serengeti2014
Member
- Aug 4, 2014
- 9
- 1
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mwezi Juni, 2016, vijana idadi 14,000 waliohitimu kidato cha sita mwaka huu walijiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria. Vijana hawa walimaliza mkataba wao wa miezi mitatu mwanzoni mwa mwezi Septemba, 2016.
Wizara ya Ulinzi na JKT inapenda kutoa taarifa kwa vijana wote waliomaliza kidato cha sita mwezi Mei, 2016 na ambao hawajajiunga na vyuo vya elimu ya Juu, wakaripoti katika makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa utaratibu ambao Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa ataelekeza.
Aidha, mwezi Mei na Juni mwaka huu, Jeshi la Kujenga Taifa liliwafanyia usaili vijana wa kujiunga na mafunzo ya JKT kwa kujitolea. Usaili huo ulifanyika kwa kushirikiana na kamati ya Ulinzi na usalama kuanzia ngazi za Wilaya hadi Mikoa. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inapenda kuwatangazia vijana wote waliosailiwa mwezi Juni, 2016 kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa kwa kujitolea, waripoti kwenye Makambi waliopangiwa ifikapo tarehe 01 Desemba, 2016 kwa nauli zao.
Ili kufanikisha zoezi hili kwa ufanisi, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imemtaka Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa kutekeleza yafuatayo kabla ya tarehe 01 Desemba, 2016:-
- Kufufua kambi ya Makuyuni JKT ili iwe miongoni mwa kambi zitakazotoa mafunzo kwa vijana wa JKT kuanzia mwezi Desemba, 2016. Hivyo shughuli zote zinafanyika hapo Kambini kama vile shule, Kilimo, ufugaji n.k. ziondolewe mara moja.
- Kambi ya Luwa na Milundikwa zilizoko Mkoa wa Rukwa, zirejeshwe kwa shughuli za JKT za kilimo na ufugaji.
- Kambi ya Mpwapwa nayo irejeshwe kwa ajili ya kuendesha mafunzo ya kilimo na ufugaji ndani ya Jeshi la Kujenga Taifa.
Imetolewa:-
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini(GCU)
WIZARA YA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA