Hebu cheki gazeti la habari leo kama naota vile,
BAADA ya kukaa mahabusu kwa siku 14, hatimaye Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, ameachiwa kwa dhamana.
Baada ya kutoka mahakamani wafuasi wa chama chake cha Chadema waliokuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha walimbeba huku wakiimba nyimbo mbalimbali za kukisifu chama hicho.
Lema alipata dhamana jana baada ya awali kukataa dhamana na kutaka kwenda mahabusu.
Siku chache baadaye uongozi wa juu wa Chadema ulifanya jitihada za kuhakikisha anatoka, lakini Novemba 7 Mahakama ilimnyima dhamana hiyo.
Hakimu Judith Kamala alisema dhamana ya Lema ipo wazi, hivyo wadhamini wake wahakikishe anafika mahakamani kadri kesi itakapopangwa na kama hatafika, basi wadhamini hao watoe taarifa.
Alikubali kumpa dhamana Mbunge huyo na kuahirisha kesi hiyo hadi Desemba 14, mwaka huu.
Lema anashitakiwa pamoja na wenzake 18 wakikabiliwa na kesi ya kufanya maandamano yasiyo halali.
Alidhaminiwa kwa kutolewa kwa barua mbili zenye vitambulisho na ahadi ya Sh 500,000 kila mmoja, ambapo Mwajuma Manonga na Sara Mohamed Kara walimdhamini Mbunge huyo.
Akitoka nje ya mahakama, alilakiwa na wafuasi wa chama hicho ambao hawakujali kama wapo ndani ya mahakama na kumbeba juu huku wakiimba nyimbo mbalimbali za kumsifu na kulibeza Jeshi la Polisi.
Shangwe hizo hazikuishia hapo, ziliendelea huku wakiwa wameshika matawi ya miti na majani na baadhi wakiwa wamembeba Lema na kuanza msafara kwenda ofisi za Chadema Mkoa zilizopo Ngarenaro na kusababisha baadhi ya benki kusitisha shughuli zao kwa muda na nyingine zikifanya kazi; huku ulinzi ukiimarishwa na Benki ya NMB Clock Tower ikifunga kwa muda kutokana na maandamano hayo.
Lema aliwaambia waandishi wa habari kwamba alikwenda mahabusu si kwamba alikosa dhamana, bali kuonesha namna ya kupinga unyanyasaji wa Polisi aliodai wanabambikia watu kesi hasa wa Chadema.
Alimgeukia Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, akimtaka aachane na siasa za Arusha kwani chimbuko la mgogoro wa Arusha ni umeya, hivyo akae chini kutatua tatizo hilo na si kutamka kuwa yeye ni RC hivyo ana wajibu wa kutuliza amani na utulivu.
Source
HabariLeo | Lema aachiwa kwa dhamana, wafuasi wambeba