Madaraka Nyerere, hazina ambayo haijatumika

britanicca

JF-Expert Member
May 20, 2015
15,636
30,004
3c2aa513e65161146e42ce3bdf280bfa.jpg

Jina la Madaraka Nyerere(pichani) sio geni miongoni mwa watanzania. Ukiachilia mbali ukweli kwamba yeye ni mtoto wa sita wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (kitu ambacho bila shaka kinampa automatic celebrity status), yeye pia ni mwandishi, mfanyabiashara na mtu ambaye huwa hasiti kuelezea hisia zake kuhusu mambo mbalimbali iwe ni katika nyanja za kisiasa, kijamii na hata kiuchumi kila mara fursa ya kufanya hivyo inapojitokeza. Mwaka juzi mwezi wa nne (April) yeye na Jaffar Amin (mtoto wa Iddi Amin-Rais wa zamani wa Uganda) waliingia katika vitabu vya kumbukumbu vya wapenda amani duniani walipokutana kwa mara ya kwanza ikiwa ni ishara ya amani na usuluhisho barani Afrika na kwingineko.

Hivi karibuni nilipata nafasi ya kuzungumza naye kuhusu mambo kadhaa yakiwemo ya kifamilia na pia kupata maoni yake kuhusu mambo mbalimbali. Je,ni kwanini mpaka leo hii hajajiingiza katika masuala ya siasa au uongozi? Anamuelezeaje Hayati Baba wa Taifa kama baba yake na kama kiongozi? Ana ushauri gani kwa wapiga kura katika mwaka huu wa uchaguzi? Ana mtizamo gani kuhusu viongozi mbalimbali ambao hupenda kumuenzi Baba wa Taifa kwa maneno huku vitendo vyao vikiwa tofauti kabisa? Unataka kujua kwanini alipewa jina la “Madaraka”? Ana ushauri gani kwa vijana kuhusu suala zima la kujiletea maendeleo?

Fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo;

BC: Madaraka, asante sana kwa kukubali kufanya nami mahojiano haya. Kwa faida ya wale ambao hawawajui watoto wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, nyumbani kwenu mmezaliwa watoto wangapi na wewe ulizaliwa lini ,ukasomea wapi na kukulia wapi?

MADARAKA NYERERE: Tuko watoto nane. Mimi wa sita. Nimesoma shule
zifuatazo:
-Shule za msingi: Bunge, Forodhani, Arusha School, Isike (Tabora), Tarime.
-Sekondari: Mzizima, na Tambaza (Dar)
-Post-secondary: Shinyanga Commercial Institute
-Vyuo: Finafrica College (Milan, Italy); Algonquin College (Ottawa, Canada)
BC: Turudishe kidogo wakati wa utoto wako.Ni kitu au tukio gani unalolikumbuka zaidi kuhusu utoto wako?Na ulikuwa na ndoto za kufanya kazi gani utakapokua?

MADARAKA NYERERE: Sina tukio lolote kubwa ninalokumbuka la utotoni. Nahisi baada ya kuanza masomo ya biashara kuanzia kidato cha tatu, tayari nilianza kuwa na mawazo ya kuwa mfanyabiashara. Kabla ya hapo, sikumbuki kama nilikuwa na ndoto za kufanya kazi nyingine.

BC: Uliwahi kuelezwa kwanini ulipozaliwa ulipewa jina la Madaraka? Ilikuwaje kukua kama mtoto wa Rais au katika mazingira ya Ikulu na mambo kama hayo?

MADARAKA NYERERE: Nilipewa jina hilo kwa sababu nilizaliwa kabla ya Uhuru, 1960, wakati mamlaka ya utawala yalianza kukabidhiwa kwa wazalendo kwa ajili ya kujiandaa kwa Uhuru. Wakati huo iliundwa Serikali ya Madaraka, na ndiyo nikapewa hilo jina. Tuliishi iliyopo Ikulu ya sasa kwa muda wa miaka michache baada ya Uhuru, lakini kwenye miaka ya katikati ya sitini, tulihamia Msasani. Mazingira ya kuishi Ikulu na Msasani hayakuwa na utofauti sana na jamii tuliyokuwa tunaiona kila siku tukienda shule, au tuliyotembela nje ya mazingira ya nyumbani, zaidi ya kwamba yalikuwa ni makazi ya rais na yalilindwa na askari. Lakini hao walikuwa ni walinzi wa rais, na sisi hatukuwa na walinzi wowote. Lakini naamini hili ndiyo hali ilivyo hata mpaka sasa hivi kwa familia ya Rais, kuacha mke wa Rais.

BC: Pamoja na masuala ya uandishi,unajishughulisha na kazi zipi zingine?Je,na wewe ni mkulima kama alivyokuwa Hayati Baba wa Taifa?

MADARAKA NYERERE: Shughuli kubwa ninayofanya sasa hivi ni kuweka jitihada katika kutangaza Kijiji cha Butiama kama eneo la kumbukumbu inayomhusu Mwalimu Nyerere kwa kuwa ni sehemu aliyozaliwa, na ni sehemu ambayo amezikwa. Ninafanya jitihada pia ya kukusanya kumbukumbu zinazomhusu yeye. Najihusisha pia na kuendeleza utalii wa utamaduni katika kanda ya Ziwa, kwa mikoa ya Kagera, Mwanza, na Mara. Aidha, kila mwaka (tangu 2008), hupanda Mlima Kilimanjaro kuchangisha pesa za hisani kusaidia masuala mbali mbali.

BC: Wewe ni mtu unayefuatilia kwa karibu masuala ya mila na desturi. Nimekusoma mara kwa mara ukielezea habari mbalimbali za kimila na kitamaduni hususani za kabila lenu la Wazanaki. Sasa kwa upande mwingine, vijana wengi wa siku hizi hawataki sana kusikia au kuzingatia masuala ya mila na tamaduni.Wanadai mambo hayo yamepitwa na wakati.Unasemaje kuhusu mtazamo huo wa vijana?

MADARAKA NYERERE: Jamii yoyote isiyoweka jitihada ya kulinda na kudumisha utamaduni wake inatoa fursa kwa tamaduni nyingine kuchukuwa nafasi na kuweka ushawishi katika mawazo ya vijana wake. Mimi naamini kuwa kushabikia tamaduni nyingine kuna hatari ya kutufanya tusiwe na misimamo thabiti ya kutetea yale ambayo yanaweza kuwa na manufaa kwetu. Ukishakuwa huna utamaduni wa kutetea, unakuwa tayari kupokea lolote linalokuja toka kwenye tamaduni nyingine, na siyo yote yanayotoka nje yana manufaa kwetu. Hao vijana ambao wanaona kuwa utamaduni umepitwa na wakati watakuwa tayari wamekumbwa na hilo tatizo. Madaraka Nyerere(mtoto) akimuangalia baba yake, Mwalimu Nyerere, akipiga ngoma.

BC: Umewahi kuandika mahali kwamba mara nyingi watu hutegemea kwamba mtoto wa mwanasiasa, tena wa mwanasiasa mashuhuri na maarufu kama Mwalimu, na yeye atakuwa mwanasiasa. Kwa bahati nzuri au mbaya wewe mpaka hivi sasa umejiweka pembeni kidogo na siasa. Unaweza kuniambia sababu zako za msingi hasa za kutojishirikisha na siasa kama ambavyo watu wengi wangetegemea?

MADARAKA NYERERE: Tatizo kubwa ninaloliona kwenye siasa za Tanzania ni kuwa kuna utaratibu wa kutokuelezana ukweli, hata kama yule anayepaswa kuelezwa ukweli anafanya mambo ambayo yanakiuka maadili ya uongozi, au yanapingana na azma ya kuleta maendeleo kwa watu, na wakati mwingine kuwa hata ni mambo ambayo yanahatarisha maslahi ya vizazi vijavyo.

Ukisema ukweli, unajenga uhasama na viongozi wenzako. Siamini kama maendeleo yanaweza kuja bila kukubali utaratibu ambao Mwalimu Nyerere aliuzungumzia wa “kujisahihisha.” Na mtawezaje kusahihishana kama hamuelezani ukweli?

Inawezekana binadamu wengi tuko hivyo, yaani hatupendi kukosoa wenzetu mara kwa mara. Na mimi sidhani kama niko tofauti sana, isipokuwa najifahamu vizuri kuwa naweza kujizuwia kusema jambo kwa muda mrefu, lakini kuna wakati lile ambalo nimelikalia kwa muda mrefu litatoka tu, halafu nitajenga uhasama na viongozi wenzangu, iwapo nimeingia kwenye uongozi.

BC: Katika utafiti wangu wakati naandaa maswali kwa mahojiano haya,nimegundua kwamba wewe ni mpenzi mzuri wa muziki. Kitu ambacho sikuweza kugundua ni aina ya muziki uipendayo, wanamuziki uwapendao .Unaweza kunitatulia kiu yangu ya kujua vitu hivyo?

MADARAKA NYERERE: Ni kweli napenda muziki, lakini siwezi kusema kuwa ni muziki wa aina moja tu ambao napenda; napenda miziki ya aina nyingi. Mimi naamini kuwa ukisikiliza muziki wowote kwa muda, utasikia kitu kinachopendeza tu. Miziki mingi ambayo naipenda ni ya zamani. Kwa hiyo kwa upande wa Tanzania nasikiliza sana Zilipendwa, na pia Zilipendwa za Congo ya kina Rochereau, na Lwambo. Lakini hata baadhi ya miziki ya kizazi kipya ya Tanzania napenda kusikiliza. Kwa kipindi kisicho cha zamani sana napenda sana miziki ya Orchestra Maquiz du Zaire, Dk Remmy Ongala, na baadhi ya miziki ya Mlimani Park Orchestra. Kwa nje, napenda miziki ya UB40 na Bob Marley, na wanamuziki wengine kama Ray Charles na Stevie Wonder.

BC: Tukiwa bado kwenye suala hilo hilo la muziki,kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika sanaa ya muziki nchini Tanzania.Kulikuwa na miziki ambayo leo hii tunaiita “zilipendwa” , kukawa na mfumuko mkali sana wa miziki ya ki-Congo na hivi sasa tunayo Bongo Fleva au muziki wa kizazi kipya. Nini mtazamo wako katika safari hii ya mabadiliko?Ungependa labda kutoa ushauri gani kwa wanamuziki vijana wa leo?

MADARAKA NYERERE: Mabadiliko makubwa ya mzuiki wa sasa yanasukumwa na teknolojia. Nakubaliana na msimamo ambao alitoa Waziri Ally hivi karibuni, mwanamuziki wa bendi ya Njenje ambao aliutoa kwenye mahojiano, kuwa tukiendelea na mtindo huu, baada ya muda si mrefu (yeye alisema miaka kumi), hatutakuwa na wanamuziki tena hapa Tanzania. Wanamuziki wengi wa sasa, wana uwezo wa kuandika mashairi tu, lakini hawana uwezo wa kupanga mpangilio wa ala kwa sababu hawajajifunza muziki. Kuendeleza muziki kunahitaji kusomea muziki (kusoma na kuandika muziki) pamoja na kujifunza kupiga ala. Ushauri kwangu kwa wanamuziki vijana ni waanze kusomea muziki.

BC: Umeshatembelea nchi kadhaa ulimwenguni zikiwemo nyingi za barani Afrika.Kwa uzoefu wako kutokana na safari hizo,unadhani bara la Afrika linakabiliwa na changamoto zipi ambazo zinafanana kutoka nchi mpaka nchi na unaweza kutoa ushauri gani katika mbinu au njia za kukabiliana na changamoto hizo?

MADARAKA NYERERE: Changamoto zinafanana kwenye nchi nyingi. Kukuwa kwa umasikini kutokana na wakazi wengi wa nchi hizi kuendelea kuishi maisha duni kutokana na uwezo mdogo wa Serikali zao kuleta mabadiliko katika maisha yao, au kutokana na uongozi mbovu, au kutokana na sera zisizozingatia mahitaji ya wengi. Utegemezi ni kikwazo kikubwa cha kuleta mabadiliko na maendeleo kwa wananchi; utegemezi wa sera, wa fikra na wa nyenzo za kuleta maendeleo. Kwa kuwa tuna utegemezi wa sera, hata zile rasilimali ambazo tunazo na ambazo zingetusaidia kupunguza kuomba omba, tunazibinafsisha kwa kufuata sera za wengine na matokeo yake tunajipunguzia uwezo wa kujitegemea.
Sioni njia ya kujikwamua na changamoto hizi kwa kuendelea kuwa wategemezi.

BC: Umepanda Mlima Kilimanjaro mara kadhaa sasa(kama sikosei mara mbili). Ingawa wewe umepanda mlima kwa sababu za NGO, Utalii wa ndani. Ungemshauri nini mtu ambaye leo hii anapanga au anatamani kupanda Mlima Kilimanjaro?Zaidi ungemshauri nini katika maandalizi ya kuupanda mlima huo?

MADARAKA NYERERE: Ingawa kupanda Mlim Kilimanjaro siyo gharama ndogo kwa Watanzania waliyo wengi, ni jambo ambalo nashauri wote wenye uwezo (wa fedha) wajaribu hata kwa mara moja. Fedha peke yake haziwezi kukufikisha kileleni, kwa sababu hata Bilionea Abramovich hakuweza kufika kileleni alipojaribu kupanda Kilimanjaro.

Hata hivyo, kwa mtu anayekusudia kufika kileleni, inahitaji kufanya mazoezi ya kuongezea mwili uwezo wa kuhimili kutembea kati ya saa 6 – 8 kila siku kwa kati ya siku 6 hadi 8. Zaidi, ni uwezo wa kufanya hivyo katika mazingira ambayo hewa ya oksijeni inapungua kadri unavyozidi kupanda juu kutoka usawa wa bahari.
Zoezi lolote linaloongeza ‘fitness’ linasaidia. Inahitaji kufanya mazoezi hayo kwa muda usiyopungua miezi mitatu. Pia ni muhimu kufanya mazoezi ya kutembea (kama ni nje, au kwenye ‘treadmill’) kwa muda mrefu (labda mara moja kwa juma).Jambo kuu linalosababisha wengi kushindwa kufika kileleni ni uwezo mdogo wa mwili kuhimili upungufu wa oksijeni, mpandaji anavyozidi kukaribia kileleni. Hata hivyo, njia ambayo nimekuwa naitumia mimi (Lemosho route) inasaidia sana kuuzoesha mwili hali ya kuwa mlimani na kuhimili upungufu huo wa hewa safi.
Jambo la mwisho muhimu ni kuwa na ari ya kufanikiwa; kutokubali kushindwa.
Madaraka Nyerere(kulia) akiwa katika kilele cha Mlima Kilimanjaro.Mwenzake ni Gerald Hando,mtangazaji wa Clouds FM

BC: Kwa muda sasa umekuwa ukiandika masuala kadha wa kadha katika blog yako.Nini kilikuvutia katika kuanzisha blog?Unazungumziaje zana hizi mpya za habari na mawasiliano? Je,kwa mtazamo wako,watanzania tunazitumia ipasavyo katika kupashana habari na kuwasiliana?

MADARAKA NYERERE: Sababu kubwa iliyonisukuma kuanzisha ‘blog’ ni kuhabarisha yale ambayo nafikiri yanaweza kuwa ya manufaa kwa wengine, au yanayofurahisha kwa namna fulani. Pia, nakusudia kuwa mwandishi katika siku za usoni (labda wa vitabu), na nilisoma mahali kuwa kila mwandishi anahitaji kujitangaza kupitia njia hii. Naamini ‘blog’ ni zana nzuri ambayo inampa kila mtu fursa ya kusema lile ambalo lipo kichwani mwake.

Kwa maana nyingine, inapanua wigo wa kupata mawazo mbadala ambayo hayatolewi kwa kuzingatia vizingiti ambavyo vinaweza kukabili baadhi ya vyombo vya habari. Hata hivyo, kuna baadhi ya Watanzania wanatumia ‘blog’ kuandika maoni au habari ambazo zinakiuka maadili ya uandishi, na badala ya kuwa jambo zuri linakuwa jambo ambalo linaleta athari kwa wale wanaoandikwa vibaya. Madaraka Nyerere (kulia) akiwa na Jaffar Amin walipokutana mjini Musoma mwaka jana.Ukitaka kusoma alichoandika Madaraka kuhusu mkutano huo, bonyeza hapa .

BC: Mengi yameshaandikwa kuhusu historia ya Mwalimu Julius Nyerere. Lakini mpaka hivi leo bado hakuna Biography ya Mwalimu ambayo imeandikwa aidha na yeye mwenyewe au mtu wa karibu sana na Mwalimu. Mtu kama wewe hivi. Je, unadhani kwanini mpaka leo hakuna biography ya Mwalimu?Una mpango wowote wa kuandika kitu kama hicho?

MADARAKA NYERERE: Nafikiri kuandika kitabu juu ya maisha ya Mwalimu ni kazi ambayo siyo rahisi iwapo kusudio ni kukiandika kwa ukamilifu, kwa sababu maisha yake yamegusa maeneo mengi ya historia, siyo ya Tanzania tu bali hata ya baadhi ya nchi za Afrika, hasa wakati wa harakati za vita vya ukombozi wa nchi hizo zilizoshirikisha pia mchango mkubwa wa Tanzania. Labda ugumu huo ndiyo unasababisha kuwa hakijaandikwa mpaka sasa.
Sijui kama nina uwezo wa kufanya hivyo peke yangu, lakini nadhani ni jambo ambalo napswa kulitafakari.

BC: Kama mtoto wa Rais,umepitia mambo mengi, kuona mengi. Kwa maneno yako mwenyewe, unamuelezeaje baba yako? Au tuseme Mwalimu Nyerere tuliyekuwa tunamuona kwenye majukwaa ya siasa alikuwa ana tofauti gani anapokuwa nyumbani?

MADARAKA NYERERE: Ni swali zuri. Sisiti kusema kuwa Mwalimu aliyesimama jukwaani hakuwa anafanya maigizo; alikuwa ni mtu yule yule ambaye aliporudi nyumbani. Maadili yale aliyoyazingatia katika uongozi wake, aliyaishi pia.

BC: Huu ni mwaka wa uchaguzi. Hivi sasa kampeni mbalimbali za kisiasa ndio zimeshamiri.Nikikupa nafasi ya kumsaidia mwananchi wa kawaida katika uamuzi wake wa kumchagua kiongozi bora ungemwambia nini mwananchi huyo?

MADARAKA NYERERE: Mimi naamini kila mpiga kura anaweza kuamua ni kiongozi gani atamfaa katika uongozi kwa kuangalia mazingira anayoishi, mahitaji yake, na kuangalia sera ambazo anaamini zitaleta mabadiliko katika maisha yake, na mwisho kuchagua yule mgombea ambaye anaamini atakabili changamoto ambazo zitaleta maendeleo kwake. Tatizo ni kuwa inawezekana kabisa kuwa hata wale wagombea watakaojitokeza hawatakuwa wamefikia kiwango ambacho mpiga kura anatarajia kutoka kwa kiongozi wake.

BC: Chaguzi za kisiasa nchini Tanzania huenda sambamba na kutajwa sana kwa jina la Hayati Baba wa Taifa.Takribani kila kiongozi hujaribu kujihusisha na jina lake kwa namna moja au nyingine huku wengi wakijinadi kwamba wanamuenzi Baba wa Taifa kwa jambo moja au mawili.Unaongeleaje suala au tabia hizo za wanasiasa?

MADARAKA NYERERE: Kila mwanasiasa analenga kujenga umati wa watu ambao watamkubali na kumpigia kura. Naamini kuwa bado mpaka sasa hivi, kuna wapiga kura wengi wanaamini kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa ni kiongozi ambaye alikusudia kwa dhati kuleta maendeleo kwa Watanzania wote. Kwa hiyo, si ajabu kuona kuwa wapo viongozi ambao wanao msimamo huo huo kuhusu Mwalimu Nyerere na wanasema hivyo wakati wa kupiga kampeni ili wapate kukubaliwa na baadhi ya wapiga kura. Hata hivyo, si ajabu kuwa wapo viongozi wengine ambao watakaojitokeza kusema wanamuenzi Mwalimu Nyerere wakati wanayofanya ni tofauti kabisa na yale aliyoyasimamia Mwalimu. Huu ni utapeli. Sio lazima kukubaliana na kila kitu Mwalimu Nyerere alichosimamia. Kiongozi wa kweli ni yule ambaye ataonyesha msimamo wake waziwazi, na siyo kutoa picha kuwa ni wa aina moja kumbe wa aina nyingine.

BC: Nimeona katika blog yako mara kadhaa umekuwa ukiwakaribisha wageni wanaotaka au wanaokuwa wamekuja kuona kaburi la Hayati Mwalimu Nyerere.Je,kuna utaratibu maalum ambao sharti mtu aufuate endapo anataka kuja kuliona kaburi?

MADARAKA NYERERE: Kila mtu yuko huru kutembelea Butiama. Haihitaji kupata ruhusa yoyote. Anapofika Butiama anaweza kutembelea Makumbusho ya Mwalimu Nyerere, kaburi lake, na baadhi ya nyumba zake. Kwa anayehitaji maelezo zaidi, anaweza kuwasiliana nami kwa barua pepe kupitia:
madaraka.nyerere@gmail.com

BC: Una ushauri gani kwa vijana wa ki-Tanzania katika suala zima la kujiletea maendeleo yao binafsi na pia ya taifa?

MADARAKA NYERERE: Narudia maneno ambayo Mwalimu aliyasema kuwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa ni muhimu sana. Maarifa ya leo hii yanajumuisha matumizi makubwa ya teknolojia zinaozohusiana na kazi na changamoto zinazotukabili.
Serikali ina jukumu la kuweka mazingira mazuri pia ili wale waliyokuwa tayari kufanya kazi ili kuleta mabadiliko kwenye maisha yao waweze kufanya hivyo kwa mafanikio. Lakini, kazi na maarifa peke yake haitoshi kwa sababu hata yale mazingira ambayo Serikali itaweka yatahusisha sera na mfumo ambao Serikali inaona ndiyo unafaa kwa wakati huo.
Swali kubwa ambalo wakati wote linahitaji majibu ni: sera zinazosisitiza soko zaidi ya jamii zinaweza kuleta maisha bora kwa kila mtu kwa mafanikio zaidi kuliko sera ambazo zinaweka mkazo kwenye masuala ya jamii?
Baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa sera za soko ambazo zimekuwa kama dini duniani kote zimeleta umasikini kwa watu wengi zaidi duniani, ingawa zimefanikiwa kutajirisha watu wachache kwa kiwango cha juu sana.
Vijana waache kuwa walalamikaji kuhusu Serikali na viongozi wao, na waanze kuchukuwa jukumu la kuhakikisha kuwa maamuzi yanayofanywa na Serikali na viongozi wao yataleta manufaa kwa wote, na kwa vizazi vijavyo.

BC: Wewe na mke wako mna watoto wangapi? Majina yao?
MADARAKA NYERERE: Tuna watoto watatu: Julius, Julia, na Helena.
BC: Madaraka,shukrani sana.Nakutakia kila la kheri katika kazi zako

Huyu kamanda angepata kama fursa ya kuwa kiongozi katika sekta yeyote angechangia sana kuleta maendeleo.
 
Mkuu Buritanica, kiukweli hii story ya Madaraka ni mzuri sana na Tanzania tuna hazina kubwa mfano nani alitegemea huyu kijana Kato aliyelelewa nyumbani kwa Mzee Machalila angekuwa hapa alipo? . Naomba historia yake, au nijulishe tuu juu ya ukoo wa Mzee Machalila niwatafute, historia nitaipata mwenyewe! .
Pasco
 
Mkuu Buritanica, kiukweli hii story ya Madaraka ni mzuri sana na Tanzania tuna hazina kubwa mfano nani alitegemea huyu kijana Kato aliyelelewa nyumbani kwa Mzee Machalila angekuwa hapa alipo? . Naomba historia yake, au nijulishe tuu juu ya ukoo wa Mzee Machalila niwatafute, historia nitaipata mwenyewe! .
Pasco

Wewe na huyo Kato wako mpaka kieleweke. Ila ili ukamilishe historia hiyo ya hapo alipofikia ni lazima uwapate pia Benard M na Eddo L ndio itafanya ulichoandika kikamilike kwa vijana wetu watakao soma maandishi yako baadae.
Sikiliza wimbo wa Professor J unaitwa Zali la Mentali kwa ajili ya nukuu ndogo ndogo
 
Mkuu Buritanica, kiukweli hii story ya Madaraka ni mzuri sana na Tanzania tuna hazina kubwa mfano nani alitegemea huyu kijana Kato aliyelelewa nyumbani kwa Mzee Machalila angekuwa hapa alipo? . Naomba historia yake, au nijulishe tuu juu ya ukoo wa Mzee Machalila niwatafute, historia nitaipata mwenyewe! .
Pasco
Pasco story ya machalila ntakupa ila kuwa na subira
 
Wewe na huyo Kato wako mpaka kieleweke. Ila ili ukamilishe historia hiyo ya hapo alipofikia ni lazima uwapate pia Benard M na Eddo L ndio itafanya ulichoandika kikamilike kwa vijana wetu watakao soma maandishi yako baadae.
Sikiliza wimbo wa Professor J unaitwa Zali la Mentali kwa ajili ya nukuu ndogo ndogo
Ila akae style ya kupokea full story ya KATO babu yake mzaliwa wa karagwe , wakahamia Chato , baba akaoa mkerewe, wakaishi kwa wazinza, wakati wa kampein KATO alijua akitangaza anatokea kule ni ngumu kujinadi, ilibidi aamie kwenye kabila la wengi kwa muda ili azidake kura zote kwa kuwaingiza Kingi wakidhani ni kabila lao, kumbe ni mnyambo asilia
 
Heading imekaa kipambe mno.

Hazina???

Kama hayo maelezo ndiyo yana-define uhazina wake then hii nchi ina hazina nyingi tu so hakuna upekee wowote alionao mpaka iwe gumzo.
 
Tunadeal na the Top only.
Original ancestors wa Juli ni Mtusi!
Original ancestors wa Benya ni Nchumbiji!
Original ancestors wa Yoani ni Banyamulenge! .

Cha muhimu sio ancestors kwa sababu hatutafuti tambiko Lao bali wote ni Watanzania ila ukweli usemwe! .

Pasco
 
Tunadeal na the Top only.
Original ancestors wa Juli ni Mtusi!
Original ancestors wa Benya ni Nchumbiji!
Original ancestors wa Yoani ni Banyamulenge! .

Cha muhimu sio ancestors kwa sababu hatutafuti tambiko Lao bali wote ni Watanzania ila ukweli usemwe! .

Pasco
Kwahiyo unataka kusemaje? Hehehe hata nyerere alikuwa mnyarwanda unalijua Ili? Yaan zanaki angalia chimbuko lao, pia hata wanyambo ni chimbuko la wanyarwanda + waganda+ warundi waliooana na wahaya, wakapatikana wanyambo
 
HUWA NAJIULIZA MARA KWA MARA NA SIPATI JIBU.

HIVI HUU UKOO WA NYERERE NA KAWAWA HAUNAGA WASOMI NA VIJANA WENYE UWEZO WA KUWA VIONGOZI HATA UKUU WA WILAYA ACHANA NA MKOA AU WAZIRI KATIKA NCHI HII?

HATA KAMA SI FADHILA JE UWEZO TU HAWANA KABISA KWELI? TUNAONA BAADHI YA VIJANA AMBAO WAZAZI WAO WALIWAHI KUWA VIONGOZI WETU NA UWEZO WAO NI WA KUTILIA MASHAKA WAKITEULIWA KWENYE NYADHIFA ZA KIUONGOZI/KIUTAWALA LAKINI KWA HAWA WAZEE HATUSIKII KITU. TATIZO NI NINI HASA?

WANAJAMVI MNAWEZA KUWA NA MAJIBU
________________________________________________________________________________________________
KWA SASA KUIAMINI CHADEMA HAIHITAJI AKILI, HEKIMA, BUSARA NA MAARIFA BALI KICHWA, MDOMO NA PUA: BY M2020
 
Mkuu Buritanica, kiukweli hii story ya Madaraka ni mzuri sana na Tanzania tuna hazina kubwa mfano nani alitegemea huyu kijana Kato aliyelelewa nyumbani kwa Mzee Machalila angekuwa hapa alipo? . Naomba historia yake, au nijulishe tuu juu ya ukoo wa Mzee Machalila niwatafute, historia nitaipata mwenyewe! .
Pasco
Kato ndo nani mkuu? Huyu wa kutojaribiwa au?
 
Back
Top Bottom