Kwa mujibu wa mtandao wa airlinepilotcentral, mapato ya marubani katika mashirika makubwa 05 ya Marekani mwaka 2026 yanaendelea kupanda kutokana na mazungumzo ya vyama vya wafanyakazi, ongezeko la mahitaji ya marubani wenye uzoefu, na mipango ya kisasa ya ndege baada ya janga la Corona.
Mashirika hayo ni American Airlines, United Airlines, Delta Air Lines, Southwest Airlines na Alaska Airlines. Mishahara huhesabiwa kwa saa za kuruka na hutegemea aina ya ndege, cheo cha rubani na muda wake kazini.
Ndege za kubeba abiria wengi za masafa marefu kama Boeing 777 na Airbus A350 zinalipa zaidi ikilinganishwa na ndege za masafa mafupi kama Boeing 737.
Kwa American Airlines, rubani mpya msaidizi (FO) anaanza kwa dola 116 kwa saa (zidisha mara kiwango cha kubadilisha fedha leo Tanzania) kwenye ndege za Boeing 737 na Boeing 777, huku akifika hadi dola 246 kwa saa akiwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 15. Nahodha kwenye Boeing 777 anaweza kufika hadi dola 447 kwa saa.
Mashirika ya ndege ya United na Delta yana viwango karibu sawa. FO mpya anapata dola 125 kwa saa na anaweza kufika dola 265 kwa saa.
Nahodha mzoefu wa Boeing 777 anafika hadi dola 483 kwa saa.
Delta pia inawapaarubani wake mgao wa asilimia 10 kutoka faida ya shirika kila mwaka.
Shirika la ndege la Southwest linajitofautisha kwa kutumia ndege za Boeing737 pekee.
Hapo FO mpya anaanza kwa dola 145 kwa saa na anaweza kufika dola 276, huku nahodha akifika hadi dola 394.
Shirika limesema hadi 2028 mishahara itapanda zaidi.
Shirika la ndege la Alaska Airlines nalo linalipa FO mpya dola 124 kwa saa na nahodha mzoefu dola 375.
Kuanzia mwezi Septemba 2026 mishahara yake itapanda kwa takriban dola 10 hadi 15.
Cha pekee kwa Alaska ni kwamba rubani anafika kiwango cha juu cha mshahara akiwa na miaka 11 tu, wakati mingine inachukua miaka 12 hadi 15.
Kwa ujumla ukubwa na uzoefu (seniority) ndio kitu muhimu zaidi katika tasnia hii. Kadri rubani anavyokaa muda mrefu kwenye shirika ndivyo mshahara wake unavyopanda, na ndiyo maana mapato yanaweza kutofautiana sana hata ndani ya shirika moja.