Mabadiliko ya Katiba ni lazima

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
270
TOKEA kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu mwezi Oktoba, kilio cha kutaka Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kimesikika kwa sauti kubwa zaidi na kilio kinazidi kuenea kila kona ya nchi yetu kikihusisha watu wa kada mbalimbali.
Kilio hiki kwanza kilianzishwa tena na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho kilidai matokeo ya mgombea wake wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano yalichakachuliwa na kikapeleka malalamiko yake Tume ya Uchaguzi lakini hakikusikilizwa.

Chama hicho kikalalamika kwamba Katiba haiwaruhusu kudai haki yao mahakamani ingawa kinao ushahidi kwamba haki hiyo ilipokonywa waziwazi. Ni katika mazingira hayo ambapo wabunge wa chama hicho waliamua kutafuta njia mbadala ya kufikisha malalamiko yao kwa umma wa Watanzania na jumuia ya kimataifa kwa kususia hotuba ya Rais wakati akifungua Bunge.

Tokea hapo kilio kimezidi kupanuka ambapo sasa kimepokewa na majaji wastaafu (mfano Jaji Manento), Jaji Mkuu aliyepo Augustine Ramadhan, Rais mstaafu Benjamin Mkapa, viongozi wa dini, wasomi na wanazuoni mbalimbali, wanaharakati, na wengineo wengi.

Sisi wa Tanzania Daima Jumatano kama sehemu ya Watanzania, tunapenda kuikumbusha serikali kwamba kilio cha Katiba mpya nchini hakikuanza leo. Ni cha muda mrefu ila kilio cha sasa sauti yake imepaa mno.

Tunawashauri viongozi wetu kusikia kilio hiki na kuanzisha mchakato wa Katiba mpya kwa kuwa kunyamaza kwaweza kuleta maafa makubwa. Katiba ambayo mbali na mapungufu yake mengine mengi, haimruhusu raia ama kikundi cha raia wema kudai haki yao kwenye chombo ambacho Katiba hiyo hiyo inakiita chenye kauli ya mwisho kwenye utoaji haki nchini, si Katiba nzuri ya kujivunia na kuendelea kuiwekea viraka.

Ipo siku itatusababisha wote tuingie kwenye maafa na si kiongozi wa serikali ama wa chama tawala ama raia wa kawaida atapona. Tuepusheni na nusu shari kabla ya shari kamili.

Tungependa kuwashauri viongozi, kutopuuzia madai hayo ili kuepuka kile kilichotokea kwa jirani zetu wa Kenya wakati wa kudai Katiba au katika nchi zingine barani Afrika ambako watawala hawakupenda mabadiliko ya Katiba.
 
Back
Top Bottom