Mada maalum ya ndege toka FB

Kiwanja cha Ndege cha Mtemere kilichopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Nyerere mkoani Pwani kusini mwa Tanzania kimefanyiwa maboresho makubwa ya miundombinu na sasa kina uwezo wa kupokea ndege zaidi na kwa usalama mwaka mzima.

Uwanja huu ndio mlango mkuu wa anga kwa watalii wanaofika Nyerere kwa ndege kutoka Dar es Salaam, Zanzibar na Arusha.

Katika maboresho hayo hivi karibuni, njia ya kurukia na kutua ndege yenye urefu wa kilomita 1.8 imewekewa teknolojia mpya ya Lami yenye polima "Hard Polymer Surface"

Teknolojia hiyo imetumia rangi ya udongo mwekundu ili kuendana na mazingira ya asili ya hifadhi na pia kuzuia uchafuzi. Faida nyingine ni kuimarisha udongo ili ndege ziweze kutua na kuruka salama katika majira yote, ikiwemo kipindi cha masika ambacho hapo awali uwanja ulifungwa kutokana na matope.

Pamoja na njia kuu ya ndege, uwanja umeongezeewa barabara ya usalama yenye urefu wa mita 300, eneo la kusimama dharura la mita 60, na eneo wazi la usalama la mita 300.

Kwa sasa maboresho hayo yameruhusu uwanja kupokea ndege ndogo na za ukubwa wa kati zenye uwezo wa kubeba hadi abiria 100. Katika hatua hiyo, hivi karibuni uwanja umepokea ndege ya aina ya Dash-8-300 kutoka shirika la ndege la Air Tanzania.

Maboresho haya yanatarajiwa kuongeza urahisi wa usafiri wa watalii kwenda Nyerere na kuifanya hifadhi hiyo kuwa kivutio kinachopatikana kwa urahisi zaidi wakati wote wa mwaka.

 
Taja kaulimbiu au Wito unaokuvutia zaidi kutoka katika mashirika haya ya ndege:

Air Congo - "𝙏𝙝𝙚 𝙃𝙤𝙥𝙚 𝙤𝙛 𝘼𝙛𝙧𝙞𝙘𝙖"
RwandAir - "𝙁𝙡𝙮 𝙩𝙝𝙚 𝙙𝙧𝙚𝙖𝙢 𝙤𝙛 𝘼𝙛𝙧𝙞𝙘𝙖"
Kenya Airways - "𝙏𝙝𝙚 𝙥𝙧𝙞𝙙𝙚 𝙤𝙛 𝘼𝙛𝙧𝙞𝙘𝙖"
Air Tanzania - "𝙒𝙞𝙣𝙜𝙨 𝙤𝙛 𝙆𝙞𝙡𝙞𝙢𝙖𝙣𝙟𝙖𝙧𝙤"
Ethiopian Airlines - "𝙏𝙝𝙚 𝙣𝙚𝙬 𝙨𝙥𝙞𝙧𝙞𝙩 𝙤𝙛 𝘼𝙛𝙧𝙞𝙘𝙖"
Uganda Airlines - "𝙁𝙡𝙮 𝙩𝙝𝙚 𝘾𝙧𝙖𝙣𝙚 𝙩𝙤 𝙩𝙝𝙚 𝙋𝙚𝙖𝙧𝙡 𝙤𝙛 𝘼𝙛𝙧𝙞𝙘𝙖"
 
Shirika la ndege la Jambojet litarejesha safari zake za kila siku kati ya Nairobi na Entebbe kuanzia Oktoba 1, 2026, baada ya kusitisha huduma hiyo kwa muda wa miaka sita.

Hatua hii inalenga kukidhi mahitaji yanayokua ya usafiri, utalii, na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki, ambapo huduma hiyo itajumuisha usafirishaji wa abiria pamoja na mizigo.

Safari hizo zitatumia ndege aina ya De Havilland Canada Dash 8-400, na safari hiyo inatarajiwa kuchukua takriban saa moja na dakika 15.

Nauli ya kwenda upande mmoja itaanza karibu Dola 170 za Kimarekani, ambayo ni takriban Shilingi za Kenya 22,000.

Aidha, abiria wanaotokea Uganda watapata fursa ya kuunganisha safari zao kuelekea maeneo mbalimbali ya pwani ya Kenya kama Mombasa, Diani, Malindi, na Lamu kupitia mtandao wa ndani wa Jambojet.

Shirika hilo linakadiria kusafirisha takriban abiria 300,000 kati ya nchi hizo mbili ifikapo mwishoni mwa mwaka 2026.
 
Ushirikiano wa kihistoria kati ya Urusi na China katika kuunda ndege kubwa ya abiria ya CR929 ulisambaratika rasmi kutokana na mgongano mkubwa wa kimkakati, vikwazo vya kimataifa, na kutosimama upande mmoja kimaslahi.

Mradi huo uliolenga kutoa ushindani dhidi ya kampuni kubwa za Boeing na Airbus ulianza kuingia doa kufuatia vita vya Ukraine mwaka 2022, vilivyosababisha Urusi kuwekewa vikwazo vikali vya kiuchumi.

China, kupitia kampuni yake ya COMAC, ilihofia kuwa kuendelea kushirikiana karibu na Urusi kungeweka rehani uwezekano wa ndege hiyo kukubalika kimataifa na kupata vipuri muhimu kutoka nchi za Magharibi.

Tofauti kubwa ya kifikra ilijitokeza kwenye uteuzi wa teknolojia, ambapo China ilitaka kutumia injini na mifumo ya kisasa kutoka kampuni za Kimagharibi kama General Electric ili kurahisisha mauzo ya nje, wakati Urusi ilishikilia msimamo wa kutumia teknolojia zao za ndani ili kujikinga na shinikizo za kisiasa.

Mbali na hayo, nchi hizi mbili zilishindwa kukubaliana kiwango cha ugawaji wa faida na masoko, huku kukiwa na mzozo wa chini kwa chini wa kutoaminiana kiufundi ambapo Urusi ilisita kukabidhi siri zake kuu za kihandisi na muundo wa ndege kwa China.

Hatimaye, ushirikiano huo ulivunjika na kuifanya China kuondoa herufi "R" iliyowakilisha Urusi na kuupa mradi huo jina jipya la C929 (Awali C-929) ikiendelea nayo peke yake, huku Urusi ikijitenga na kuelekeza nguvu zake zote katika kufanya marekebisho ya ndani kwenye mradi wake wa ndege ya MC-21 kwa kutumia injini na vifaa vya asilimia mia moja vya nyumbani.
 
OUAGADOUGOU - Jeshi la Anga la Burkina Faso limeongoza mafunzo ya kipekee kwa vijana katika Kambi ya Kizalendo ya Camp Vacances Faso Mêbo 2026.

Katika mafunzo hayo, watoto waliovalia sare za kijeshi walipata fursa ya kuketi ndani ya helikopta ya kisasa ya Airbus H125 Écureuil namba BF2219 iliyofungwa silaha ya mashine kwa ajili ya ulinzi.

Pia walipewa mafunzo ya jinsi ya kutumia mtambo wa Kichina wa kudhibiti ndege zisizo na rubani "anti-drone jammer gun" unaotumika kudhibiti na kudondosha 'drone' za kijasusi katika operesheni.

Rais wa Mpito, Kapteni Ibrahim Traoré, ndiye mwenye msimamo wa mpango huu unaotekelezwa kupitia Initiative présidentielle Faso Mêbo.

Traoré amesema lengo ni kuwajenga vijana kwa nidhamu, uzalendo na ufahamu wa teknolojia ya anga na ulinzi, ili kuwa nguzo ya usalama wa taifa linalokabili vitisho vya kigaidi.

Mafunzo hayo yanachanganya vipengele vya ndege za kijeshi, helikopta na mifumo ya kukabiliana na ndege zisizo na rubani ili kuwapa kizazi kipya taswira halisi ya majukumu ya Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Burkina Faso FDS.
 
WASHINGTON, D.C. - Anga ya Washington D.C. lilijaa kishindo cha kihistoria wakati ndege ya Rais wa Marekani, "Air Force One", ikipita juu ya jengo la Capitol ikiambatana na ndege za kijeshi zilizosindikiza, na kuzindua rasmi mashindano ya kwanza ya magari ya NTT INDYCAR SERIES "Freedom 250 Grand Prix".

Safari hiyo maalum ya angani ilifanyika kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 250 ya uhuru wa Marekani. Ndege ya Rais ikiwa katikati na ndege za kivita pembeni ziliruka kwa mpangilio juu ya alama kuu za kitaifa kabla ya magari kuanza kushindana chini.

Mashindano haya ya kipekee yanafanyika kwenye mzunguko wa barabarani wenye urefu wa maili 1.7 na kona 7, unaopita karibu na Ikulu ya Marekani na Mnara wa Washington.

Madereva wanatakiwa kukamilisha mizunguko 147 ili kufikia umbali wa maili 250, huku magari yakitarajiwa kufikia kasi ya zaidi ya kilomita 290 kwa saa kwenye barabara ya Pennsylvania Avenue.

Ni mara ya kwanza kwa mashindano ya IndyCar kufanyika katikati mwa jiji kuu la Marekani, na tukio hilo limevutia mamilioni ya watazamaji ndani na nje ya nchi.
 
Mnamo Agosti 24, 2001, ndege ya Air Transat Flight 236 ya aina ya Airbus A330 ilikuwa ikisafiri kutoka Toronto, Canada kwenda Lisbon, Ureno, ambapo ikiwa angani ilizima injini zote mbili katikati ya Bahari ya Atlantic kutokana na kuvuja kwa mafuta hali iliyosababishwa na makosa ya kiufundi.

Marubani wa ndege hiyo walifanikiwa kuiongoza ndege hiyo bila nguvu ya injini kwa umbali wa kilomita 100 kutoka kimo cha futi 34,000 na kutua salama katika uwanja wa kijeshi wa Lajes huko Azores.

Ushujaa na ujuzi wa marubani, ulipelekea watu wote 306 waliokuwa kwenye ndege hiyo kunusurika, na tukio hilo lilirekodiwa kama safari ndefu zaidi ya ndege ya abiria kuteleza angani bila nguvu ya injini katika historia ya usafiri wa anga.
 
Televisheni ya Taifa ya Irani mnamo Agosti 22, 2026, ilipeperusha matangazo maalum yakionesha mtandao mkubwa wa mahandaki mapya ya siri chini ya ardhi, ambayo sasa yanatumika kama viwanda vya kimkakati vya kuzalisha na kuhifadhi mamia ya ndege zisizo na rubani maarufu kama "Drone" na makombora ya masafa marefu.

Katika video hiyo iliyonaswa chini ya milima mirefu, Mkuu wa Majeshi ya Irani Meja Jenerali Ali Abdollahi, anaonekana akikagua mistari ya uzalishaji wa ndege zisizo na rubani za kisasa za kujitoa mhanga na zile za ujasusi.

Vituo hivi vipya vimejengwa mita mamia chini ya ardhi ili kuhakikisha uzalishaji huo hauathiriwi na mashambulizi ya anga au mifumo ya rada za kigeni baada ya migogoro ya hivi karibuni kikanda.

Ndegenyuki hizo zimeundwa kubeba vilipuzi vizito kwa ajili ya kugonga shabaha kwa usahihi, zikiwa zimepangwa kwenye majukwaa maalumu ya kurushwa moja kwa moja kutoka chini ya ardhi huku zikiwa zimefungwa teknolojia mpya ya vita vya kielektroniki ili kukabiliana na mifumo ya ulinzi wa anga ya adui.

Mkuu wa Majeshi alisisitiza kuwa kasi ya uzalishaji wa zana hizo za kujitoa mhanga imeongezeka mara tatu zaidi chini ya mkakati wao wa "Miji ya Droni na Makombora" ili kuonesha kuwa miundombinu yao ya kijeshi bado inafanya kazi kikamilifu.
 
Uamuzi wa Mkurugenzi wa CIA, John Ratcliffe, wa kuacha kutumia ndege ya kawaida ya kidiplomasia aina ya C-40B na badala yake kusafiri kwenda Moscow kwa kutumia ndege kubwa ya kijeshi ya mizigo aina ya C-17 Globemaster III unatajwa kama ishara kubwa ya mabadiliko ya kiusalama na kimkakati.

Ndege ya C-40B, ambayo kwa kawaida hutumiwa na viongozi wakuu wa serikali kwa safari za kiofisi, hutoa faraja na mazingira ya kawaida ya kidiplomasia, lakini haina uwezo mkubwa wa kubeba mizigo mizito wala kutoa ulinzi maalum wa kijeshi unaohitajika kwenye mazingira yenye ushindani mkubwa.

Kubadilisha kwenda kwenye C-17, ambayo ni ndege ya kimkakati ya usafirishaji wa vifaa vya kivita, kuliruhusu msafara huo kubeba mifumo thabiti zaidi ya mawasiliano ya siri, vifaa vya kiufundi vya kujihami, na uwezekano wa magari yenye ulinzi wa ziada kwa ajili ya operesheni hiyo ya siri nchini Urusi.

Hatua hii haikuashiria tu uzito na dharura ya misheni hiyo huko Moscow, bali pia ilionyesha jinsi CIA ilivyoweka kipaumbele usalama wa hali ya juu na uwezo wa kiufundi badala ya itifaki za kawaida za usafiri wa viongozi.

Mabadiliko haya ya ghafla ya aina ya usafiri yanathibitisha kuwa safari hiyo haikuwa ya kidiplomasia tu, bali ilikuwa ni operesheni maalumu ya kiintelijensia iliyohitaji zana nzito za kiulinzi ambazo zingeweza tu kubebwa na ndege ya mizigo ya jeshi la anga.

Chanzo:
Simple flying
 
Operesheni Almasi ya mwaka 1966 ilikuwa hatua ya kijasusi ya Mossad iliyofanikiwa kuiba ndege ya kisasa ya kivita kwa wakati huo aina ya MiG-21 kutoka Iraq kupitia rubani Munir Redfa, ikiiwezesha Israel na washirika wake kusoma teknolojia ya Kisovieti (Sasa Urusi baada ya kuvunjika muungano huo)

Mossad ilimshawishi Redfa kwa kumpa dola milioni moja na usalama wa familia yake, ambayo ilitoroshwa kisiri kutoka Iraq kabla ya kufanya safari hiyo ya hatari.

Rubani huyo alitoroka wakati wa mazoezi ya kijeshi na kurusha ndege hiyo hadi uwanja wa jeshi la anga wa Hatzor nchini Israel.

Tukio hili lilipa Israel faida kubwa ya kijeshi, ikiwa ni pamoja na uwezo wa kudungua ndege sita za Syria kwa siku moja na kupata ushindi mkubwa katika Vita vya Siku Sita.

Baadaye, Israel iliiazima ndege hiyo kwa Marekani chini ya mpango wa "HAVE DOUGHNUT", hatua iliyosaidia wahandisi wa Kimarekani kuboresha mbinu zao za kivita dhidi ya teknolojia ya Kisovieti wakati wa Vita Baridi.
 
MONTREAL — Mfanyakazi mmoja wa kampuni ya huduma za ardhini Samsic Airport amefariki dunia tarehe 24 Agosti 2026 baada ya kugongwa na ndege ya French Bee aina ya Airbus A350 iliyokuwa ikirudi nyuma katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Montreal-Trudeau (YUL).

Tukio hilo lilitokea wakati wa mchakato wa pushback wa ndege.

Bodi ya Uchunguzi wa Usalama wa Usafiri wa Kanada (TSB) imesema uchunguzi kuhusu ajali hiyo unaendelea.

Ni tukio lingine linalozidisha maswali juu ya usalama wa wafanyakazi wa ardhini viwanja vya ndege duniani.
 
Uamuzi wa kufunga mifumo ya ulinzi wa makombora kwenye ndege za mizigo za FedEx ulitokana na tishio kubwa la makombora yanayorushwa kutoka begani maarufu kama MANPAD yanayolenga ndege zinazopaa au kutua maeneo yenye migogoro.

Kichocheo kikuu kilikuwa shambulio la mwaka 2003 huko Baghdad, ambapo ndege ya mizigo ya DHL ilipigwa na kombora lakini ikafanikiwa kutua kwa dharura.

Tukio hili lilionyesha kuwa ndege za kiraia ziko hatarini, ikapelekea Idara ya Usalama wa Ndani ya Marekani kuzindua mradi wa majaribio ambapo FedEx ikawa ya kwanza kushiriki kwa kufunga mfumo wa ulinzi wa Guardian kati ya mwaka 2006 na 2008.

Mfumo huu unatumia teknolojia ya mwanga ya infrared (laser) kugundua kombora linaporushwa na kulifuatilia kwa kasi kubwa.

Kisha, hurusha mwanga mkali wa 'laser' unaolipofusha kombora na kulivuruga uwezo wake wa kufuata joto la injini za ndege, na kulifanya likose lengo.

Ingawa majaribio ya awali yalimalizika, FedEx imekuwa ikiomba vibali vipya vya kuweka mifumo ya kisasa zaidi ya leza ili kulinda marubani na shehena zake, huku ikiepuka kubadili njia za safari za kimataifa ambako kunaweza kuongeza matumizi makubwa ya mafuta na muda.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…