Serikali ya China imeweka chini ya ulinzi vipuri nyeti vya ndege ya kivita ya Marekani ya F-35 baada ya shehena iliyotokea nchini Australia kuelekezwa kimakosa hadi Hong Kong.
Tukio hili limezua hofu kubwa za kiusalama na uchunguzi wa bunge nchini Washington kuhusu uwezekano wa China kufikia teknolojia hiyo ya siri ya kijeshi.
Shehena hiyo iliyokuwa na kifuniko cha chumba cha rubani na mlango wa sehemu ya kuhifadhia silaha kutoka kwenye ndege ya jeshi la anga la Australia, ilisafirishwa mwishoni mwa mwezi Mei 2026.
Lengo lilikuwa ni kuvifikisha vipuri hivyo nchini Marekani kwa ajili ya matengenezo na ukaguzi kupitia kampuni ya usafirishaji ya UPS kwa niaba ya mkandarasi Lockheed Martin.
Hata hivyo, baada ya ndege hiyo kuwasili kituo kisichotarajiwa nchini Korea Kusini, ilielekezwa Hong Kong ambako maofisa wa China walivikamata vipuri hivyo, na mpaka sasa havijarudishwa.
Sehemu zote mbili za vipuli vilizokamatwa zimepakwa mchanganyiko maalum wa rangi za siri zinaofyonza miale ya rada ili kuifanya ndege hiyo isionekane kwa urahisi, jambo linalozidisha wasiwasi wa kiintelijensia kwamba China inaweza kuvifanyia utafiti wa kisayansi ili kunakili teknolojia hiyo.
Wakati maofisa wa usalama wa Marekani wakionyesha wasiwasi mkubwa na kuanzisha uchunguzi wa kina kuhusu udhaifu wa ugavi wa kijeshi, Waziri wa Ulinzi wa Australia, Richard Marles, amepunguza ukubwa wa athari hizo akidai kuwa vipuri hivyo vilikuwa vimeharibika na haviwezi kutumiwa kirahisi kwa madhumuni ya kijeshi.
Kampuni hiyo ya usafirishaji inaripotiwa kuwa hapo awali ilishirikiana na kampuni iliyowekwa kwenye orodha nyeusi kwa kuhusishwa kuwa na mawasilano na jeshi la China.