Thomas Salme, raia wa Sweden, alifanya kazi kama rubani wa ndege za abiria za kibiashara kwa zaidi ya miaka 10 kwa kutumia hati za kughushi za urubani.
Salme alianza kazi yake mwaka 1997 na kampuni ya ndege ya Italia Air One kama rubani msaidizi, na baadaye akawa nahodha wa ndege za Boeing 737 akikusanya zaidi ya saa za ndege 10,000 na kusafirisha maelfu ya abiria bila kusababisha tukio au ajali.
Hata hivyo, mpango wake uligunduliwa Machi 2010 wakati mamlaka za Uholanzi zilipopokea taarifa kuhusu hitilafu katika rekodi zake za leseni.
Salma alikamatwa akijiandaa kurusha katika ndege ya Corendon Airlines na baadaye kukiri kosa lake.
Mahakama ya Uholanzi ilimpa adhabu ya faini na kifungo jela kwa kosa la udanganyifu na kurusha ndege bila leseni halali.
Katika Kisa kingine....
William Chandler, rubani mkuu wa ndege wa shirika la ndege la Afrika Kusini (SAA), aliruka kwa zaidi ya miaka 20 kabla ya udanganyifu wake kugunduliwa mwishoni mwa 2018.
Chandler alikuwa na leseni halali ya urubani wa kibiashara (CPL), ambayo ilimruhusu kuruka, lakini alighushi leseni kubwa ya urubani wa usafiri wa anga (ATPL) - Leseni yaa kiwango cha juu kinachohitajika kwa safari za kimataifa za masafa marefu.
Inatajwa kuwa, Chandler alikataa kupandishwa cheo kuwa nahodha kwa miaka mingi kwa sababu jukumu hilo lingemhitaji kuwasilisha cheti chake cha ATPL (kilichoghushiwa) kwa uthibitishaji.
Hata hivyo udanganyifu huo uligunduliwa kufuatia "tukio la kuripotiwa" wakati wa safari kutoka Johannesburg kwenda Frankfurt mnamo Novemba 2018, ambapo ndege ilifanya "kona za ajabu" baada ya kukutana na misukosuko juu ya Milima ya Alps ya Uswisi.
Chandler alijiuzulu mapema 2019 mara tu uchunguzi ulipoanza.
SAA iliwasilisha mashtaka ya uhalifu kwa kosa la udanganyifu na kujaribu kupata milioni za mshahara na posho zilizolipwa kwake kwa njia ya udanganyifu.