MAISHA YA UTEGAJI WA LUBONDO

MAISHA YA UTEGAJI WA LUBONDO

josephdeo

Member
Joined
Nov 23, 2015
Posts
96
Reaction score
208
Makaburi yamezika ndoto nyingi, ndio! wala sina uwezo kulikataa hilo ila tu ninalo la kuongezea kwenye hilo. Kama ilivyo kwa makaburi pia mapenzi nayo yamechangia sehemu nyingine kubwa ya kuzika ndoto za watu wengi. Nasema haya nikiwa muhanga na si mhamasishaji.

Naweza kusema maisha ni fumbo gumu kulitatua, haswa ujuzi wa Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema udhihirika pale ambapo alitunyima fursa wanadamu kutokuijua kesho yetu. Kwa sehemu kubwa maisha yetu yamekuwa jana na sasa huku kesho na baadae vikiendelea kuwa fumbo ambalo kupatikana jibu lake itachukua kumalizika kwa ulimwengu.

Nakiri wazi pasina uficho kuwa niliteleza na kukosea ila dunia ilinichagulia njia ngumu mno kwa upande wangu kupita mara baada ya kutoka kwenye njia ya awali. Njia ambayo ilinikumbusha na kunifunza kuwa ikiwa malezi ya wazazi hayakuingia vyema akilini basi ulimwengu ungekupa malezi ya kikatili mno. Wahusika wakuu wa malezi hayo wakiwa ni walimwengu wenyewe ambao wasingeweza kukukosoa kwa makosa yako bali kukuadhibu. Hata wasikupe nafasi ya kujutia ili ujisahihishe bali wangeongeza kidonda juu ya kovu.

Mengi nimeyapia achilia mbali kuyaona na laiti kama ningejua kuwa ningekwenda kukabiliana nayo basi ningechagua chaguzi lingine tofauti na hilo. Nashukuru nipo hapa sasa hata baada ya kuzipita nyakati hizi zilizoacha kumbukumbu isiyofutika kamwe.

Mauti pekee ndio yatafanyika kuwa tamati wa hiki ambacho upita akilini mwangu. Sasa zinapita kama kumbukumbu mbaya maishani ila nilithibitisha kuwa mpaka binadamu kufariki basi anakuwa kakiepuka kifo mara kadhaa kabla. Hili nalikubali kwani hata wakati mwingine siamini kama niko hai, eti nami bado niko kwenye ulimwengu huu!. Nikisema ya kuwa wakati mwingine siamini kama bado niko hai basi fahamu kuwa sitanii kwani ni zaidi ya mara moja nimekiepuka kifo.

Ninacho kisema hapa ni ile hali ya kukiona kifo mahili kadhaa toka ulipo simama kisha kinakupita na kwenda zake. Nawe unaweza kujitiza ili kuhakikisha hilo ni mara ngapi umepitia nyakati kama hizo za kuhisi ulipenya na kukikwepa kifo. Basi tuachane na hayo kwani si tija kwenye simulizi yetu badala yake nilitaka kukuonyesha tu.

Hata kwa theluthi ya punje ya mchele sikuwahi kuwaza ya kuwa ipo siku eti nami nitakuja kuwa mvuvi. Sikuwahi kwa kuwa nyumbani hakuna ambaye amewahi kujihusisha na shughuli hii. Zaidi ya hapo labda kula samaki wabichi ambao sikujua hata wanapatikanaje. Kwa wakati huu ungeniambia kuwa baada ya miaka kadhaa mbele nami nitakuwa kati ya wazalishaji wa bidhaa hii ya samaki basi ningekukatilia katu.

Kamwe nisingekubaliana na wewe! Ubishani mkali ungezuka baina yetu. Ndoto yangu ilikuwa nije kuwa askari mpelekezi na ndicho kilichokuwa akilini mwangu pekee, si uvuvi!. Ila maisha haya yaache yaitwe maisha kwa sababu kuna wakati inatubidi kukubali kuishi kati ya kile unachokihitaji na uhalisia wa maisha yako. Japo sikuwa kati ya wanafunzi bora katika darasa letu ila nilikuwa kati ya wanafunzi walioyahimili vyema masomo.

Si tu shuleni bali mpaka nyumba nilikuwa nikiweza kumheshimisha mzee wangu na kumfanya kutamba mtaani kwa matokeo ya mitihani yangu. Familia iliweka matumaini yao mengi kwangu kwa minajili ya kuja kuwakomboa na janga la umasikini hapo baadae. Labda waliweka matarajio makubwa kuliko uhalisia wenyewe na ndio ikawa sababu ya kunichukia pale ambapo niliteleza na kuanguka.

Ila ilikuwa ni haki kwao kwani sikuwaangusha kwenye mtihani wa kumaliza darasa la saba nilipata wastani wa 210 kati ya 250 uliokuwepo. Sikuishia hapo bali hata masomo ya shule ya upili nayo niliyahimili vyema. Ila safari yangu ilifanana na moto wa mabua ambao uliwaka kwa kasi mno mwanzoni ila ulishindwa kuhimili kasi yake baada ya mda mfupi baadae. Nasema hivyo kwa kuwa nilikuja kukengeuka.

Hilo lilijitokeza mara baada ya kupata balehe na sauti yangu kuwa ya kiume tofauti na ya kivulana niliyokuwa nayo. Kwa mbali mazalia ya ndevu yakaanza kukipamba kidevu changu huku kifua nacho hakikukubali kuachwa nyuma nacho kilianza kustawisha nywere ndongo ndongo. Shida yote ilianza mara baada ya haya kutokea kweli adhabu zetu huanza mara baada ya kupata vile tulivyovitamani. Ndio nami adhabu yangu ilipoanzia hapo mara baada ya kupata balehe niliyokuwa nikihitamani.

Macho yangu kwa wakati huu yalipomtizama binti hayakuwa yale ya kirafiki tena bali matamanio ya kujua kile alichokistiri ndani kilifananaje. Sijatokwa na kumbukumbu za maisha ya shule bado kwani mtihani wa kidato cha pili niliofanya mwaka 2012 nilikuwa mwanafunzi pekee kutoka mtaa wetu niliyefaulu kwenda kidato cha tatu. Wengine wanne ambao tulisoma kidato kimoja ila shule zikiwa tofauti hawakufanikiwa kwenda mbele na wawili kati yao waliacha shule.

Kwanini mzee wangu alitembee kifua mbele?, Sababu za kufanya vile zilikuwa wazi kabisa. Alisomesha kati ya watoto wenye akili ambao mtaa wetu ulibarikiwa kuwa nao. Lakini sikuendelea kumuheshimisha mzee wangu kama alivyokuwa akitaka na hii ilikuwa ni baada ya kuwafahamu wasichana. Taratibu kama mwendo wa kinyonga mambo yalianza kuharibika. Bahati iliyokuwa mbaya kabisa ni kuwa yalihariba kwa taratibu pasina kutoa onyo wala ishara yoyote ile kwangu.

Ndio maana siku zote huwasisitizia watu kuwa unapoambiwa na wengine kuhusu mabadiliko ya kitu fulani kwako wasikilize na jitathimini. Kwa sababu ni ngumu kwako wewe kuweza kung'amua mabadiliko yanayotokea kwako. Ikiwa utapata nafasi ya kuyatambua basi nafasi ya kuyarekebesha inakuwa haipo tena. Kwangu mabadiliko yalianza katika ratiba yangu ya kwenda shule, nilikwenda shule kwa mda niliotaka.

Hata nilipofika shuleni pia sikuwa najishughulisha na lengo mama la mwanafunzi shuleni, kujifunza!. Badala yake nilitumia wakati mwingi kutafuta na kumchambua ni binti gani ambaye angenasa haraka kwenye mtego wangu. Maisha yakaenda hivyo na kwa kuwa sikuwa na yeyote aliyeyatambua kwa mapema mabadiliko yale, wazazi waliwiwa na uzito wa majukumu ya familia. Maendeleo yangu shuleni yakaanza kudorola taratibu na sikupata nafasi ya kung'amua.
 
Oya mkuu naomba nikushauri. Usitumie nguvu nyingi kufikisha ujumbe!! Tunajuwa ulikuwa kiwembe kwenye uandishi wa INSHA, yani kwa lugha nyepesi ww ndio miongoni mwa wanafunzi wazuri kwenye masomo ya Art.
Tafadhali nenda tu kwenye stori moja kwa moja ili wasomaji tuburudike, tukupe like za kutosha, bila kusahau kwenye story yoyote wakosowaji hawakosi. Nadhali nimeeleweka.🙏🙏
 
#02

Jahazi lilizidiwa kabisa shehena na kuzama nikiwa kidato cha nne. Wimbi la pepo la ngono likaniandama na kunifanya niwe mraibu kwani nisingeweza kupitisha wiki sijalala na mwanafunzi wenzangu au binti wa makamo yangu. Hali hiyo ikashamiri huku mtu wa kukemea wala hakutokea na matokeo yake binti mmoja kati ya wengi niliyeshiri naye tendo la ndoa akashika mimba. Hatukuwa tunasoma naye binti yule yeye alikuwa akisoma katika shule binafsi.

Nilipatana naye mara baada ya shule yetu kuomba kushindana na shule yao katika mchezo wa mpira wa miguu. Wakati wengine wakifika pale kwa dhumuni la kutizama kandanda mimi kama ilivyokawaida yangu nilifika pale na kuanza kufanya tathimini zangu za nani ambaye angenasa kwenye mtego wangu kwa urahisi. Baada ya pekua pekua ya hapa na pale ndipo nikakutana na binti yule aliyekuwa na hulka ya ukimya kiasi na upole wa sura yake ulinivutia zaidi.

Kwa ushawishi wangu ambao ulikuwa wa kilaghai nikafanikisha kumtia mtegeni kwa siku ile ile. Mapenzi yetu yakaanza huku yakistawishwa na ngono zembe tuliyoifanya kila mara tulipokutana. Utamu wa mchezo ule ukatukolea na mara nyingine binti yule hakufika shuleni ili aje nyumbani. Au angewahi kutoka shuleni ili apite nyumbani kwanza kabla ya kwenda kwao. Masomo aliyaweka pembeni licha ya kwao kuweza kugharamia elimu iliyo na gharama.

Nakumbuka vyema kuwa taarifa ya ujauzito wa binti yule niliipata nikiwa kwenye mitihani ya nusu muhula mwezi wa sita mwaka 2014. Mimi nilikuwa kidato cha nne huku binti akiwa kidato cha tatu. Nikafanya mtihani wa muhula japo nilikuwa na mawazo mno na niliishia kupata alama za namba za viatu kwa sababu hakuna somo nilivuka arobaini. Mtihani wa muhula huu ulimshangaza kila mtu shuleni juu ya anguko langu kwani zile alama hazikuwahi kuwapo huko nyuma. Ila maisha yakaendelea vyema japo wasi wasi haukuniondoka kwa kuwa nilihisi wakati wowote ule taarifa ya mimba ya Amina ingefahamika.

Mwezi wa saba mwaka huo huo wa 2014 ndipo hali ya hewa rasmi ikachafuka. Hiyo ilikuwa ni baada ya wazazi wake na Amina kugundua kuwa binti yao yu mjamzito. Tumbo lilikuwa si la kuficha tena kwa kuwa ukubwa wake ulimuumbua na mabadiliko kadhaa aliyoyaonyesha. Baada ya kipigo kitakatifu jina langu likatajwa kama muhisika wa ujauzito ule. Haikuishia kwenye jina tu bali mpaka sehemu ambayo tulifanyia ushenzi ule ikatajwa, nyumbani kwetu!.
 
#03

Nikiwa nafanya usafi wa ufagiaji wa kiwanja cha nyumbani kwa kuwa palikuwa mlimani na niliweza kuwaona wote walikuwa na safari za kuja nyumbani kabla hawajafika. Nikaona kuna kakikundi fulani ambako jazba ilijaa vifuani mwao, ilikuwa ni rahisi kugundua na haikuitaji akili za ziada. Mwendo wao pekee ulionesha ni kwa kiwango gani walikuwa wamekwazika.

Japo Amina hakuwepo ila mama yake alifanya nikawagundua kwa urahisi kwa sababu alifanana mno na Amina mwenyewe, mama yule alijizaa kwa bintiye. Kengele ya hatari ikagonga kichwani mwangu kwa sababu sikuwaona wazazi wa Amina pekee bali wanaume wengine wawili. Wanaume wale kwa aiba zao nilifahamu fika walikuwa watumishi katika jeshi la polisi. Sikutaka kuendelea kupoteza wakati pale mara baada ya kuwa nimepata hakika ya mashaka yangu.

Mbio zangu mwisho wake ulikuwa alipokuwa amepanga kaka yangu, umbali kidogo toka ilipokuwa nyumba yetu. Bahati ikaangukia kwangu nilimkuta akiwa yupo nyumbani hivyo hima nikamuelezea ujio wangu na namna ninavyoihisi hatari. Kwa kuwa mkasa mzima juu ya mimba ya Amina nilikuwa nimekwisha mueleza. Ikanibidi aniache kwake ili yeye aende nyumbani kufahamu ni nini kilikuwa kikiendelea.

Aliponiacha pale moyo ulikuwa unapiga kwa kasi huku jasho jepesi likiambaa ambaa usoni. Mkono nayo haikuwa nyuma ilikuwa ikitetemeka kwa kiasi ambacho sikuwahi kuona. Kila mda nilikuwa nikichungulia nje ili kujihakikishia usalama wangu isije kuwa watu wale wamenifuata mpaka kule. Woga ulitawala mwilini mwangu na uso ukasawajika vilivyo huku ile kauli ya mavi kugonga chupi na kurudi nikiithibitisha. Kuwa waswahili walikuwa hawaongopi waliposema kuhusu hilo.

Hakuna siku niliyataja majina ya Mungu yote tena pasipo kukosea kwenye sala kama siku hii. Kama saa likakatika toka kaka Rweyunga ameondoka na sasa ndio alikuwa akirejea. Majibu yake ni kama waliwasha moto mwingine juu ya ule uliokuwa tayari umewaka. Yaani alikuja na petroli kutaka kuuzima moto. Kaka alianza kwa kuniambia kuwa wale walikuwa wazazi wa Amina kweli na walikuja pale nyumbani kwa ajili ya kunikamata ili wanifikishe kwenye vyombo vya sheria.

Huko ningeweza kujibu vyema tuhuma zilizokuwa zikinikabili, wala hawakutaka suluhu kwa namna yoyote ile. Mbaya zaidi ukiachana na hayo ni kuwa mama naye alikuwa upande wa watesi wangu. Yaani hakutaka kuiona sura yangu tena ikikanyaga viunga vya nyumbani pale. Huku akimpa kaka onyo la kuwa kama ningeenda pale nyumbani basi ndio ingekuwa tiketi yangu ya jela. Pia hakakana kabisa kuwa na mtoto kama mimi ambaye nilihifedhehesha familia.

Tumaini langu pekee likabaki kwa kaka yangu ambaye aliniachia ziwa ila kutokana na ushawishi wa nyumbani nikaanza kuona mabadiliko. Huduma za chakula zikapungua kwani ilikuwa milo mitatu ikawa miwili tena kwa shida wakati mwingine nisipate chochote. Ikaja kwenye hasira za mara kwa mara ambazo sikuwahi kumuona nazo kabla, kosa kidogo tu angelalama kwa usiku mzima.

Hali hiyo ikatoa taarifa ya kuwa hakufukuzae hakwambii toka bali viashiria. Alishaonyesha kila dalili ya kutonihitaji kwake kwa sababu nilikuwa msalaba uliomchosha kuubeba na alikuwa tayari kuutua. Ila tu namna ya kuniambia kuwa anihitaji ndio hakuwa nayo, soni ilimshika kila mara alipotaka kufanya hivyo. Sikutaka kuendelea kuwa mzigo wake wakati nilikuwa mtu mzima. Pia matatizo niliyatafuta mwenyewe hivyo pekee mimi ndie niliyetakiwa kuwajibika. Sio kuwasumbua wengine kwa makosa yangu.

Mpango wa kutoroka ukajengeka kichwani kwangu ila shida ilikuwa ni pesa. Ningetorokaje pasina kuwa na pesa hata ya nauli tu, sikutaka kuendelea kuwepo pale kwa kaka kwani niliona angeweza hata kuniuza kwa dau dogo kwa wale wanaonitafuta. Nikategea mpaka siku kaka amepata mshahara kutoka kwa waajili wake kampuni fulani ya ulinzi. Pesa ambayo uhingia kama mshahara ilikuwa ni 250,000. Katika pesa hiyo mimi nikachukua 50,000 na majira ya alfajiri na mapema nikafika kwenye kivuko cha Kamanga.

Sikuwa na begi zaidi ya mfuko wa plasitiki maarufu kama rambo. Ndani yake kukiwa na suruali mbili pamoja na tisheti moja zote mali ya kaka. Hatukuwa tumeachana mwili hivyo na nilichukua hizo kwa kuwa nguo zangu na vitu vyangu vingine vilikuwa viko nyumbani. Kulingana na taarifa niliyopewa na kaka sikutakiwa kufika nyumbani labda kama nilihitaji tiketi ya kwenda jela. Nilimfahamu mama fika hakuwa mwanamke wa kupindua maamuzi yake pindi anapoamua.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom