1.Nilikuwa sijui kuwa mtu anaweza kula sukari kwa kuilamba hadi asubuhi, hadi siku nilipojikuta kitu pekee kilichopo geto ni sukari tuu. Hakuna gesi wala majani, hiyo ni saa tano usiku.
2.Nilikuwa sijui kama jagi la umeme linawezakupikia wali na mtu ukala fresh tuu. Nina mchele tuu ndani, sina gesi, sina vocha, sina hata mia mbovu mfukoni.
3.Nilikuwa sijui kama mtu yeyote anawezakuwa fundi. Nilijikuta nimekuwa fundi mzuri tuu baada ya kukaa mtaani miaka 7 baada ya kuhitimu chuo.
Hapo nilikuwa nimeshahudhuria saili kadhaa DUCE na baadae zikahamishiwa Dodoma nikawa naona matangazo ya kazi tuu lakini siombi kwasababu hata nikiitwa usahili dodoma sina nauli.
Mwanamke niliyezaa nae mtoto wa kwanza akanikimbia na mtoto ila nikapata wa kunifaa na mwenye maono, tukajichanga tukakodi fremu baada ya mama mmoja kutuamini na kutuachia vitendea kazi vya grocery na jiko kufuatia kuhamia dodoma kumfuata mumewe kikazi. Hapo vinywaji kreti mbili mchanganyo. Nikitoka kwenye ufundi nawashawishi wenzangu tunakuja kujipooza kwenye grocery yangu. Akiwa mjamzito akanisihi niende dodoma kwenye kazi niliyoitwa usahili ila nikakataa sina pesa na kichwa kilishasahau yote ya chuoni hivyo nikupoteza tuu pesa maana sitoboi. Miaka saba mtaani siyo mchezo. Alipokea pesa wenyewe wanaita ya mchezo, akanikabidhi niende tuu maana tulioitwa usahili ni wachache hivyo kuna uwezekano mkubwa sana wa kupata au kuingia database. Nikaenda dom kwa gari za IT za usiku asubuhi nikapiga pepa na kujishikiza kwa dogo UDOM hostel kusikilizia matokeo kesho yake ya kwenda usahili wa vitendo, nikaitwa na nikafanya na kurudi Dar kuendelea na mishe za saidia fundi na wakati mwingine fundi na kila aina ya kibarua ninachopata. Miezi mitatu baadae nikiwa nasafisha kiwanja cha mtu kwa kufyeka napigiwa simu ya "hongera, nimeona jina lako walioitwa kazini".
Kwasasa namshukuru Mungu kwa yote kwani kupitia mshahara niliweza kuboresha biashara, kuitanua na kufungua ofisi ya pili kubwa zaidi na kuwaajiri vijana wenzangu wasio na ajira nao wapambanie kombe na mama watoto kazi yake ni kwenda kukagua na kukusanya maokoto.
Msikate tamaa vijana wenzangu, ipo siku milango itafunguka. Pia omba Mungu umpate mwenza wakukustahimili wakati huu wa dhiki kwani huyo ndie atakayekupa moyo na nguvu ya kuvuka hiki kipindi