandaa kwenda kupora fedha za mauzo katika kituo cha mafuta cha Gaza kilichopo Kibaha kwa Mfipa.
  Akizungumza na waandishi wa habari, jana Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Absalom Mwakyoma, alisema tukio hilo lilitokea jana asubuhi huko Maili Moja wilayani Kibaha ambapo polisi walipata taarifa za majambazi hao na kuanza kuwafuatilia tangu Ubungo na kuwakamata.
  Alisema watuhumiwa waliokamatwa ni wawili wa kundi la kwanza ambao ni Mkwabi Mtiba (40), mkazi wa Yombo Dar es Salam ambaye alikutwa na bastola moja aina ya Browing yenye risasi nne na Juma Chacha (30), mkazi wa Mbagala Dar es Salaam ambaye alikutwa na bastola aina ya Makalov iliyokuwa na risasi sita.
  Mwakyoma alisema watuhumiwa hao walijigawa katika makundi mawili ambapo matano yalitangulia kwenye kituo cha mafuta cha Gaza kwa ajili ya kufanya uporaji, baada ya kubaini kuwa meneja wa kituo hicho alikuwa akipeleka pesa benki.
  Alisema wakiwa wanatumia gari ndogo aina lenye namba T753 ALW walijaribu kumteka Meneja wa kituo hicho, Kurwa Daud Abdalah (33), aliyekuwa akitumia gari namba T313 BBD Toyota Mark II akiwa na fedha, lakini aliwakwepa na kukimbilia kituo cha polisi cha Tumbi kutoa taarifa za kuwepo kwa majambazi hayo.
  “Majambazi haya matano ambayo nayo yameshakamatwa yalishindwa kumpora fedha hizo zilizokuwa zikipelekwa benki kwa kuwa yalikuwa yakisubiri wenzao tuliokwisha kuyakamata kwani wao ndio waliokuwa na silaha kwa ajili ya kurahisisha uhalifu wao,” alisema Mwakyoma.
  Kamanda Mwakyoma alitaja watuhumiwa wengine watano kuwa ni Hassan Sabi (27), mkazi wa Kinondoni Dar es Salaam, Hussein Farji (31), mkazi wa Kiwalani; Ramadhani Shabani (22), mkazi wa Magomeni Kagera; Jacob Maganga (32), mkazi wa Yombo Kiwalani na Charles Mbaga (28), mkazi wa Kinondoni.
  Alisema watuhumiwa hao wanahojiwa na polisi na watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
  Hata hivyo, amewataka wananchi wa mkoa huo kuendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali katika kufanikisha kuwafichua wahalifu.
  Katika tukio la tatu, mkazi wa kijiji cha Suwa Machimboni wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga, Jumanne Salimu (35), ameuawa kwa kushambuliwa na wananchi kwa tuhuma za ujambazi.
  Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Simon Sirro, mtuhumiwa huyo aliuawa Januari 25, mwaka huu majira ya saa 1:30 usiku kijijini hapo baada ya kumvamia Joseph Simon kwa lengo la kumpora fedha.
  Sirro alisema baada ya Simon kuvamiwa alipiga yowe kuomba msaada na watu waliofika kwenye eneo la tukio walimshambulia mtuhumiwa huyo hadi kufa.
  Alieleza kuwa mtuhumiwa huyo ambaye ni mkulima wa kijiji cha Mazingara, alimvamia Simon ambaye ni mfanyabiashara baada ya kupata habari kuwa alikwenda na fedha kwa ajili ya kununua madini kwenye kijiji hicho ambacho ni cha machimbo ya madini. Hata hivyo, hakuna mtu aliyekamatwa na polisi inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini na kuwafikisha mahakamani watu waliyohusika na mauaji hayo.
  Imeandikwa na Charles Ole Ngereza, Arusha, Margareth Malisa, Pwani na Dege Masoli, Handeni.
  [​IMG]
  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Basilio Matei


  CHANZO: NIPASHE
   
Loading...