WanaJF:
Baada ya JKI kuingia madarakani miaka mitano iliyopita, mivutano baina ya vyama vya siasa vya upinzani na serikali (yaani polisi) kuhusu maandamano ilionekana kutoweka kabisa.
Wengi waliipongeza serikali ya JK kwa kuiondoa mivutano hiyo ambayo ilikuwapo kwa takribankipindi chote cha Mkapa. Itakumbukwa yule IGP Mahita daima alikuwa anavutana na wapinzani, wakati huo CUF (iliyokuwa na nguvu kubwa) kuhusu maombi yao ya kufanya maandamano.
Mahita aliibua ile kauli yake maarufu dhidi ya CUF: Kama nyie ngangari, basi mie ni ngunguri.
Askari wake walikuwa wanatembeza virungu dhidi ya wafuasi wa CUF na kuwaumiza vibaya, akiwemo hata mwenyekiti wao Lipumba ambaye aliwahi kuvunjwa mkono.
Miaka mitano ya JK tumeona maandamano yakiruhusiwa bila pingamizi na polisi wakiyalinda, na yalifanyika kwa amani, hadi watu wakafikia kusema; kumbe ni polisi ndiyo huwa wanaanzisha vurugu kwenye maandamano.
Baada ya uchaguzi huu tunaona tena hali ya wakati wa Mkapa na Mahita inaanza kujirudia polepole maandamano ya wapinzani hasa ya Chadema (chama cha upinzani ambacho sasa ndiyo chenye nguvu) yanakataliwa kwa sababu zisizo na msingi.
Tumeshuhudia kule Arusha wiki hii, maandamano ya Chadema yakikataliwa eti kwa kisingizio kwamba idara ya polisi haina askari wa kuyalinda huku ikipeleka kwenye uwanja wa mkutano askari kibao kwa lengo la kuyazuia maandamano.
Kulikoni serikali ya JK sasa? Inaogopa nini? Kwa nini isiendeleze tu sera yake ya awali ya kuyaruhusu maandamano na kuyalinda kama ilivyokuwa katika miaka yake mitano iliyopita?