Baada ya miaka saba ya maumivu, kusubiri, na vita vikali vya kisheria ng'ambo ya bahari, hatimaye familia 32 za Kenya zilizopoteza wapendwa wao katika ajali ya ndege ya Ethiopian Airlines (ET302) zimepata afueni ya kisheria.
Kampuni ya utengenezaji wa ndege ya Boeing itatoa jumla ya dola milioni 87.36, zaidi ya shilingi za kitanzania bilioni 230, kama malipo mapya ya fidia kwa familia hizo zilizoathirika ambapo Kenya ina idadi kubwa ya wahanga katika ajali hiyo.
Katika mpango huu mpya, kila familia inatarajiwa kupokea dola milioni 2.73, ambayo sawa na shilingi za Kitanzania bilioni 7.17
Ajali hiyo ya kihistoria ilitokea mnamo Machi 10, 2019, ambapo ndege hiyo ilianguka dakika 06 tu baada ya kupaa kutoka Addis Ababa kuelekea jijini Nairobi.
Tukio hilo liligharimu maisha ya watu wote 157 waliokuwemo ndani, huku Kenya ikipoteza raia wengi zaidi kuliko nchi nyingine yoyote kati ya mataifa 30 yaliyohusika.
Ingawa hakuna kiasi cha fedha kinachoweza kurudisha uhai wa waliopotea, ushindi huu katika mahakama za Marekani umekuja baada ya Boeing kupatikana na hatia ya kuwapotosha wadhibiti wa usalama wa anga, hatua iliyozipa familia hizo hadhi ya kisheria kama waathiriwa wa uhalifu wa jinai na kufungua njia ya kupata haki yao.