kbm
JF-Expert Member
- Oct 5, 2012
- 5,224
- 1,676
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Chama cha Wafanyakazi Madereva wa Malori Tanzania (Chawamata), kimetoa wito wa kukutana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ili kumfikishia malalamiko ya posho ndogo wanazolipwa kwa safari za ndani na nje ya nchi.
Malipo yaliyopendekezwa katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Usafiri na Usafirishaji chini ya Mwenyekiti Hawa Wenga, ni Sh. 32,250 kwa siku kwa safari za ndani na dola 25 kwa safari za nje.
Katibu wa Chamawata, Greyson Wimile, katika kikao kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam na kuwakutanisha madereva hao, alisema Januari 7, mwaka huu, walimpelekea barua Waziri Mkuu malalamiko yao ili atatue.
Alisema barua hiyo iliambatana na orodha ya majina 763 ya madereva ambao hawakubaliani na posho wanayolipwa kwa siku.
Wimile alisema mapendekezo yao ni kulipwa sh. 70,000 kwa safari za ndani na dola 75 kwa safari za nje ya nchi bila kujali aina mzigo alioubeba dereva.
"Dereva anayesafiri nje ya nchi kulipwa dola 15 kwa malori yanayibeba ' dry cargo' na dola 25 wanaobeba mafuta kwa siku ni ndogo haikidhi mahitaji kukingana na kazi," alisema Wimile.
Alisema malipo ya dereva kwa safari za ndani anayeendesha malori yanayobeba 'dry cargo' kulipwa sh. 32,250 na malori ya mafuta ni sh. 53, 750 kwa siku, hayakuzingatia kwa makusudi maazimio ya kikao cha Oktoba 13, mwaka jana.
Alisema dereva, kulingana na aina ya mzigo anaobeba, anastahili kulipwa sh. 70,000 kwa siku na dola 75 kwa siku safari za nje.
Mmoja wa madereva hao, Dominic Lyaro, alisema madereva huchangia uchumi wa nchi kwa asilimia kubwa, hivyo madai hayo yashughulikiwe mapema.
"Kasi ya serikali hii tunaitaka na kwetu. Kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu (mstaafu) Mizengo Pinda, haikuwa na maana, hivyo tunamtaka Majaliwa atumbue majipu haya," alisema Lyaro.
Madereva wa malori nchini wameilalamikia serikali kwa muda mrefu kwa kutosimamia kuwapo kwa malipo yanayokidhi mahitaji yao na kusababisha migomo ya mara kwa mara.
CHANZO: NIPASHE