Maisha ni mafupi?

foroy

Senior Member
May 2, 2018
186
288
Kuna huu msemo maarufu wenye mantiki na dhana iliyojengwa katika kutojipa tabu kwa kujali mambo yasiyo ya lazima; maisha yenyewe mafupi!

Life is too short...wazungu pia wanautumia.

Kwa uzoefu wangu matumizi ya msemo huu yamekuwa maarufu zaidi katika muktadha wa aina tatu :-

1) NEEMA: Mara nyingi katika nyakati za heri na ridhiko la nafsi, yaani siha njema, uchumi imara na mazingira rafiki, watu wengi hurejea huu msemo. Katika kula na kunywa, anasa na tafrija, utasikia ikisemwa; maisha yenyewe yako wapi? Piga pombe, au kula nyama...maisha yenyewe mafupi!

2) VIFO: Katika mazingira ya vifo hususan vile vya ghafla na visivyotarajiwa, watu wengi huukumbuka pia usemi huu, hasa baada ya kushtushwa na taarifa hizo. Lo! Kweli maisha mafupi, Kanumba kafariki?

3) MIGOGORO: Katika mazingira ya migogoro na sonono, msemo huu hukumbukwa sana. Maisha yenyewe mafupi, achana naye! Usijipe stress...usiwaze sana...usilishikilie, nk.

Lakini yanapotokea mabadiliko katika mazingira hayo, labda afya kuzorota, uchumi kuyumba na dhiki nyinginezo, huu msemo huwa hautumiki na unasahaulika.

Ndipo linakuja swali, je maisha ni mafupi kweli? Kipimo cha urefu na ufupi wa maisha ni kipi? Maisha ni mafupi kutoka wapi kwenda wapi? Maana kupima urefu wa kitu ni lazima iwe kutoka point moja kwenye nyingine.

Ukweli ni kwamba maisha sio marefu wala si mafupi. Urefu au ufupi wa maisha ni dhana mtambuka na tafsiri yake inategemea mtazamo, hisia na maoni binafsi (subjective).

Siku za binadamu duniani zinaweza kuwa chache kwa namba, lakini hilo halihusiani na urefu au ufupi wa maisha yake. Kwasababu tafsiri ya maisha ipo katika JUMLA ya kile ulichokiishi katika siku za uhai wako.

Kuna watu walifariki dunia wakiwa na umri mdogo lakini wameacha historia kubwa kwa waliyoyafanya na kuyaacha duniani.

Na wapo walioishi miaka mingi sana, lakini hakuna cha maana walichofanya. Na wamefariki bila kuacha lolote la kukumbukwa.

Muigizaji Steven Kanumba alifariki akiwa na umri mdogo wa miaka 28, lakini ameacha alama isiyofutika katika tasnia ya filamu Tanzania. Jina lake linaimbwa mpaka kesho. Mastaa wengi wanaotamba Tanzania ni zao la Kanumba.

Tupac Amaru Shakur, rapa wa Kimarekani alifariki akiwa na umri wa miaka 25 tu baada ya risasi kusitisha uhai wake mnamo 13 September 1996. Mpaka leo Tupac ndiye mwanamuziki wa hiphop mwenye heshima na ushawishi zaidi katika historia ya muziki huo ulimwenguni.

Kile alichokifanya ndani ya hiyo miaka 25 ndiyo maisha halisi ya maisha Tupac. Jina la Tupac limeendelea kuishi mpaka leo, na litaendelea kudumu kizazi na kizazi. Kwa tuliomfuatilia Tupac tangu enzi hizo, bado tunamuona kama Icon na role model. Ni kwa sababu ya kile alichokiishi.

Ipo hivyo kwa kina Bob Marley, Patrice Lumumba, Samora Machel, Malcom X na wengineo.

_________

Maisha ya binadamu ni mfano wa dakika tisini za soka. Mashabiki wa timu iliyofungwa huona muda unakimbia kama mwizi, na wanaoongoza huona kama saa imesimama na wanatamani referee amalize mchezo.

Mtu mwenye hali ngumu ya kimaisha, anaona siku haziendi. Na katu hawezi kusema maisha yenyewe mafupi. Maana siku moja ya mateso ni ndefu kuliko wiki.

Maisha huonekana mafupi ukiwa kwenye mazingira ya starehe kama vile kitambaa cheupe, bambalaga, kidimbwi, and the like. Lakini usiku wa mtu aliyelala njaa nyumbani ni mrefu kuliko usiku wa mtu aliyezingirwa na watoto warembo, wakila bata pale Wavuvi Camp!

Aliyefungwa jela, huwezi kumwambia maisha ni mafupi akakuelewa. Kwa vile siku moja ya gerezani ni zaidi ya masaa ishirini na nne ya uraiani.

Kuna wazee wanatamani warudie ujana, kwa sababu walitumia vibaya fursa na wakati wao. Na hili ni somo kuwa hata ukiishi miaka mia mbili duniani, kama hukutimiza wajibu wako na kutumia vizuri fursa ulizopata, ipo siku utajutia uzee wako huku ukitamani siku zirudi nyuma.

Hapo nidipo utagundua kuwa maisha sio mafupi bali yanatosha. Kinachotakiwa ni kuyaishi kikamilifu (full responsibly); simaanishi kwa ukamilifu (perfectly).

Kuyaishi maisha kikamilifu ni kutumia ipasavyo fursa zipatikanazo ndani ya siku za uhai wako. Fursa za kiroho, za kiuchumi na hata kijamii:-

Kula na kunywa kile unachokipenda na unachomudu kukipata.

Ishi na watu vizuri.

Furahia maisha kwa kutembelea ndugu na jamaa. Maisha ni watu.

Fanya ibada mara nyingi iwezekanavyo.

Tembelea maeneo yanayokuvutia kama fukwe, viwanja vya michezo, mbuga za wanyama na maeneo ya starehe unayomudu kuyafikia.

Fanya kazi kwa bidii na malengo kwa mujibu wa fursa zilizopo na uwezo ulionao.

Fanya jambo la maendeleo kwa ajili yako na wanaokutegemea kwa kadiri ya uwezo wako.

Wasaidie na kuwafariji wenye shida na changamoto mbalimbali za maisha kwa kadiri ya nafasi na uwezo wako.

Huzunika inapobidi, omboleza na waombolezao, omba radhi ukikosea...

Timiza wajibu wako.

Maisha ya binadamu ni kama kupwa na kujaa. Siku zako zitakapofika ukingoni na uhai kukoma, utakuwa umeyaishi maisha yako kikamilifu bila kujali umri uliofikia.

Machozi ya huzuni kwa waliobaki hai yataambatana na tabasamu la faraja kwa kumbukumbu maridhawa utakazowaachia. Kimwili utakuwa mbali, kiroho utaendelea kuishi nao.

Maisha sio mafupi, yaishi kikamilifu.
Screenshot_20231018-161318.jpg
 
Sijausoma huu waraka wako wote. Maisha ni mafupi NDIO, Hapo ulipo hujui baada ya nusu saa kitatokea nini. Kitendo cha mwanadamu kuzaliwa tu tayarii shida anazo(nature)

Binadamu maisha yake yote yametawaliwa na shida, hivyo bahati inapotekea ya kufuruhia maisha usiache, furaha kwa mwanadamu ni kama umeme unakuja na kutoweka.

Mpaka sasa sijui kusudi la sisi kuwepo kwenye hii sayari.
 
Sijausoma huu waraka wako wote. Maisha ni mafupi NDIO, Hapo ulipo hujui baada ya nusu saa kitatokea nini. Kitendo cha mwanadamu kuzaliwa tu tayarii shida anazo(nature)

Binadamu maisha yake yote yametawaliwa na shida, hivyo bahati inapotekea ya kufuruhia maisha usiache, furaha kwa mwanadamu ni kama umeme unakuja na kutoweka.

Mpaka sasa sijui kusudi la sisi kuwepo kwenye hii sayari.
Kwa hivyo chochote usichokijua hatima yake ni kifupi? Ndo tafsiri yako?
 
Back
Top Bottom