Maandamano UVCCM yashtukiwa

Pilato

Member
May 29, 2008
60
1
Maandamano UVCCM yashtukiwa

*Ni yale ya kutaka bodi ya mikopo ivunjwe
*Yahojiwa mbona hawakuwatetea kupiga kura

Na Tumaini Makene,

MAANDAMANO yaliyoandaliwa na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) yakilenga
kuwajumuisha wanafunzi wa shule za sekondari na vyuo vya elimu ya juu nchini, yameshtukiwa yakielezwa kuwa ni mkakati kufunika udhaifu wa kushindwa kutekeleza ahadi ya kuwapatia wanafunzi mikopo.

Maandamano hayo ni yale yenye nia ya kutaka kuishinikiza serikali kuvunja Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini (HESLB), kwa kuondoa uongozi uliopo na kuiunda upya kwa madai kuwa imeshindwa kuwahudumia wanafunzi hao kulingana na mahitaji yao.

Baadhi ya wananchi, wadadisi wa masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi, wamesema kuwa huo ni mkakati wa UVCCM kutaka kurudisha imani ya kundi kubwa la vijana nchini, hususan wanafunzi, ambao wameonekana kuanza kuipa kisogo CCM na hata kuonesha kukerwa na mwenendo wa serikali yake, katika kushughulikia kero mbalimbali katika jamii.

Wiki iliyopita Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Bw. Beno Malisa alikubaliana na ombi la wanafunzi wa vyuo vikuu walio wanachama wa CCM mkoa wa Dar es Salaam juu ya kuitisha maandamano hayo.

Nia hiyo ilifuatia tamko la hivi karibuni la Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM lililosomwa Dar es Salaam, ambalo nalo lilisema kuwa tatizo la migomo ya wanafunzi wa elimu ya juu, moja ya sababu zake kubwa ni ukiritimba wa bodi ya mikopo, ukisema hauko tayari kuona hilo likiendelea, bali watendaji 'wapinduliwe' mara moja.

Tamko hilo la UVCCM taifa, lilijibiwa na HESLB, ambapo Mkurugenzi Mtendaji, Bw. George Nyatega, alisema vijana hao walitoa taarifa za 'uzushi na kukurupuka' bila kufanya uchunguzi wa kina juu ya chanzo cha migomo ya vyuo vikuu, huku akitaka bodi hiyo isigeuzwe 'jimbo la uchaguzi' na wanasiasa.

Akizungumza hali hiyo, mmoja wachambuzi mahiri wa masuala ya kisiasa na kijamii, Bw. Bashiru Ally ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Sayansi ya Siasa, alisema kuwa bodi ya mikopo ni dalili ya tatizo kubwa nchini kwa sasa.

Bw. Bashiru alisema kuwa ni vigumu kuzungumzia tatizo dogo bila kujikita katika suala la msingi, ili kupata majibu ya uhakika, badala ya 'majibu mepesi kwa matatizo magumu.'

"Unajua sekta ya elimu ina matatizo mengi tofauti tofauti ambayo yamekuwa yakiibuka kwa nyakati tofauti kwa sura tofauti, leo utasikia Dodoma wamegoma kwa sababu ya mishahara au wanafunzi kukosa fedha, au wanafunzi wengine wanapata kidogo kuliko wanavyohitaji.

"Lakini pia mfumo wa kutambua umaskini wa wanafunzi na kuwapata wanafunzi wahitaji bado ni tatizo kubwa hapa nchini...hivi kwanza unawekaje madaraja ya kuwatambua maskini katika nchi maskini kama hii. Hao wanaomudu kulipa kutokana na utajiri wao, wameupataje huo utajiri.

"Hata bodi ikivunjwa leo nini kinafuata...hata kama bodi ikipewa fedha...kwanza hizo fedha zinatoka wapi katika uchumi unaokufa huu. Uchumi huu unakufa...lakini bodi ya mikopo ni kiashiria tu cha mfumo mbovu ambao umewaparanganyisha watu," alisema Bw. Bashiru.

Huku akisema kuna kila haja ya jamii kukaa chini na kuutafakari ubepari, aliongeza kuwa mfumo huo ni chanzo cha jamii kuhangaika kila siku na suala moja baada ya jingine bila kupata majawabu yanayotosheleza kuhitimisha kila mjadala au kashfa inayoibuka.

Alisema Watanzania wamegeuka kuwa jamii ya watu wanaohangaika na 'kashfa na mijadala mipya' kila siku, bila kupata muda wa kujadili undani wa matatizo yao na kutafakari kwa kina nchi inakotoka, ilipo na inakoelekea.

Alisema vijana wote nchini bila kujali itikadi za vyama, wala kutumikia makundi ya watu wachache kwa maslahi ya muda mfupi, wanapaswa kuwa chachu ya kuibua mijadala ya kitaifa, juu ya msambaratiko wa kijamii kwa sababu ya kukumbatia mfumo aliouita wa kinyama, yaani ubepari.

"Vijana hawa wananishangaza kwani bodi ya mikopo ina-exist (iko) nje ya mfumo huu mbovu wa kinyama tulioamua kuukumbatia. Mbona wameshindwa kuwazungumzia wamachinga waliojaa barabarani au huko Kariakoo, wale si vijana wala hawana mwelekeo...wanapaswa kuwa chachu ya mjadala mpana wa kitaifa juu ya tatizo la msingi linalosumbua jamii.

"Tumekuwa watu wa ajabu, leo kashfa hii, kesho mjadala ule, tulikuwa na Dowans, mara matokeo ya kidato cha nne, hatujamaliza hilo ghafla watoto 10 wamekufa Mwananyamala, mara mauaji ya albino, mara wananchi huko Babati wamevamia mashamba, sasa wanasumbuana na polisi...yaani ni confusion (mkanganyiko) tu katika jamii.

"Ubepari ni mfumo ambao tayari umejionesha kwa sura halisi ya unyama, mfumo unaotoa fursa kwa kakundi kadogo kunufaika, huku kundi kubwa likibakia kuwa fukara, mfumo unaoua vijiji, ukiua hata kilimo kinachotoa ajira kwa wengi na kukuza miji, sasa ukikuza miji bila watu kuwa na ajira, unategemea nini.

"Sasa wanaonufaika wanaendelea kunufaika, maskini wanaendelea kuwa maskini...sasa katika mazingira ya nchi maskini kama hii unawapimaje maskini...wanafunzi sasa wanasoma wakiwa njaa, hawana uhakika wa malazi...mfumo wa kinyama unazalisha watu wanyama pia.

"Mfumo wa kinyama utazalisha watu watakaokuwa wanyama, kwa sababu wamesumbuka sana, unategemea wakija kuwa wabunge au wakuu wa wilaya, wataacha kujitengea mafao makubwa yanayozidi hata profesa kama ilivyo sasa! Haya ndiyo vijana kama UVCCM walipaswa kutafakari kabla ya kutoa tamko, nchi haitaendelea kwa watu kutoa matamko kwa malengo ya kisiasa.

Alitoa rai kwa vijana nchini na jamii kwa ujumla kuacha kutafuta majibu mepesi kwa mambo magumu ambayo yanahitaji mjadala na tafakuri inayoendana na muktadha wa kuangalia nchi inatoka wapi, iko wapi na inaelekea wapi.

"Hao UVCCM wote nawafahamu nimewafundisha hapa, wanafiki tu...mbona wamechagua bodi ya mikopo tu, mbona hawataki kushughulikia uchafu wa uchaguzi, watu walinunua kura, mbona hawazungumzii huko Babati wananchi wanahangaika sasa...mbona hawakutoa tamko juu ya vijana wenzao elfu sitini waliokosa haki ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu uliopita, hatukusikia.

"Waende kwenye Azimio la Arusha watapata majibu ya hayo mambo wanayotaka, wajifunze kutafakari kwa upana kabla hawajatoa matamko, matamko ya vyama mbalimbali hayatatusaidia, vijana wa chama hiki, mara wa chama kile, mpaka tutafakari kwa kina chanzo cha mparanganyiko wetu,

"Tatizo la bodi ni la kimfumo zaidi si kiutendaji...tusiangalie maslahi ya kiitikadi, wala makundi ya watu wachache...nchi hii ikisambaratika, itasambaratika na watu wote bila kujali ikitikadi zetu," alisema Bw. Bashiru kwa kirefu.

Akitumia uzoefu wa kuwa kiongozi wa wanafunzi kama waziri wa mikopo na baadaye waziri mkuu, Chuo Kikuu Dar es Salaam, Bw. Julius Mtatiro ambaye kwa sasa ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) alisema kuwa tatizo la mikopo nchini ni la kimfumo zaidi si bodi pekee.

Akiweka wazi kuwa bodi ya mikopo inayo matatizo yake, Bw. Mtatiro alisema kuwa kuna mambo mengi juu ya mfumo wa utoaji mikopo nchini hayawekwi wazi, hivyo katika hali ya kawaida ni rahisi kuisukumia bodi ya mikopo lawama zote juu ya matatizo yanayowakumba wanafunzi.

"Ninaposema mfumo namaanisha mfumo wa serikali, hapa UVCCM inatumika tu, tatizo ni serikali imeshindwa kubuni mbinu za namna ya kufadhili elimu ya juu, hata kwa kupitia bodi hiyo hiyo, kwa mfano hakukuwa na haja ya wanafunzi wote kupatia fedha zao Dar es Salaam, wala Mwanza au Morogoro wangeweza kupata fedha zao huko huko waliko.

"Hivi kwa nini watu hawajiulizi, kila bodi inapolalamikiwa kwa nini serikali huwa inakaa kimya, wanakaa kimya kwa sababu wanajua ukweli uko wapi, wanajua wakiwabwekea bodi, bodi watasema ukweli, mbona serikali kila siku wanakuwa wepesi kuzibwekea agents (wakala) zingine zinapoboronga.

"Kwa mfano kuna wakati serikali inafanya projection (makadirio) ya idadi ya wanafunzi itakaowakopesha kwa mwaka husika, inaweza kuweka elfu themanini, lakini ukifika wakati husika, wenye sifa stahili wako 140,000, bodi ya mikopo wanakwenda kimya kimya kuwaambia, serikali nayo kimya kimya inatafuta fedha," alisema Bw. Mtatiro.

Kwa maoni yanayotokana na uzoefu wa kushughulikia matatizo ya mikopo akiwa chuoni, alisema bodi ya mikopo inachangia asilimia 5 ya matatizo yaliyopo huku asilimia 95 zote zinachangiwa na serikali, akiongeza kuwa hiyo ndiyo sababu wanafunzi wengi huchelewa kupata fedha mpaka vyuo vinafunguliwa au 'wakati wa mwisho mwisho'.

"Tatizo ni ukosefu wa mbinu sahihi, serikali imeishiwa mbinu sasa wanawatumia UVCCM...wakishamaliza kuvunja bodi hii ambayo imeanza kupata uzoefu wataunda kitu kingine katika mfumo huo huo mbovu, serikali yenyewe iko kwenye matatizo makubwa ya fedha, kulipa Dowans na vitu vingine..." alisema Bw. Mtatiro.

Naye mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC), Sunday Charles, alisema kuwa kushughulika na bodi pekee, katika suala zima la mfumo wa utoaji mikopo nchini ni kutaka kufanya propaganda kwa manufaa ya kisiasa kwenye matatizo ya wanafunzi.

Alisema ni vigumu kuitofautisha bodi na serikali moja kwa moja, kwani pamoja na kwamba serikali kupitia bunge hupitisha bajeti za mikopo, kiuhalisia si fedha yote huenda bodi kwa wakati mwafaka, baada ya kupitia hazina.

"Cha kwanza lazima tutambue kuwa bodi wana-implement (wanatekeleza) matakwa ya serikali...bunge hupitisha bajeti za fedha za mikopo in terms of figures (mahesabu ya kwenye karatasi) lakini ki-uhalisia sio pesa inayopitishwa hufika yote bodi, hata hivyo kiasi kidogo hicho kinachopatikana bado hupitishwa hazina, na hazina pia hutoa pesa hizo kwa kibaba.

"Lakini kingine hakuna clear link (uhusiano wa wazi) kati ya management (uongozi) ya chuo na bodi ya mikopo, suala la mikopo manejimenti nyingi za vyuo zinalitazama kama ni mkataba wa mwanafunzi na bodi yenyewe...

"Tumewashtukia muda tuu, na kama ukitaka kuona kwamba ni propaganda ya kukamata wanafunzi wa elimu ya juu, kwa nini iwe ni mikopo tu, ili hali kuna matatizo makubwa nchini...kuna suala la Dowans wanapitia tuu juu juu, mgao wa umeme, kupanda kwa bei ya nishati ya umeme, gesi, wako wapi UVCCM, mbona hawasemi.

"Tatizo letu kwa sasa ni kupandishiwa pesa za kujikimu walau 5000 mpaka 10,000, hawasemi wao wanafumba watu macho eti tatizo ni bodi, UVCCM lazima watambue kuwa wanafunzi wa elimu ya juu wana-reason (wanatafakari)," alisema Bw.
Charles.

majira,feb,2011.
 
Back
Top Bottom